Kila mkataba unatakiwa ukupe ulichokitarajia

Muktasari:

Haki kwa upande mmoja ni wajibu kwa mwingine. Endapo upande mmoja utatimiza wajibu wake na mwingine ukaacha, hapo ndipo kuvunjika kwa mkataba kunapoanza.

Mkataba wowote unatoa haki na kubainisha wajibu wako. Kila mtu anapoingia mkataba anatarajia kutimiza wajibu wake na mwenzake akifanya hivyo ili kila mmoja apate haki yake.

Haki kwa upande mmoja ni wajibu kwa mwingine. Endapo upande mmoja utatimiza wajibu wake na mwingine ukaacha, hapo ndipo kuvunjika kwa mkataba kunapoanza.

Sheria inaeleza kwamba wadau wa mkataba ni lazima watimize wajibu au ahadi zao isipokuwa tu kama wajibu huo umekatazwa au kuzuiliwa kisheria.

Kabla ya kutafakari namna ya kupata haki zako ni muhimu kutambua wajibu wako. Kufanya hivi ni muhimu ukasoma na kuelewa kila kipengele kinachohusiana na wajibu wako ili ujue utakavyotimiza.

Usiiishie kutambua wajibu wako bali na wa upande mwingine ili ujue utambana vipi kwani kadri atakavyotimiza wajibu wake ndivyo utakavyopata haki zako na kinyume chake.

Kutotimizwa kwa wajibu kwa upande mmoja husababisha kuvunjika kwa mkataba. Kumbuka, mkataba unaweza kumalizika kutokana na kupita kwa muda wa utekelezaji, kupitishwa kwa sheria mpya au agizo la Serikali linalokataza mkataba huo, kifo cha mmoja wenu, na kufirisika au kufungwa kwa taasisi iliyo ingia mkataba.

Mkataba pia waweza kuvunjika kutokana na tukio lisiloweza kuzuilika kama vile mafuriko, ajali, kimbunga, moto au namna yoyote ambayo mwanadamu hawezi kuizuia.

Kabla hujaingia kwenye mkataba wowote, jambo muhimu na la msingi unalopaswa kufanya ni kuhakikisha umesoma kwa makini na kuelewa kila kipengele kilichopo katika mkataba huo.

Kama lugha iliyoandikwa inakutatiza ni bora ukaomba msaada kwa watu wenye uelewa wa jambo hilo kuliko kujifanya umeelewa kumbe ulichokielewa sicho.

Usikubali kusaini mkataba ambao hujui kilichoandikwa kwa sababu wakati utakapotaka kujua kilichoandikwa yumkini ukawa umeshachelewa.

Hata kama aliyeandika huo mkataba una mwamini kiasi gani, tafadhali chukua muda wa kutosha kuupitia kabla hujausaini. Muda unaodhani unauokoa sasa, unaweza kuja kuupoteza baadaye, tena mara nyingi zaidi mkataba huo utakapokuja kukugeuka.

Unapoingia mkataba wowote, ni muhimu uhakikishe unaelewa kila kipengele kilichomo. Mikataba mingine hutekelezwa kwa kipindi maalumu hivyo hakikisha unatimiza wajibu wako ndani ya muda husika uliotajwa.

Unapaswa kuwa mlinzi wa mwenzako kuhakikisha kila kipengele cha mkataba kinafuatwa na kutekelezwa ipasavyo.

Mkataba ukivunjwa, una haki ya kulipwa fidia. Sheria inaeleza endapo mtu au taasisi utakayoingia nayo mkataba itavunja mkataba huo, inapaswa ikulipe.

Hii ni kwa pande zote mbili, yaani, endapo upande mmoja utavunja mkataba, aliyevunja anawajibika kisheria kumlipa aliyeingia naye mkataba, fidia ya hasara yoyote itakayojitokeza kutokana na kuvunjwa kwa mkataba huo.

Ikiwa kiwango cha fidia ambacho aliyevunja mkataba anatakiwa kulipa kitakuwa kimeelezwa kwenye mkataba, malipo yanapaswa kuwa yaliyoelezwa tu. Hii ni endapo tu yule aliyepata hasara ataweza kuthibitisha hasara au madhara aliyoyapata kutokana na kuvunjwa kwa mkataba huo. Inaruhusiwa kisheria kuongeza riba ambayo utataka ilipwe kuanzia siku ya kuvunjwa kwa mkataba.

Kitu muhimu ni kuwa makini kuanzia wakati wa kusaini mkataba ili upate fidia stahiki endapo uliyeingia naye mkataba ataamua kuuvunja kinyume na matakwa ya sheria.

Kukokesekana kwa umakini kuanzia mwanzo husababisha majuto tena baada ya kupata hasara.