Friday, July 13, 2018

Mambo ya kuzingatia kwa mfanyakazi kabla ya kuchukua mkopo

 

By Gidion Obeid, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Kukopa si jambo baya, ila mkopo unaweza kukuadhiri usipokopa kwa busara. Wafanyakazi wengi wamekopa tayari au wana mpango wa kukopa siku zijazo.

Dada yangu anayefanya kazi kwenye shirika moja serikalini nilimsikia akisema hatakopa tena.

Kauli hii ilinifanya niwaze, inawezekana ameona maumivu ya mkopo na amedhamiria kutokurudia kosa.

Mkopo mzuri ni ule ambao utaongeza ubora wa aina ya maisha unayoishi. Maana yake ni kwamba, uzuri wa mkopo unaupima kwa kuangalia ni jinsi gani utakupunguzia umaskini kwa kukuongezea kipato.

Kama mkopo umekufanya uwe maskini zaidi ya ulivyokuwa kabla ya kukopa, mkopo huo ni mkopo mbaya.

Taasisi nyingi za kifedha zinazofanya biashara ya kukopesha zinalenga kuwapata wafanyakazi kwa sababu vipato vyao vinatabirika na pia ni rahisi kukata marejesho moja kwa moja kwenye mshahara. Kwa sababu hiyo, wanatumia njia mbali mbali kuwashawishi wafanyakazi wakope. Jihadhari usikope kwa sababu umeshawishiwa au kwa tamaa ya kupata fedha nyingi kwa mkupuo.

Tafakari ya kutosha inahitajika kabla haujaamua kukopa.

Ukielewa mambo yafuatayo kabla ya kukopa, yatakusaidia kukwepa mikopo ambayo itakuongezea umaskini.

Kuwe na sababu za msingi za kukopa

Ni vema kuamua sababu za kukopa kabla haujakopa. Usikope kwa sababu una fursa ya kukopa, bali kwa sababu unaweza kutumia vizuri kile utakachokikopa. Lazima ujiulize, ‘kwanini ukope’.

Wakati ni kawaida kumuona mfanyabiashara anakopa ili kuongeza uzalishaji na mauzo kwenye biashara yake, mara kadhaa wafanyakazi wamekuwa wakikopa kwa ajili ya shughuli ambazo haziongezi kipato.

Siyo sahihi kukopa ili ukafanikishe sherehe ya harusi.

Kusudi la mkopo mzuri inatakiwa iwe kuongeza uzalishaji au mauzo ili kipato kiongezeke.

Pia, unaweza kukopa ili kupunguza gharama za maisha. Kopa ili uongeze mtaji wa biashara na hatimaye kuongeza kipato, au kopa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ili kupunguza gharama za kodi.

Si vizuri kukopa ukaanze biashara usiyokuwa na uzoefu nayo. Hatari ya kupata hasara kwenye biashara inayoanza ni kubwa zaidi kuliko kwenye biashara ambayo imeishakuwepo kwa muda fulani.

Usikope mikopo inayoongeza gharama za maisha ambazo hautaweza kuzimudu. Namjua mfanyakazi aliyekopa ili anunue gari, sasa hivi analalamika hana hela za kununua matairi na mafuta baada ya miezi mitatu tu toka amelinunua.

Siku hizi gari analiacha nyumbani anaenda kazini kwa daladala. Unaweza ukawa maskini mwenye gari, kopa kwa busara.

Kopa kwa riba nafuu

Riba ni kodi anayokutoza mkopeshaji kwa kukuazima fedha zake kwa muda fulani. Ni kiasi cha ziada anachokilipa mkopaji juu ya kile kiasi alichokikopa.

Ukokotoaji wa riba huwa ni mgumu kueleweka kwa watu ambao hawana taaluma ya uhasibu au usimamizi wa fedha. Kwa sababu hiyo, unaweza ukakopa sehemu ambayo riba yake ni kubwa wakati ulikuwa una fursa ya kukopa kwa riba nafuu.

