Namna ya kuwa na matumizi madogo kuliko mshahara wako

Muktasari:

  • Mungu anaweza kukujalia ukapata fedha nyingi, ila usipozingatia matumizi bora ya kile ulichokipata, bado utaendelea kuwa na maisha duni.

Siri ya mafanikio yoyote ya kifedha iko kwenye nidhamu ya matumizi.

Mungu anaweza kukujalia ukapata fedha nyingi, ila usipozingatia matumizi bora ya kile ulichokipata, bado utaendelea kuwa na maisha duni.

Wako wafanyakazi ambao kipato chao ni kidogo, lakini wameweza kufanya mambo makubwa ya maendeleo kuliko wafanyakazi wenzao wenye mishahara mikubwa.

Wafanyakazi wengi huamini kuwa mshahara hautoshi, lakini kiuhalisia, fedha yoyote usiyoipangilia vizuri haitoshi.

Mahitaji ya binadamu hayana ukomo kama hayatadhibitiwa.

Hii ndiyo sababu kubwa inafanya fedha isiweze kutosheleza kila hitaji.

Mtu akiendekeza mtazamo wa kuwa mshahara hautoshi, atadumaza uwezo wake wa kuwaza namna bora ya kupanga anachokipata ili kiweze kutosheleza mahitaji yake ya kawaida na ya maendeleo.

Wakati watu wanapambana kila siku ili kipato kiongezeke, kujifunza namna gani anaweza kutumia mshahara anaoupata kwa manufaa zaidi, inakuhakikishia uwezekano wa kufikia ndoto zako.

Namfahamu bosi mmoja ambaye alikuwa ana mshahara zaidi ya Sh10 milioni

kwa mwezi, lakini alipokuwa amebakiza mwaka mmoja kustaafu alienda kwenye taasisi moja ya kifedha na kuomba akopeshwe Sh13 milioni ili akajenge kwao.

Najua watu wengi wenye mishahara midogo wataanza kumshangaa bosi huyu, lakini wasipokuwa na nidhamu ya matumizi, hata wao wataelekea huko.

Kwenye makala haya, tutaona njia mbali mbali unazoweza kuzitumia ili uweze kutumia kidogo kuliko kile unacholipwa. Njia hizo ni pamoja na Kufuatilia matumizi yako.

Cha kwanza kabisa ili kuweza kupunguza matumizi yako ni kuanza kufuatilia fedha yako inaenda wapi. Mshahara ukiingia tu, baada ya wiki moja, unashangaa hauna fedha.

Ulishawahi kukaa na kujiuliza fedha zako unazitumiaje? Ulishawahi kujiuliza, kwa matumizi yako ya msingi tu, unahitaji shilingi ngapi kwa mwezi?

Ukianza kuwa unatumia akili kwenye kuzitumia, utaanza kuona jinsi unavyotumia fedha nyingi kwenye mambo mengine ambayo si ya muhimu kwenye maisha yako.

Wakati mwingine unanunua vitu kwa bei ghali wakati ungeweza kuvipata kwa bei pungufu.

Usiogope kujifanyia tathimini ya jinsi unavyotumia pesa zako. Itakupa uelewa mpana wa aina ya maisha unayoyaishi. Utaweza kujipima namna unavyotumia fedha, hali hii itakufikisha kwenye maisha unayoyatamani.

Yawezekana ukagundua kuna baadhi ya tabia hata kama unazipenda, inabidi uziache ili uweze kuongeza nidhamu kwenye matumizi.

Mara nyingi tunaona usumbufu kuanza kuwaza kuhusu matumizi ya fedha?

Ni vyema tukakumbuka kuwa ni uamuzi unaoufanya kila siku ndio utakaoamua uwe na maisha bora au duni.

Unapoamua kuhusu matumizi yako unaamua kuhusu hatma yako. Usione usumbufu kuwaza kuhusu hatma yako.

Panga matumizi yako, usitumie fedha kiholela.

Usinunue kitu kwa sababu una fedha ya mshahara, nunua kwa sababu unachokinunua unakihitaji na kiko kwenye mpango.

