‘Mhandisi wa mtaani’ mwenye ndoto ya kuanzisha chuo cha ufundi

Muktasari:

  • Ni mtundu wa kutengeneza vitu mbalimbali. Anakumbukwa na wengi kwa kuwahi kutengeneza helikopta kabla ya kusitisha mchakato wake kufuatia tangazo la Serikali

Hakuna mtaa nchini usio na kitu mithili ya karakana ndogo. Kama sio banda la mafundi wa kuchomelea vyuma, basi litakuwa banda linalowasitiri mafundi seremala.

Hapo bado hujazungumzia mafundi gari na gereji zao mitaani, mafundi baiskeli na sasa mafundi wa pikipiki na bajaji.

Humu mwote wanapatikana mafundi wakiwamo mabingwa wa fani zao. Hata hivyo, usiwaulize kama wana vyeti kwa kusomea katika mifumo rasmi au la.

Miaka nenda rudi, mafundi hawa hodari wanafanya kazi hizo na kuwa wataalamu wa kuaminika kwa jamii zinazowazunguka.

Ni katika kundi hili la mafundi wa mitaani, ndipo unapokutana na Adam Kinyekile, kijana mtundu anayesema ufundi na ubunifu wa vitu vimo ndani ya damu yake.

‘’Sikusukumwa na kitu chochote kuwa mbunifu ila ubunifu na uvumbuzi ni vitu ambavyo vipo kwenye damu; yaani nikiwaza kitu nisipokifanya naweza kukosa usingizi hata mwaka, lazima nikifanye ndipo niwe huru, anasema Kinyekile anayeendesha shughuli za ufundi Tunduma mkoani Songwe.

INAENDELEA UK 14

INATOKA UK 13

Anasema tangu aanze shughuli za ubunifu ama anaunda vitu vipya au amekuwa akitengeneza vitu vipya kwa kutumia vifaa vilivyotengenezwa na wengine.

Mhandisi wa mtaani

Anajiita mhandisi wa mtaani kwa kile anachosema kuwa hana elimu rasmi inayoweza kumtambulisha katika dunia ya wahandisi wa aina yake. Lakini ameamua kujiita kama ujumbe kwa jamii kuwa ili mtu awe mhandisi sio lazima awe na elimu ya chuo kikuu.

‘Elimu yangu ni darasa la saba. Ninaamini wahandisi wengi wanasoma vitu ambavyo vimebuniwa na watu ambao hawajasoma kokote. Hawa wanabuni vitu kisha kuviweka kwenye maandishi na ndipo watu wanasomea na kuitwa wahandisi,’’ anaeleza.

Kinyekile ana orodha ya vitu alivyotengeneza kwa kutumia utundu wa kiufundi unaoamwezesha kukusanya vifaa mbalimbali na kutengeneza vitu anavyovitaka. Amewahi kwa mfano kukusanya vifaa na kutengeneza mfano wa helikopta kabla hajazuiliwa kuendelea na mpango wake.

Moja ya mashine anayojivunia nayo ni ile anayoiita kwa jina la Mr Mazingira inayoweza kufanya kazi kadhaa kwa tofauti.

‘’ Mashine hii ina uwezo wa kufanya kazi nyingi kwa wakati tofauti. Kwa mfano, inaweza kulima,inavuta maji, inapukuchua mahindi gunia 1,000 kwa saa, inapukuchua karanga, maharage na kusaga chupa za plastiki, magunzi ya mahindi na taka za kwenye madampo aina zote isipokua chuma,’’ anaeleza.

Utundu wake haujaishia hapo, ametengeneza kile anachokiita karakana au gereji inayotembea. Hili ni gari lenye mitambo ya kila aina, huku ikiwa na uwezo wa kuchaji betri za magari, huduma za upepo na uchomeleaji na ukataji wa vyuma.

Alianzaje?

Kinyekile anasimulia: ‘’Safari yangu ya ubunifu niliianza nikiwa Mafinga katika gereji ya bosi wangu. Nilianza na vitu vidogovidogo kama viti, stendi za majiko, meza za kujipambia na vinginevyo. Nilitamani kufanya vitu vingi, lakini sikuweza kwa sababu nilikua chini ya gereji ya mtu. Hata hivyo, nilikua na ndoto kuwa ipo siku nitakuwa na gereji yangu na nitafanya vitu vikubwa zaidi.Na kitu cha kwanza kabisa kubuni nikiwa kwenye ofisi yangu ilikua ni karakana inayotembea.’’

Matarajio yake

Ndoto zangu natamani sana kuanzisha kiwanda cha aina mbalimbali za mashine,lakini pia kuwa na chuo cha ufundi ambacho hakita bagua elimu ulio nayo

Kwa sasa anajivunia kupokea wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali wanaokwenda katika karakana yake kujifunza masuala ya ufundi.

‘’Wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya ufundi wanakuja katika mafunzo kwa vitendo. kwa mfano, wanafunzi kutoka Veta Songea, Mikumi, Mbeya, Chuo cha Usafirishaji, Makongo JWTZ, Chuo cha ufundi Mbalizi, Kihumbe na vinginevyo. Ni wengi walionufaika na maarifa yangu,’’ anasema.

Akisifia kuwasaidia watu zaidi ya 300 waliopitia kwenye mikono yake, Kinyekile anasema kwa sasa yuko mbioni kutengeneza chombo mithili ya bajaji kitakachotumia umeme unaojizalisha wenyewe huku kikiwa na uwezo wa kubeba abiria wanne.

Azuiwa kutengeneza helikopta

Kama unakumbuka mbunifu huyu aliwahi kuwakuna watu wengi baada ya jaribio lake la kutengeneza helikopta. Hata hivyo, anasema amesimamisha mradi huo kwa kile anachokieleza kama kuzuiwa na Serikali.

Serikali ilitoa tangazo kupitia gazeti la Mwananchi Julai 2016 kwamba nchi hii bado haijawa na wataalamu wa kutengeneza ndege, hivyo ikatoa wito kwa watu binafsi na taasisi kusitisha shughuli zote za utengenezaji wa ndege. Kwa tangazo hilo nilivunjika moyo na kulazimika kusitisha maono yangu, anasema Kinyekile ambaye sasa yuko mbioni kutengeneza bajaji itakayoweza kuchukua abiria wanne.

Serikali na msaada kwa wabunifu

Kinyekile haridhiki sana na msaada anaoupata kutoka serikalini, licha ya kusifu jitihada za uongozi wa Mkoa wa Songwe kumkutanisha na wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Costech walinitembeza Shule ya Ufundi Arusha na kiwanda cha Nyumbu. Pia walinialika kwenye mkutano wao mmoja ambao nao sikuweza kuufaidi kwani walikua wanatumia lugha ya Kiingereza ambayo mimi sikuielewa, ‘’ anaeleza.

Anaongeza: ‘’Tanzania ina watu wengi wenye vipaji mbalimbali ila Serikali inashindwa kuwatambua na kuwatumia kwa ajili ya maendeleo ya nchi.Nchi za wenzetu wametumia rasilimali watu wenye ubunifu kufanikiwa. Sijui tunakwama wapi.’’

Wasifu

Kinyekile alizaliwa mwaka 1981 katika Wilaya ya Mafinga mkoani Iringa. Alisoma na kuishia darasa la saba mwaka 1997; hakuweza kuendelea na masomo ya sekondari kwa sababu ya uwezo mdogo wa wazazi wake. Ndipo alipoamua kujiingiza kwenye shughuli za ufundi kuanzia mwaka 1998 mpaka sasa.