Tutembee kifua mbele kufufuka kwa ATCL

Muktasari:

Usafiri wa anga una historia yake Tanzania ambayo si ya kuridhisha kwa kipindi kirefu. Usafiri wa anga ambao kwa kiasi kikubwa unachangia kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii umekua ukisuasua na kudorora kabisa baadhi ya nyakati.

Linapofanyika jambo jema kwa manufaa ya wananchi ni vyema likapongezwa na kuandikwa ili libaki katika kumbukumbu za leo na kesho.

Usafiri wa anga una historia yake Tanzania ambayo si ya kuridhisha kwa kipindi kirefu. Usafiri wa anga ambao kwa kiasi kikubwa unachangia kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii umekua ukisuasua na kudorora kabisa baadhi ya nyakati.

Wakati nchi kama Morocco ikiwa inaingiza takriban watalii milioni 12 kwa mwaka, Tanzania inaingiza wastani wa watalii milioni mbili tu licha ya kuwa na vivutio vingi zaidi kuliko Morocco.

Moja ya sababu ya idadi ndogo ya watalii ni kutokuwa na shirika la usafiri wa anga litakalotoa huduma husika kwa wageni wanaotoka nje kuja nchini hata kutembelea maeneo tofauti wanayotaka kuyaona.

Moja ya shirika la umma ambalo lilikuwa limegubikwa na kusuasua kwa usimamizi wa uwekezaji wa Serikali ni Shirika la Ndege (ATCL) ambalo kwa namna moja au nyingine lilikabiliwa na changamoto ya mtaji hivyo kuendelea kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Hili linathibitishwa na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/2014.

Ripoti zinaonesha wakati wa ubinafsishaji, shirika la ndege lilikuwa na ndege mbili ambazo ni B737–200 iliyokuwa inamilikiwa na ATCL na B737–300 iliyokodishwa.

Pamoja na ubinafsishaji wa Shirika hilo, mategemeo ya ufanisi kuongezeka na kujiendesha kwa faida ilikuwa kinyume. Shirika lilipata hasara na kughubikwa na matumizi makubwa yasiyoendana na mapato.

Kuanzia mwaka 2012 hadi 2006 Shirika liliendelea kupata hasara likiwa na mtaji hasi wa Sh6.9 bilioni. Sababu zinazotajwa kuiyumbisha ATCL ni gharama kubwa za kukodi ndege kutoka Shirika la ndege la Afrika Kusini (SAA).

Kwa mfano, mwaka 2007 ATCL ilikodi ndege aina ya Airbus namba A320-214 kutoka kampuni ya Wallis Traiding. Gharama yake ilikuwa Dola 370,000 (wastani wa Sh700 milioni) kwa mwezi. Wakati huo gharama za matengenezo ya ndege yakiwa juu ya aliyekodisha, ATCL.

Wakati wote wa mkataba, 2007 hadi 2011 ndege iliyokodiwa haikuwahi kufanya kazi. Muda wote ulitumika kuitengeneza. Hadi mkataba unasitishwa, gharama za matengenezo pamoja na ada nyingine ambazo zilitakiwa kulipwa na ATCL kwa kampuni iliyoikodishia ndege zilikuwa zaidi ya Dola 42.45 milioni (wastani wa Sh80.7 bilioni).

Wahenga wanasema, ukijua utakoenda ni vyema ukajua na unakotoka pia. Ni jambo la kupendeza na kuleta matumaini ndani ya miaka miwili, Serikali moja kutoka katika nchi masikini kusini mwa jangwa la Sahara inanua ndegesita, tatu zikiwa zinaendelea kutoa huduma kwa malipo taslimu.

Wachumi husema, kopa inapobidi. Usikope tu kwa sababu wengine wanakopa. Unapokopa ni lazima uuziwe bidhaa kwa gharama ya juu, pili kulipa riba ya mkopo kadiri ya makubaliano. Tatu, kuendelea kuwa mtumwa wa mkopo hadi utakapomaliza kuulipa.

Wakati mwanzo ATCL ilitumia wastani wa Sh80.7 bilioni kukodi ndege ambayo haikuwahi kufanya kazi, Serikali ya awamu ya tano imenunua kwa fedha tasilimu ndege tatu na nyingine tatu zikitarajiwa kuwasili siku za usoni kwa gharama ya Sh227.6 bilioni ikijumisha malipo ya awali kwa ndege zilizobaki.

Pamoja na ATCL kuendelea kutoa huduma katika baadhi ya mikoa nchini, taarifa zinaonyesha Serikali ina nia ya kuanza kutoa huduma nje ya mipaka ili kuongeza wigo wa huduma na kukuza mapato.

Kila Mtanzania mzalendo bila kujali kipato, itikadi ya chama au dini anapaswa kutembea kifua mbele na kujivunia Shirika letu la ndege kwa kumilika na kuendesha biashara ya usafiri wa anga kwa kutumia ndege zake zenyewe.

Taarifa zinaonesha ATCL bado inajiendesha kwa hasara ingawa kiwango kinaendelea kupungua mwaka hadi mwaka. Ikifika wakati Shirika likaanza kupata faida, maana yake kila Mtanzania atafaidika kwa namna moja au nyingine kupitia huduma zinazotolewa na Serikali ikiwemo afya, maji, elimu, miundombinu na nyingine.

Faida hizo zinaweza zisisubiri shirika kuanza kupata faida, manufaa yanaweza kuonekana baada ya muda mfupi idadi ya watalii itakapoongezeka na kuongeza fedha za kigeni.

Licha ya kutokuwa na shirika la ndege kwa muda mrefu, sekta ya utalii imekuwa ikichangia zaidi fedha za kigeni. Kuimarika kwake, kutawashirikisha wananchi wengi hivyo kukuza kipato chao.

Biashara ya Usafiri wa anga ni chanzo kikubwa cha mapatoyanayoweza kutumika kuboresha miundombinu na huduma kwa wananchi hivyo kupunguza umasikini kutokana na kuimarika kwa sekta mbalimbali.

Hivi karibuni tumepokea ndege kubwa aina ya Dreamliner ambayo itakuwa ikifanya safari za nje ya Afrika. Hili ni jambo jema la kujivunia kwa kila Mtanzania.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango wa Tamisemi.