Asilimia ni sehemu ndogo tu ya ukokotoaji mzima wa riba.

Hivyo, asilimia siyo kigezo pekee kinachoweza kukusaidia kugundua riba nafuu.

Inawezekana kabisa mkopeshaji anayedai riba ya asilimia 10, ndiyo akawa ana riba kubwa kuliko mkopeshaji mwingine anayedai riba ya asilimia 12.

Namna rahisi ya kutambua mkopeshaji ambaye riba zake ni nafuu, ni kuwauliza wakopeshaji wote swali moja linalofanana. Uliza swali kama hili, kama nikikopa Sh1,000,000 kutoka kwako, kwa kipindi cha mwaka mmoja, marejesho kwa mwezi mmoja yatakuwa shilingi ngapi?

Baada ya kupata majibu ya swali hilo, linganisha kiasi cha marejesho. Anayekudai riba nafuu ni yule atakayekuambia kiasi cha marejesho kidogo zaidi kuliko wengine.

Kinachobaki kwenye mshahara baada ya makato kikutosheleze

Usikope zaidi ya uwezo wako wa kulipa. Nilisikitika kusikia habari za wafanyakazi waliompa mkopeshaji kadi zao za benki ili aweze kuchukua mshahara wote mara tu utakapowekwa kwenye akaunti.

Mshahara wote ukiishia kwenye kulipa madeni itakufanya uishi maisha ya shida na wala usifurahie matunda ya kazi yako.

Kiasi cha mshahara kinachobaki baada ya makato yote inashauriwa kisiwe chini ya theluthi moja ya mshahara ghafi (mshahara kabla ya makato yoyote).

Yaani kama mshahara ghafi ni sh. 300,000, inashauriwa ubaki na siyo chini ya sh. 100,000. Ukiwa na baki inayozidi hiyo ni bora zaidi.

Mkopo usikufanye ushindwe kujihudumia mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi na malazi. Utu wako usidhalilike kwa ajili ya mikopo.

Ni vema kutathimini kama kiasi kinachobaki baada ya mkopo kinakutosheleza.

Elewa pia kuhusu muda wa kurejesha mkopo na gharama zingine za mkopo.

Muda utakaoutumia kulipa mkopo unachangia kwenye ukokotoaji wa kiasi cha marejesho ya kila mwezi. Jinsi muda wa kurejesha unavyoongezeka ndiyo jinsi kiasi cha marejesho kinavyopungua. Pia muda ukiwa mrefu unaweza kukopa mkopo mkubwa zaidi, kwani urejeshaji wake pia ni wa muda mrefu.

Jinsi mkopaji anavyoendelea kukaa na hela za mkopeshaji riba atakayoilipa kwa ujumla itakuwa kubwa zaidi. Hii ni kwa sababu mahesabu ya riba yanafanyika kwa mwaka, hivyo kwa kila mwaka unaondelea kukaa na fedha ya mkopeshaji utaulipia riba.

Pia, jinsi unayoendelea kuchelewa kumaliza deni ndivyo unavyochelewa kukopa tena kama una mpango huo. Ukimaliza deni mapema utaweza kukopa tena.

Kwenye mikopo huwa kuna gharama za bima na wakati mwingine kuna gharama za kuuandaa mkopo wako. Hizi gharama ni tofauti na riba utakayolipa na huwa zinajumlishwa kwenye mkopo, au zinapunguzwa kwenye kiasi cha jumla utakachopewa kama mkopo.

Ni vyema kumuuliza mkopeshaji akufafanulie kuhusu gharama zote zinazohusiana na mkopo kabla ya kukopa.

Gidion Obeid ni Mhadhiri wa Uhasibu na Usimamizi wa Fedha, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na mwanafunzi wa Shahada za Uzamivu (PhD). Kwa ushauri wasiliana naye kwa namba 0625698050

-->