Oscar Mdenye, ofisa ustawi wa jamii alijitosa kutengeneza majiko

Muktasari:

  • Lakini ajabu ni kuwa, baada ya kutambua matamanio ya watu wengi, Oscar Mdenye (41) ambaye ni Ofisa ustawi wa jamii wa wilaya ya Nkasi aliamua kutafuta ujuzi wa kutengeneza majiko ya aina hiyo ila yanayotumia kuni na mkaa. Majiko hayo yanatumia kiwango cha chini cha nishati ukilinganisha na majiko mengine, ni kama robo ya matumizi ya majiko ya kawaida.

Tumezoea kuona majiko mazuri na ya kisasa ya kuvutia yanayotumia nishati ya gesi na umeme pekee huku majiko ya mkaa yakiwa yaleyale tuliyozoea kuyatumia huku wale watumiaji kuni wakitumia mafiga. Jambo hilo linawafanya watumiaji wa mkaa na kuni katika kupika kutamani kuwa na uwezo wa kumudu gharama za umeme au za gesi ili waweze kupata ahueni ya kutumia majiko hayo.

Lakini ajabu ni kuwa, baada ya kutambua matamanio ya watu wengi, Oscar Mdenye (41) ambaye ni Ofisa ustawi wa jamii wa wilaya ya Nkasi aliamua kutafuta ujuzi wa kutengeneza majiko ya aina hiyo ila yanayotumia kuni na mkaa. Majiko hayo yanatumia kiwango cha chini cha nishati ukilinganisha na majiko mengine, ni kama robo ya matumizi ya majiko ya kawaida.

Anasema alianza kutengeneza majiko hayo 2014 kwa mtaji wa Sh2.5 milioni baada ya kupata ujuzi kwa mtu mwenye asili ya Italy 2009. “Kwa kipindi chote nilikuwa bado nafanya kazi sehemu tofauti na nilikuwa sina makazi maalumu, hadi nilipohamia huku na kuona siwezi kuhama tena nikaamua kuanza shughuli hii kwa sababu eneo ninaloishi pia kuni na mkaa ndiyo vyanzo vya nishati ya kupikia kwa watu wengi,” anasema Mdenye.

Anasema mbali na kujifunza kutoka kwa raia huyo, vitu vingine wamekuwa wakivibuni kulingana na mahitaji ya wateja wengi ili kuwapunguzia adha ya kuhangaika na moshi na moto mkali. Anasema hutumia vyuma na mabati kwa asilimia kubwa kutengeneza majiko hayo na anao uwezo wa kutengeneza hadi majiko matatu kwa wiki. “Tunatengeneza majiko ya aina nne, yapo ya matumizi ya nyumbani, matumizi ya taasisi kama shule, majiko ya mikate, heater za maji kwa ajili ya hoteli au nyumba za kulala wageni na saluni,” anasema Mdenye Anasema licha ya kuwapo kwa aina hizo nne za majiko pia hutengenezwa katika ukubwa tofauti kulingana na mahitaji ya mteja. “Jiko la matumizi ya nyumbani la tundu moja tunauza kwa Sh560, 000 matundu mawili Sh650,000 na matundu matatu Sh750,000. Jiko la matumizi ya taasisi au biashara la ujazo wa lita 120 ni Sh1.5 milioni, lita 200 ni Sh2.2 milioni na lita 300 ni Sh2.8 milioni. “Jiko la mikate linaanzia Sh1.5 milioni hadi Sh7 milioni kutegemeana na idadi ya mikate. Heater tunaanzia Sh700,000 hadi Sh2 milioni kutegemeana na ujazo na anaamua mteja mwenyewe atumie kuni au mkaa.” Anasema wateja wakubwa wa majiko hayo ni wafanya biashara wa kati na watumishi wa serikali au mashirika.

Anasema wateja hao huwapata kutokana na kujitangaza katika matukio tofauti kama siku ya Mwenge, na sherehe mbalimbali za kitaifa pamoja na kwenye mitandao ya kijamii. Anasema masoko ya biashara hiyo hayajaimarika kwa sababu ya mbinu na kushindwa kujitanua kutokana na majukumu ya kazi kama mwajiriwa, hivyo hulazimika kutumia muda wa baada ya kazi kutengeneza na kuuza. “Soko lipo na uhitaji ni mkubwa, watu wanayapenda na kuyakubali lakini mtaji wangu bado mdogo haukidhi mahitaji ya bishara,” anasema Mdenye. Licha ya kutumia vifaa duni kutengenezea majiko hayo na kukumbwa na gharama kubwa ya vifaa na usafirishaji kutoka Dar es Salaam hadi Nkasi, Mdenye bado ana ndoto ya kuwa na kiwanda cha kati chenye uwezo wa kujiendesha.

“Lakini katika malengo yangu nataka kuboresha majiko haya ili yawe na uwezo wa kutumia kuni, mkaa, makaa ya mawe na gesi ili kuendana na nyakati na mahitaji ya wateja,” anasema Mdenye.