Hata Sh500 ni ya muhimu, fedha ni kitu cha thamani.

Fedha inakaa muda mrefu kwenye mikono ya watu wanaoipa thamani inayostahili.

Nawajua watu wengi tu wakipita sokoni wanajikuta wananunua kiatu kizuri

kwa sababu amekipenda, lakini sio kwa sababu siku hiyo alikuwa ana mpango wa kununua kiatu.

Jifunze kutafakari kabla ya kununua kitu, weka hisia zako pembeni, tumia ufahamu.

Panga matumizi yako ya kila mwezi. Amua utanunua chakula cha shilingi ngapi, mavazi na hata kiasi utakachotumia kwa ajili ya starehe.

Ikiwezekana weka na fedha ya tahadhari.

Ukiwa una fedha ya tahadhari inakusaidia sana hasa zinapotokea dharura ambazo zingekusababisha utumie fedha kinyume na bajeti yako.

Kupanga matumizi kunakusaidia kupunguza matumizi yasio ya muhimu.

Jifunze kujilipa kwanza upatapo mshahara.

Ni vyema kutenga kiasi cha mshahara wako kama zawadi yako binafsi kwa kufanya kazi kwa bidii mwezi mzima.

Kiasi hiki ni vema ukipe kipaumbelekwenye matumizi yako kama matumizi ya chakula yalivyo ya muhimu.

Unashauriwa kiasi hicho ukitenge kabla haujafanya matumizi yoyote.

Fedha hii ni akiba yako ambayo utaweza kuitumia kwenye mipango yako mbalimbali ya kujiendeleza.

Unaweza ukaona ni jambo gumu kwa sababu siku zote matumizi yakoyamezidi mshahara wako.

Lakini hebu jiulize swali, je unamfahamu mtumwenye mshahara mdogo kuliko wa kwako lakini maisha yako na yake hayaonekani kama yana tofauti?

Kama una mfahamu hebu jiulize swali lingine, kama ukiamua matumizi yako yawe sawa sawa na mshahara wa huyo mtu, utaweza kuwa na ziada yashilingi ngapi?

Mwandishi wa vitabu James Alutcher aliwahi kusema “Kama unafanya kazi kwa ajili ya chakula na mavazi tu, wewe ni mtumwa wa kisasa”. Maneno haya ni magumu lakini yanachangamsha ubongo wako kutafakari namna gani mshahara wako utautumia kwa manufaa mapana.

Mtumwa kwenye kazi zake zote ngumu anazofanya analipwa chakula na mavazi ili aendelee kuwa na uhai pamoja na nguvu za kumtumikia bwana wake.

Hawezi kuwa na baki yoyote kwenye malipo anayoyapata.

Usiwe kama mtumwa, jifunze kuweka akiba.

Mshahara ukiongezeka usiongeze matumizi ongeza akiba.

Yawezekana umewaza ni namna gani utaweza kuweka akiba na umeona haiwezekani. Hili linaweza kutokea kama matumizi yako ni makubwa ukilinganisha na mshahara wako. Basi, jifunze kutumia kwa kiasi kile unachokipata sasa hivi kwa mwezi bila kukopa. Mshahara unaoupata uweze kuyatosheleza matumizi yako ya sasa.

Ukifanikiwa kuwa na nidhamu ya matumizi, jitahidi mshahara wako uongezeke.

Yawezekana ukaongezewa mshahara kwa sababu ya kupandishwa cheo au nyongeza ya kawaida kwa watumishi wote.

Mshahara wako utakapopanda usiongeze matumizi. Fedha itakayoongezeka iweke akiba.

Hii ni njia rahisi ya kujifunza kuweka akiba.

Kumbuka kitakachokuletea utajiri sio mshahara ila nidhamu kwenye kusimamia matumizi yako.

Itaendelea wiki ijayo.

Gidion Obeid ni Mhadhiri wa Uhasibu na Usimamizi wa Fedha, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na mwanafunzi wa Shahada za Uzamivu (PhD). Kwa ushauri wasiliana naye kwa namba 0625698050.