Tazara na mikakati ya kukuza usafirishaji

Muktasari:

  • Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni baada ya kupitia katika sintofahamu ya kusuasua kwa biashara kwa muda mrefu kwa wasa-firishaji hao wa mizigo na abiria kati ya nchi hizi mbili.

Shirika hilo awali lilikuwa likishindwa kutengeneza faida ikiwa ni pamoja na ulipaji wa mishahara kwa wafanyakazi wake

Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) imedhamiria kuongeza na kuboresha usafirish-aji mizigo katika kipindi cha miaka miwili ijayo hadi kufikia tani 600,000.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni baada ya kupitia katika sintofahamu ya kusuasua kwa biashara kwa muda mrefu kwa wasa-firishaji hao wa mizigo na abiria kati ya nchi hizi mbili.

Kwa miaka mingi shirika hilo linalo-safirisha mizigo kati ya Tanzania na Zam-bia halikuwa na uwezo wa kujitegemea katika kulipa mishahara na kutengeneza faida.

Lakini katika kipindi cha hivi karibuni matumaini ya kurudi katika hali yake ya kawaida yameanza kuonekana baada ya kuanza kufanya vizuri katika baadhi ya sehemu.Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu (2015/2016 hadi June 2018), Mkurugenzi mkuu wa Tazara Bruno Ching’andu anasema kiwan-go cha mizigo iliyosafirishwa kimeongeze-ka kutoka tani 88,000 hadi tani 220,000.

“Tumeshuhudia ukuaji wa asilimia 130 kwa miaka mitatu iliyopita lakini ninaami-ni katika kipindi cha miezi 18 hadi 24 ijayo tutafikia lengo letu la kusafirisha tani 600,000 kwa mwaka kama mipango itaenda kama tunavyohitaji,” anasema Anasema anaamini malengo hayo yata-fanikiwa kwa sababu wamejitahidi kupun-guza maeneo yaliyokuwa yakiathiri kasi ya treni kutoka maeneo 52 hadi kufikia maeneo 14 mwaka 2016.

Usalama wa mizigo pia haukuzingatiwa wakati treni ikipunguza mwendo katika vituo hivyo 52 ambayo vilionekana kuwa kikwazo jambo ambalo lilifanya usafiri huu kukatiwa tamaa lakini siku hizi mambo yameanza kuwa bora,” anasema Ching’andu

Pia muda wa usafirishaji mizigo umepungua kutoka kati ya siku 30 hadi 35 na kufikia siku 5 hadi 7 huku wizi wa mizigo ukipungua kwa asilimia 99 katika kipindi cha miaka hiyo mitatu.

Anasema kama mambo yatakaa sawa wanajitahidi kupunguza muda wa kuomba mabehewa kwa ajili ya kusafirisha mizigo hadi kufikia masaa 48 kutoka siku 22 hadi 40 zilizokuwepo miaka mitatu iliyopita.

Anasema endapo itakuwa hivyo itasaidia katika kupunguza muda wa mabehewa kugeuka hadi kufikia siku 18 kutoka siku 73 zilizokuwepo awali.

“Sasa hivi tumeanza kurejesha imani kutoka kwa wateja wetu ambao awali walikimbia kutokana na ugumu waliopitia walipotumia usafiri huu,”

“Hivi sasa tunapokea oda ya kusafirisha mizigo mingi ambayo wakati mwingine inakuwa nje ya uwezo wetu,” anasema Ching’andu.

Anasema mahitaji wa usafirishaji wa madini ya kopa na Manganese kutoka Zambia kuja Tanzania yanazidi kuongezeka jambo ambalo linaongeza mahitaji ya usafirishaji. “Ongezelo la mizigo mingi ya kuelekea Dar es Salaam imechangiwa na kuimarishwa kwa huduma kunakofanywa na uongozi ikiwemo kupunguza muda wa usafirishaji, ajali na matatizo ya kiusalama,”

“Kuongezeka kwa uwezo wa bandari ya Dar es Salaam pia kumechangia kuongeza idadi ya mizigo ya kusafirishwa,” anasema Ching’andu.

