Msomi aliyeamua kujikita kwenye ufugaji wa nyuki

Muktasari:

  • Kani (24) ni mhitimu wa Stashahada ya Masoko kutoka Chuo Kikuu cha Cavendish (Uganda) ambaye ameamua kujikita katika ufugaji wa nyuki na uuzaji wa asali ili aweze kujikwamua kiuchumi.

Dar es Salaam.“Kiukweli siamini katika kuajiriwa, napenda kujiajiri ili nikifanikiwa niweze kutoa fursa za ajira kwa vijana wenzangu ambao wamekosa fursa hiyo na huku wakiwa na sifa ,” anasema Banjamin Kani. “Maana hata mimi nilipomaliza chuo na kurudi nyumbani nilikaa muda mrefu bila kazi ya kufanya kabla ya kuamua kujikita katika biashara.”

Kani (24) ni mhitimu wa Stashahada ya Masoko kutoka Chuo Kikuu cha Cavendish (Uganda) ambaye ameamua kujikita katika ufugaji wa nyuki na uuzaji wa asali ili aweze kujikwamua kiuchumi.

Aliamini katika biashara hiyo kwa sababu asali ni bidhaa inayoweza kutumiwa na watu wa rika zote, hususan wale wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali.

Anasema licha ya kuwa tayari na wazo la kuanzisha biashara hiyo baada ya kuona fursa za masoko zilizopo hakuwa na mtaji wa kufanikisha ndoto hizo.

“Ilikuwa 2016 nilikopeshwa Sh80,000 ambayo niliitumia katika kutengeneza mzinga mmoja wa asali na kuuweka nje ya nyumba yetu. Muda wa kurina asali ulipofika nilifanya hivyo na nilipouza nilipata Sh120,000 ambayo niliongeza mizinga mingine miwili,” anasema Kani.

Jambo hilo lilimtia moyo nakuwa mwanzo wenye matumaini makubwa jambo ambalo lilimfanya aongeze bidii katika shughuli zake nyingine ili aweze kuongeza mizinga ya asali.

“Mpaka sasa nina mizinga 12 na upatikanaji wa asali katika mizinga hiyo unategemeana na uingiaji wa nyuki hivyo upo uwezekano wa mimi kupata kuanzia Sh800,000 na kuendelea kila ninaporina asali.”

Anasema kutokana na biashara hiyo kutohitaji uangalizi wa karibu kama biashara nyingine amekuwa akijishughulisha na kilimo cha karoti, mahindi na mboga za majani ili kumudu gharama za maisha.

“Kwa sasa asali inauzwa kwa gramu na bei ninayouza Tabora inatofautiana na ya mkoa mwingine, kwa mfano gram 1,200 ambayo ndiyo kama lita moja huku tunauza Sh7,000 lakini tukienda Dar es Salaam au Arusha Tunauza kwa Sh12,000,” anasema.

“Kutokana na kufungashwa katika chupa za ukubwa tofauti na bei pia huwa tofauti, zipo za gram 250 ambazo zinauzwa kwa Sh1,000, gram 500 zinauzwa kwa Sh3,500 jinsi ukubwa unavyoongezeka unaenda sambamba na bei.”

Lakini mbali na uuzaji wa asali, Kani pia huuza nta ambayo inatokana na masega ya asali ambayo hujulikana kama makapi baada ya kukamuliwa.

Kwa faida ya wengine wasiofahamu nta hutumika kama malighafi katika kutengeneza vitu vingi ambavyo baadhi yake ni kiwi pamoja na mishumaa.

“Masega tunayachemsha, baadae tunayakamua kwa kutumia gunia na yale majimaji yanayotoka ndiyo yanatengeneza nta ambayo huuzwa Sh1,1000 kwa kilo moja.”

Anasema mbali na changamoto anazokutana nazo katika uzalishaji wa asali lengo lake ni kufikia uzalishaji wa tani moja ya asali ili aweze kukuza kipato chake na kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Ili kufikia uzalishaji huo nahitaji kuwa na mizinga 200 ambayo bado ni safari ndefu kutokana na mtaji wangu mdogo na kupata mkopo kuna masharti mengi jambo ambalo linalofanya tujitahidi kujiendesha wenyewe.”

Anasema endapo atafikia uzalishaji huo atakuwa na uwezo wa kufungua kiwanda kwa ajili ya kufungasha asali na kuuza nje ya nchi ambacho kitakuwa msaada kwa watu wengi wanaofanya shughuli hiyo.

‘‘Tabora hatuna kiwanda kinachofanya hivyo nta tunayozalisha tunawauzia wafanya biashara wakubwa kutoka mkoa mingine.”