Mitizamo ya kiuchumi kuhusu vita vya biashara

Kati ya mijadala mikubwa ya uchumi wa dunia mwaka huu ni pamoja na dhana ya vita vya biashara. Mjadala huu umedumu kwa muda kati ya Marekani na China.

Kwa juma la pili la mwezi wa nane 2018 mjadala kuhusu vita vya biashara umeibuka kwa kasi kati ya Marekani na Uturuki. dhana ya vita vya biashara sio mpya sana kwa wanaofuatilia biashara na uchumi wa kimataifa. Hata hivyo bado wapo wengi wasiofahamu baadhi ya masuala ya msingi katika dhana hii. Makala haya yanajikita katika kuelezea mitizamo kadha wa kadha kuhusu dhana hii ya vita vya biashara.

Uelewa wa dhana

Dhana ya vita ya biashara inatumika kueleza hali ya nchi moja kuwa katika ugomvi unaopelekea kutumia mbinu za biashara ya kimataifa kujaribu kuiadhibu nchi nyingine.

Sababu za ugomvi zinaweza kuwa za kibiashara na uchumi. Hata hivyo huweza kuwa sababu zisizo za kibiashara. Nchi husika hutumia mbinu kadhaa za kudhoofisha biashara ya kimataifa katika nchi moja, mbinu hizi ni pamoja na za kuongeza kiwango cha ushuru wa forodha. Mbinu nyingine sio za ushuru wa forodha.

Hizi ni pamoja na kupunguza au kuzuia kabisa kiasi cha bidhaa zinazotoka nchi husika kuingia katika nchi inayoanzisha vita hii.

Mifano ya nchi

Kati ya nchi ambazo zimekuwa katika vita vya biashara katika mwaka 2018 ni pamoja na Marekani kwa upande mmoja na China kwa upande mwingine. Vita hii imechukua sura ya Marekani kuongeza ushuru wa forodha kwa baadhi ya bidhaa kutoka China zinazoingia Marekani. Kati ya bidhaa hizi ni chuma.

Katika juma la pili la mwezi wa nane 2018 nchi iliyojikuta katika hali ya vita vya biashara na Marekani ni Uturuki. Marekani imetumia mbinu ya kuongeza ushuru wa forodha kwa chuma na aluminium zinazotoka Uturuki.

Nini hufanyika

Ni muhimu kuelewa namna vita vya biashara vinavyofanya kazi na kuweza kufikia malengo yake ya kudhoofisha uchumi wa nchi inayolengwa. Aina na kiwango cha athari za vita vya biashara kwa nchi inayopigwa vita hivi hutegemea mambo kadhaa. Haya ni pamoja na aina ya ‘silaha’ zinazotumika katika vita hii, ukubwa wa ‘silaha’, hali ya uchumi ya nchi husika na kadhalika. Kati ya ‘silaha’ zinazotumika katika vita hii ni kuzuia bidhaa na huduma kutoka nchi husika zisiingizwe kabisa ndani ya nchi inayoanzisha vita.

Katika hali hii, bidhaa husika hazitaruhusiwa kuingia katika nchi inayoanzisha vita hii. Silaha nyingine ni kuongeza kiwango cha ushuru wa forodha wa baadhi ya bidhaa au bidhaa moja kutoka nchi husika.

Nini hutokea

Kinachotokea pale bidhaa inapopigwa marufu kuingia katika nchi inayoanzisha vita vya biashara ni kwa nchi husika kushindwa kuuza bidhaa na huduma husika. Hii husababisha wazalishaji wa bidhaa na huduma husika kushindwa kuuza au kupunguza mauzo ya bidhaa na huduma katika nchi inayoanzisha vita hii. Hili linapotokea wazalishaji wanapoteza mauzo, fedha na faida.

Huweza kujikuta wakipunguza wafanyakazi kwa sababu ya kutokuwepo sababu za kiuchumi na kibiashara kuendelea kuzalisha.

Wafanyakazi wanaoathirika na wategemezi wao wanakosa vipato na hivyo kuwa katika hali ngumu kumudu maisha kwa maana ya kuwa na uwezo wa kununua bidhaa na huduma.

Serikali inaweza kukosa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yaliyokuwa yakitokana na bidhaa zilizo katika vita vya biashara moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Masoko ya fedha na uchumi kwa ujumla huweza kutikisika, kudorora na hata kuporomoka.

Yote haya huweza kusababisha matatizo makubwa ya kiuchumi bali pia ya kisiasa na kijamii.

Visasi

Kati ya hatari za vita vya biashara kutoka nchi moja ni kwa nchi inayopigwa vita na hata washikika wake kulipiza kisasi. Kisasi huweza kulipizwa kwa nchi husika nayo kuanzisha vita vya biashara.

Hufanya hivyo kwa au kukataza bidhaa kutoka nchi inayoipiga vita kuingizwa nchini mwake au kwa kuongeza ushuru wa forodha au kwa kufanya vyote hivyo. Madhara yake hufanana na yale yaliyoelezwa hapo awali kwa wazalishaji, wafanyakazi na wategemezi wao na nchi kwa ujumla.

Nani anafaidi

Kimsingi vita vya biashara kwa ujumla wake na hasa kunapokuwepo kulipiza kisasi kimahususi havina mshindi. Nchi zote mbili zinazohusika moja kwa moja huweza kuadhirika.

Kutokana na mwingiliano na mafundo ya kiuchumi kati ya nchi moja na dunia yote kutokana na utandawazi hata nchi zisizokuwa katika vita hii moja kwa moja huweza kuathirika. Kutegemeana na ukubwa wa vita husika, uchumi wa dunia unaweza kuathirika.

Biashara huru

Vita vya biashara ni kinyume na utaratibu wa biashara huru ya kimataifa. Katika biashara huru ya kimataifa, nchi huuza bidhaa na huduma kwa uhuru bila kuwekeana vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi.

Kutokuwepo kwa vikwazo hivi huwezesha nchi kuuza na kununua bidhaa kutoka kwingineko duniani bila vikwazo hivi.

Hata hivyo sio kila nchi na sio kila wakati nchi huzingatia na kukumbatia biashara huru. Nchi zinaweza kutokuzingatia biashara huru za kimataifa kwa sababu mbalimbali.

Kati ya sababu hizi ni kulinda wazalisaji wa ndani katika ujumla wake na hasa viwanda vichanga vya ndani. Ubinafsi na haja ya kujilinda kiuchumi kwa njia mbalimbali na hasa kwa kutumia mbinu za kikodi na zisizo za kikodi ni kinyume cha dhana ya biashara huru.

Kutokana na sababu ya faida hizi za biashara huru, ni muhimu sana kwa nchi kufanya juhudi za hali ya juu kuepuka vita vya biashara.