Anasema ili kufanikisha azma ya kuongeza usafirishaji mizigo, Tazara inahitaji walau vichwa 30 vya treni ili kuweza kufikia lengo la kusafirisha tani 600,000 zilizopo katika mikakati yao.

Licha ya kuwa na uhitaji huo, wanavyo vichwa 14 ambavyo vinafanya kazi huku vingine 6 vinahitaji matengenezo kila wakati.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuidhinisha Sh10 bilioni kwa ajili ya kutengeneza vichwa 10 vya treni. Vitatusaidia lakini ili kuanza kutengeneza faida tunahitaji vichwa vingine vipya,” anasema

Katika jitihada binafsi ili kukabiliana na upungufu wa vichwa vya treni, Tazara iliingia makubaliano, Access Agreement (OAA) na Shirika la reli la Zambia (ZRL) mwaka uliopita ili kuyawezesha mashirika hayo kuazimana vichwa na mabehewa na kutumia reli.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Tazara alibainisha kuwa vichwa vya treni vya ZRL havina uwezo wa kufika Dar es Salaam licha ya kuwa vile vya Tazara vina uwezo wa kufika kila eneo katika nchi ya Zambia.

“Makubaliano bado hayajaweza kuzaa matunda kwa sababu bado hatujapata kile tulichokitegemea licha ya kuwa imetusaidia kuongeza kituo katika maeneo ya Lusaka, Livingstone na Ndola,” anasema

“Hii tunaweza kusema kuwa, upo ulazima wa kubadilisha vichwa vya treni unapofika stesheni ya Kapiri Mposhi ili uweze kusafirisha mzigo kutoka Zambia kuja Dar es Salaam,” anasema

Ching’andu anasema uongozi unajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanatengeneza faida ili kampuni hiyo ianze kutoa gawio kwa serikali.

Anasema mpaka sasa hawana uwezo wa kutoa gawio kwa serikali kwa sababu ya kutopata faida inayoiweza kuwatosheleza wao kwanza kumudu gharama za kujiendesha.

“Hata Serikali inatambua kuhusiana na suala hili na ni wao pia wanatusaidia kulipa mishahara kwa waajiriwa na mahitaji mengine,” anasema Ching’andu na kuongeza kuwa

“Lakini mambo yote yatakuwa sawa katika kipindi cha miaka miwili ijayo,” anaongeza.

Usafirishaji abiria

Katika upande mwingine Tazara ilipata ongezeko la abiria kutoka 483, 000 mwishoni mwa Juni 2017 hadi kufikia 543, 000 juni 2018 kwa treni inayofanya safari kati ya Zambia na Dar es Salaam huku siku za kusafiri zikipungua kutoka 8.5 hadi siku 6.4.

Kutoka Makambako hadi Kidatu abiria waliongezeka hadi kufikia 393, 550 mwaka 2018 kutoka 294, 031 waliokuwepo mwaka 2017.

Kwa treni ya ndani inayofanya safari zake kutoka eneo la makao makuu Tazara hadi Mwakanga, Dar es Salaam abiria pia waliongeza.

“Abiria waliotumia treni hii mwaka 2017 walikuwa 2.37 milioni ambao wameongezeka hadi kufikia 2.42 milioni Juni 2018,” anasema Ching’andu

Kumbukumbu

Reli ya Tazara, ambayo pia huitwa Reli ya Uhuru (Uhuru Railway), ilijengwa kati ya 1970 na 1975 kwa lengo la kuipa nchi ya Zambia iliyokuwa haina pwani ya bahari ‘kiunganisho’ hadi Bandari ya Dar es Salaam kama njia mbadala ya kusafirisha bidhaa zake zilizokuwa zikipitia Rhodesia (sasa Zimbabwe), Afrika ya Kusini na Msumbiji.

Ikumbukwe nchi hizo tajwa zilikuwa bado chini ya utawala wa kikoloni na/au wazungu wachache huku mapambano ya kudai uhuru yakiendelea. Kwa upande wa Tanzania lengo lilikuwa ni kusukuma maendeleo katika maeneo reli hiyo ingepita.

Hivyo mradi huu tayari ulikuwa na soko kuhusu matumizi yake (turnkey project) na uliwezeshwa na kugharamiwa na fedha kutoka Jamhuri ya Watu wa China.