Mfugaji bora ni yule anayemjua kuku wake

Muktasari:

Lengo la makala haya ni kuweka mambo wazi kila mfugaji ajue jinsi ya kutunza kuku wenye kutaga kwa wingi.

Karibu tena kwenye makala kuhusu hatua za kupata mayai kabla hujaingia bandani kuyaokota. Ni elimu bora kwa mfugaji kujua namna gani mayai hutengenezwa kwenye mwili wa kuku kabla hajataga.

Lengo la makala haya ni kuweka mambo wazi kila mfugaji ajue jinsi ya kutunza kuku wenye kutaga kwa wingi.

Kimsingi, sio wafugaji wote wanajua mayai yanavyotengenezwa kwenye mwili wa kuku, japo idadi kubwa ya wafugaji wana mwanga fulani katika mambo mengi kwenye ufugaji.

Kwa mfano, kujua namna gani tumbo la kuku linazalisha mayai, ni hatua muhimu kwenye harakati za mtu kuwa mfugaji bora.

Tumbo la kuku ndiyo kiini cha mradi katika shamba la kuku wa mayai. Uzalishaji wa mayai unategemea hali ya afya ya mfuko wa uzazi wa kuku.

Mfugaji anatakiwa kufuga kwa lengo la kumfanya kuku atage mayai mengi. Lishe duni na magonjwa ya mara kwa mara kwa kuku, ni kuharibu ubora wa mfuko wa uzazi wa kuku anayetaga.

Ushauri wangu kwa wafugaji ni kuwa magonjwa mengi ya kuku yanatokana na mazingira wanayoishi kuku. Hali ya usafi wa banda au uchafu wa banda ndiyo sababu ya afya nzuri au mbya kwa kuku wako.

Ukiondoa uchafu wa kimazingira, lishe na huduma zingine za kiusimamizi huchangia uzalishaji kuwa mzuri au mbaya pia.

Hivyo ni vizuri kuchagua kuwa mfugaji bora kwa kuweka sawa mambo yote muhimu katika mahitaji ya kuku.

Kwa upande mwingine, mfugaji anaweza kufahamu mambo mengi katika ufugaji lakini kuna mambo mengine mengi hayajui.

Kutofahamu huko humfanya ashindwe kushughulikia ipasavyo matatizo yanayojitokeza shambani kwake.

Yajue mambo haya

Mambo matatu anapaswa mfugaji kujua kuhusu kuku. Moja, kuku ana ovari ya upande mmoja pekee kwenye mji wa uzazi inayofanya kazi.

Kuku anapotoka kwenye yai hukua akiwa na ovari zote mbili kulia na kushoto, lakini akifikia umri wa kuzalisha mayai ovari ya kushoto ndiyo hukomaa na kufanya kazi. Kwa hiyo mfugaji anatakiwa kujua kuwa kuku sio sawa na wanyama wengine kama vile ng’ombe, mbuzi na wengineo, ambayo matumbo yao ya uzazi hutumia ovari mbili kulia na kushoto ambazo hupokezana kutengeneza mayai.

Kutokana na sababu hiyo ya kuku kuwa na mfuko wa upande mmoja unaofanya kazi, hawezi kuzalisha mayai mawili kwa wakati mmoja kama ambavyo hutokea kwa wanyama wenye ovari mbili kuzaa pacha kwa kutumia ovari zote mbili.

Pacha wanaoweza kutokea kwa kuku ni yale ya yai moja kugawanyika ndani kwa ndani na kutengeneza viini viwili. Mgawanyiko huo wa yai unaweza kusababisha yai moja kutoa vifaranga wawili, lakini sio kuku mwenyewe kutoa mayai mawili yanayojitegemea kwa wakati mmoja.

Jambo hii huleta utata kwa watu wengi na wafugaji wengi kushindwa kujua kuwa kuku anataga yai moja tu kwa siku au zaidi?

Ukweli ni kwamba; mfumo wa uzazi wa kuku umeumbwa kufanya kazi moja baada ya nyingine; hivyo kalenda ya kuku pamoja na ndege wengine hutengeneza yai moja baada ya yai lililotangulia kutagwa. Hivyo kuku hawezi kutaga mayai zaidi ya moja kwa siku.

Pia sio rahisi kutokea kuku akawa na ovari zote mbili kulia na kushoto zinazotoa mayai. Endapo ovari ya kushoto ikiharibika kabla kuku hajaanza kutaga, ovari ya kulia inaweza kukomaa na kufanya kazi kama kawaida.

Jambo la pili asilolijua mfugaji ni kwamba; kuku akimaliza kutaga yai ndani ya dakika 30 hadi saa moja, mrija wa uzazi hufungua njia ya yai lingine kuanza kutengenezwa.

Hata hivyo, hilo linaweza lisitokee endapo kuku atakuwa ametaga muda wa jioni kuelekea usiku.

Kwa mfano, kuku anayetaga yai jioni ya saa tisa na kuendelea, mara nyingi mfuko wa uzazi hushindwa kufungua njia ya yai lingine kuanza kutengenezwa, badala yake husubiri hadi kesho yake mwanga wa jua umchangamshe na kisha njia kufunguka.

Kumbuka makala zilizopita zilisisitiza juu ya kuwa mwanga wa ziada kwa kuku wanaotaga angalau saa nne baada ya saa 12 za mwanga wa jua, ili homoni za kuzalisha mayai kwa kuku ziendelee kufanya kazi.

Homoni zinazoratibu uzalishaji wa mayai kwenye mwili wa kuku, hufanya kazi vizuri kuku akiwa macho.

Jambo la tatu lisilojulikana kwa mfugaji ni kwamba; kuku huchukua saa 25 hadi 26 kutengeneza yai na kutaga.

Sehemu ya kwanza kutengenezwa kwenye yai ni kiini cha njano ambacho hukuzwa na kuwa kikubwa. Tangu kuku akiwa kifaranga huwa anavyo vingi tayari kwenye ovari.

Sehemu ya pili inayoongezwa juu ya kiini hicho cha njano ni ute mweupe ambao yai likichemshwa ute huo hushikana na kuonekana kama sehemu ya ndani ya nazi inapovunjwa. Sehemu inayofuata ni mfano wa karatasi nyepesi ambayo hushikana na ganda gumu la nje.

Kila sehemu ya yai ina sehemu maalumu katika mlija wa uzazi wa kuku kutengenezwa. Sehemu zote za yai hutengenezwa kwa muda mfupi isipokuwa ganda la nje ya yai ambalo huchukua muda mwingi kuliko vyote.

Pia, ganda la nje ya yai hutumia madini mengi kuliko sehemu zote kwenye yai na huchukua saa 18 na zaidi kutengenezwa.

Upungufu wa madini ya kalshiamu na fosforasi husababisha kuku watage mayai yasiyo na ganda gumu.

Mayai mengi utakuta yametagwa yakiwa kwenye kikaratasi chepesi bila ganda gumu. Kuku wenye matatizo ya kutaga mayai laini mara kwa mara, hupatwa na shida ya kulemaa miguu na kushindwa kutaga kwa kukosa nguvu ya kusukuma yai wanapotaga.

Ili kutatua tatizo hili, boresha chakula chako upande wa madini.