‘Mastaa’ 11 wa kigeni waliopotea Ligi Kuu

Timu mbalimbali za Ligi Kuu zimesajili wachezaji wengi kutoka nje ya nchi, wengine wakifanya vizuri na wengine wakishindwa kuwika.

Baadhi ya wachezaji hao wameshuka viwango kwa sababu mbalimbali ikiwemo ushindani wa namba na wengine kuwa majeruhi wa muda mrefu. Hii ni orodha ya baadhi ya wachezaji hao.

Klaus Kindoki Yanga (DR Congo)

Amesajiliwa msimu huu akichukua nafasi ya Mcameroon,Youth Rostand. Hata hivyo kipa huyu kutoka DR Congo hajaweza kuonyesha kiwango ambacho mashabiki wa Yanga walitarajia na mara kwa mara amekuwa akiambulia maneno makali kutokana na kiwango duni.

Alianza katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Stand United na kupigwa mabao matatu, Yanga iliposhinda 4-3, pia alianza dhidi ya Mwadui na kuruhusu bao la kusawazisha lililomkasirisha Kocha Mwinyi Zahera na kuamua kumtoa wakati wa mapumziko. Kindoki aliangua kilio baada ya kutolewa akijutia makosa yake.

2.Nicholas Gyan- Simba (Ghana)

Huu ni msimu wake wa pili akiwa Simba. Alisajiliwa kama mshambuliaji wa pembeni akitokea Ghana, lakini kocha aliyeondoka, Mfaransa Pierre Lechante alimbadilisha namba na kumchezesha kama beki wa kulia.

Msimu huu ameshindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na uwepo wa beki Shomari Kapombe, aliyekuwa katika kiwango bora kabla ya kuumia. Athari ya kusugua benchi ilimuathiri beki huyo ambaye alicheza chini ya kiwango katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mbabane Swallows.

3.Ennock Atta- Azam (Ghana)

Ni winga lakini pia anamudu kucheza nafasi ya beki wa kushoto ni mmoja ya wachezaji wazuri katika kikosi cha Azam, lakini ushindani wa namba umekuwa ukimuweka benchi kwa kuwa siyo chaguo la Kocha Hans van der Pluijm.

4.Elisha Muroiwa-Singida United (Zimbabwe )

Beki huyo kutoka Zimbabwe amekuwa na wakati mgumu kupata nafasi ya kucheza mbele ya wabongo Kennedy Juma, Salum Kipaga na Salum Chuku ambao wanafanya kazi nzuri uwanjani. Uwepo wa idadi kubwa ya mabeki wenye uwezo wa kukaba, umemfanya Mzimbabwe huyo kusugua benchi muda mrefu.

5.Daniel Amoah- Azam (Ghana)

Nafasi yake hasa ni beki wa kati lakini pia humudu kucheza upande wa kulia. Aliachwa na Azam msimu huu kutokana na majeruhi ya kifundo cha mguu yaliyomuandama kabla ya kupelekwa Afrika Kusini kufanyia upasuaji. Hata hivyo, baada ya kupona na Azam kuona maendeleo yake mazuri imetangaza kumrejesha katika usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufungwa Desemba 15.

6.Thabani Kamusoko- Yanga (Zimbabwe)

Ungesema nini kuhusu kiungo huyo miaka miwili iliyopita kwa jinsi alivyokuwa fundi uwanjani.Ndiyo yeye aliyesababisha kuanza kwa msemo wa ‘kampa kampa’ tena. Hata hivyo majeruhi ya muda mrefu ya goti yamemfanya apoteze namba na kusugua benchi mbele ya kijana Feisal Salum ‘Fei Toto’.

7.Diaby Amara- Singida United (Ivory Coast)

Amekuwa akipata nafasi mara chache ya kucheza, lakini hajaonyesha kiwango kama ilivyotarajiwa na wengi. Amara Amekuwa na wakati mgumu kuwania namba dhidi ya Habib Kiyombo, Lubinda Mundia, Tibet John, Eliuter Mpepo na Ally Ng’anzi.

8.Haruna Niyonzima- Simba (Rwanda)

Kati ya viungo waliokuwa kivutio katika soka la Tanzania ni Niyonzima. Nahodha huyo wa zamani wa Rwanda, alikuwa akipiga pasi zenye macho, alikuwa na vitu vingi mguuni mwake.

Nguli huyo alicheza Yanga kwa mafanikio kwa misimu minne kabla ya kutua Simba, lakini mambo kwa upande wake yamekuwa magumu kwa kuwa hapati nafasi ya kucheza mbele ya kiungo Mzambia Clatous Chama.

9.Amissi Tambwe- Yanga (Burundi)

Mmoja wa washambuliaji bora wa kigeni nchini aliwahi kuibuka mfungaji bora mara mbili msimu wa 2013/2014 akiwa Simba na msimu wa 2015/2016 akiitumikia Yanga.

Tangu msimu uliopita hakuwa katika kiwango kizuri kutokana na majeraha ya goti yaliyomuweka nje kwa muda mrefu.

Msimu huu amerejea lakini bado hajakuwa katika ubora wake licha ya wiki iliyopita kuipa ushindi wa mabao 3-1 Yanga dhidi ya Prisons yeye akifunga mabao mawili.

10.Alex Kitenge- Stand United (Burundi)

Mshambuliaji huyu wa Burundi amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka. Alionekana kuja vizuri baada ya kuifunga Yanga mabao matatu peke yake katika mchezo ambao Stand United ilikubali kipigo cha mabao 4-3.Hata hivyo tangu aifunge Yanga amepotea na hajawika tena huku akijitetea kuwa mabeki wanamkamia.

11.Donald Ngoma- Azam (Zimbabwe)

Alisajiliwa Yanga msimu wa 2016/2017 na aliuwa akiwalaza na viatu mabeki wengi kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na aksi yake uwanjani.

Msimu uliopita hasa mzunguko wa pili hakuichezea Yanga mechi nyingi kutokana na kuwa majeruhi ya goti na msimu huu akaibukia Azam iliyo chini ya kocha wa zamani wa Yanga Hans Pluijm.

Bado hajaonyesha makali yake kama wakati akiwa Yanga licha ya kwamba mpaka sasa ameifungia Azam mabao matatu kwenye ligi.