Tafsiri kushushwa kwa riba ya Benki Kuu

Muktasari:

  • Hii ni riba ambayo Benki Kuu hutoza pale inapozikopesha benki za biashara. Benki hizi nazo huwakopesha wateja wake kwa kuwatoza riba ya juu kidogo ili zitengeneze faida itakayoziwezesha kuendelea kutoa huduma.

Kati ya taarifa nzuri za uchumi tukiimaliza Agosti ni kupunguzwa kwa riba kulikotangazwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka asilimia tisa hadi saba kuanzia tarehe 28.

Hii ni riba ambayo Benki Kuu hutoza pale inapozikopesha benki za biashara. Benki hizi nazo huwakopesha wateja wake kwa kuwatoza riba ya juu kidogo ili zitengeneze faida itakayoziwezesha kuendelea kutoa huduma.

Kimsingi, punguzo hili ni habari njema kwa benki na njema zaidi kwa wateja wa benki husika kwa sababu asilimia mbili zilizopungua si kitu kidogo hasa kwa mikopo mikubwa.

Kuna tafsiri mbalimbali za kiuchumi kuhusu punguzo hili nami nitaainisha baadhi ili kunogesha mjadala uliopo kuongeza mchango wangu.

Benki Kuu

Katika ujumla wake, Benki Kuu ni mamlaka dhibiti ya sekta ya fedha. Husimamia mambo yote makuu yahusuyo sekta hiyo kwa upana wake.

Hutekeleza sera, sheria na kanuni za fedha nchini. Husimamia taasisi zote za fedha zikiwemo benki na biashara. Katika jukumu hili, hutoa leseni za uanzishaji na uendeshaji wa biashara. hufuta leseni pia pale inapobidi.

Kati ya majukumu ya masuala ya kisera ya Benki Kuu ni usimamisi wa sera za fedha yakiwamo masuala ya riba.

Sera za fedha

Sera za fedha ni muhimu kuchochea na kusisimua uchumi wa nchi yoyote duniani. Sera hizi huhusisha masuala ya riba inayotozwa na taasisi za kifedha kwenye mikopo.

Sera pana za fedha huwa na riba ndogo kwa wakopaji. Riba ni bei ya mkopo inayolipwa na mkopaji. Riba inapokuwa chini hurahisisha ukopaji kwa ajili ya uwekezaji na matumizi ya kawaida.

Yote haya huchochea na kusisimua uchumi. Ili kuwa na riba ndogo mambo kadhaa ni muhimu ambayo ni pamoja na sera pana za kifedha kutoka mamlaka za fedha katika nchi husika ambayo kwa Tanzania ni Benki Kuu.

Sera pana za fedha ni huhusisha kupunguza riba inayolipwa na benki za biashara zinapokopa kutoka Benki Kuu kabla hazijawakopesha wateja wake sokoni.

Riba

Kwa lugha rahisi, riba ni bei ya mkopo. Mkopaji anayekopa kutoka taasisi yoyote ya fedha hulipa deni lake pamoja na riba. Riba hii huwa ni asilimia fulani ya mkopo.

Kiwango cha riba kwa maana ya asilimia ya mkopo hutegemea mambo tofauti. Katika soko huru ambako mvutano huru wa nguvu za ugavi na utashi sokoni hutawala, riba huamuliwa na nguvu za soko.

Ugavi unapozidi utashi kwa maana ya uhitaji riba huenda chini. Kinyume chake ni kweli pia. Hii ni sawa na pale bidhaa kama nyanya au bidhaa nyingine zozote zinapokuwa nyingi sana sokoni kulinganisha na uhitaji wake, bei hupungua.

Riba benki

Pamoja na mambo mengine, BOT ni benki ya benki za biashara na taasisi zote za fedha. Katika hili Benki Kuu huzikopesha benki hizo ili nazo zikakopeshe kwa wateja wake.

Inapozikopesha benki hizi hutoza riba. Benki zitakapokopesha lazima nazo zitoze riba kubwa kuliko ya Benki Kuu. Ni katika muktadha huu Benki Kuu huweza kuongeza au kupunguza riba inayotozwa kwa wateja wa benki za biashara.

Mara ya kwanza, mwanzoni mwa mwaka jana, BoT ilipunguza riba kutoka asilimia 16 hadi 12. Baadaye, Agosti 2017 ilishusha tena kutoka asilimia 12 hadi tisa.

BoT pia huweza kuongeza fedha katika mzunguko. Zote hizi ni hatua za kisera kuhakikisha upatikanaji wa mikopo na kwa riba ndogo. Hata hivyo riba ndogo pekee haitoshi kuwashawishi wakopaji kuchukua mikopo.

Punguzo

Nia kuu ya kupunguza riba kama ilivyofanywa na Benki Kuu ni kuongeza uwezekano wa upatikanaji wa mikopo kwa wakopaji.

Punguzo la riba ni kama punguzo la bei kwa bidhaa na huduma nyingine sokoni. Bei inapopunguzwa ni hamasa kwa wateja kununua zaidi. Hii ni kweli pia kwa riba zinapopunguzwa. Lengo ni kuchochea upatikanaji wa mikopo.

Mikopo nayo inatakiwa kuchochea uchumi kupitia uzalishaji wa huduma na bidhaa. Uzalishaji huchochea ajira na kipato. Kipato nacho huchochea matumizi hivyo kuhamasisha uzalishaji zaidi. Kutokana na mzunguko huo faida huwafikia wengi.

Hivyo kushusha riba ni mbinu ya kimkakati ya kisera. Mbinu hii hutumiwa na mamlaka dhibiti ya fedha pale soko linaposhindwa kuweka riba sawa.

Mafanikio

Mafanikio ya kushusha riba yatapimwa kwa kuongezeka ukopaji utakaochangiwa na punguzo hili. Benki Kuu kupunguza riba kwa asilimia mbili kusitegemewe kuzishawishi benki za biashara nazo kupunguza riba zao kwa kiasi hiki.

Uwezekano ni kupunguza riba kwa kiasi kidogo kuliko asilimia mbili. Hii ni kwa sababu kiwango cha riba kinachotozwa na benki za biashara hutegemea gharama nyingine zikiwamo za uendeshaji.

Riba inayotozwa na benki za biashara hutegemea pamoja na mambo mengine gharama za benki husika na faida inayotaka kupata. Gharama hizi ni pamoja na za wafanyakazi, miundombinu, ulinzi, bima hata riba inayotozwa na taasisi nyingine.

Vilevile riba hutegemea kiasi kinachokopwa. Kwa kawaida riba hupungua kadiri kiasi kinachokopwa kinavyokuwa kikubwa. Hivyo ni vizuri kuwa na mategemeo halisi katika jambo hili la kupunguzwa riba ya mkopo.