Thursday, July 12, 2018

Saidi: Nalima na kukamua mafuta ya maparachichi

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

Mara nyingi tumekuwa tukisikia wakulima wa matunda wakihimiza kujengewa viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa zao.

Jambo ambalo huenda ulikuwa hulijui kuhusu marachichi, licha ya kula na kutengeneza juisi, zipo bidhaa nyingine zinazoweza kuzalishwa kutokana na matunda hayo yanayostawi maeneo mengi nchini.

Tunda hilo husifika kwa kuukinga mwili dhidi ya kemikali hatari na kumfanya mtu kuonekana kijana na kuondoa chembe haribifu mwilini.

Jambo hilo lilimfanya mtaalamu wa masuala ya kilimo na mkurugenzi wa kampuni ya Nzalacado, Dk Twahir Saidi kuanza kutengeneza bidhaa zitokanazo na tunda hilo.

“Nilianza kukamua maparachichi mwaka 2012 ili kupata mafuta ninayoyahitaji ambayo yana faida nyingi mwilini,” anasema Dk Saidi.

Anasema mafuta yatokanayo na maparachichi huondoa lehemu mwilini na kemikali zote zenye madhara katika mwili wa binadamu.

Wazo la kuongeza thamani ya matunda hayo anasema alilipata baada ya kuona matunda hayo yakiuzwa kwa bei ndogo yanapofikishwa sokoni.

“Mtu anapotumia mafuta haya ngozi yake haiwezi kuwa na mafuta wala kuwa na nyama uzembe. Unapoyatumia mafuta haya unatakiwa kuchanganya kijiko kimoja katika chakula chako,” anasema Dk Saidi.

Anasema katika kila tani kumi za maparachichi anayonunua hupata lita 500 za mafuta na kila lita moja huiuza kwa Sh30,000 na chupa ndogo ya milimita 330 kwa Sh15,000.

Anasema chupa hiyo ndogo ukiitumia ni sawa na kula maparachichi 50. Licha ya mafuta ya maparachichi, anasema hutengeneza pia mafuta ya nyonyo anayoyauza Sh20,000 kwa lita.

Anasema mafuta yote anayokamua hayaongezwi kitu cha aina yoyote na yeyote anayetumia hupata vitamini sawa na aliyekula maparachichi ya kawaida.

Anasema uzalishaji wa mafuta hayo hutegemea upatikanaji wa matunda husika. Kutokana na kuwa na kampuni pekee inayozalisha mafuta hayo nchini, anasema ametengeneza soko la uhakika kwa wakulima wa zao hilo kwa mikoa ya Njombe na Rungwe.

Mpaka sasa, anasema ana uwezo wa kuzalisha hadi lita 5,000 kwa mwaka ambao ni mdogo ikilinganishwa na uwezo wa mashine aliyonayo yenye uwezo wa kuzalisha lita 10,000 kwa kipindi hicho.

Miongoni mwa vitu vinavyopunguza ufanisi wa uzalishaji wake ni udogo wa mtaji alionao. Kupata mashine hiyo kubwa, anasema aliandika wazo la kupata mashine inayoweza kukamua mafuta hayo na kuliuza kwa wachina ambao wulishirikiana naye kuitengeneneza.

Msimu wa kuvuna maparachichi huchukua kati ya miezi mitatu hadi minne hivyo kuwa na muda ziada ambao mashine husimama bila kufanya uzalishaji.

Kutokana na fursa huyo, anasema walijaribu kuongeza ufanisi kwa kuiwezesha kuwa na uwezo wa kusaga mbegu za maparachichi, nyonyo na mbarika jambo lililoongeza ufanisi wao katika uzalishaji.

Anasema kuhakikisha anakuwa na kianzio, analo shamba la eka 200 ambalo amelima matunda hayo.

-->