Tuwekeze zaidi kwenye mifumo ya TEHAMA kwa usahihi wa takwimu na kuongeza mapato wananchi pia

Muktasari:

  • Mifumo ya Tehama imekuwa chachu ya ongezeko la mapato kwa nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea. Mwaka 2013 wastani wa ongezeko la GDP kwa nchi zinazoendelea ulikuwa asilimia 0.8 na asilimia 0.3 kwa nchi zilizoendelea. Nchi kadhaa duniani zimeakisi faida ya kutumia mifumo ya Tehama katika ukusanyaji wa mapato ikiwemo Tanzania.

Ripoti kadhaa zinaonyesha uwepo wa uhusiano wa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na ukusanyaji wa takwimu sahihi na kuongeza mapato ya Serikali. Utafiti uliofanyika kati ya mwaka 2008-2012 katika nchi 56 duniani umebainisha kuongezeka kwa mapato kwa wastani wa dola 983 bilioni na kutengeneza nafasi za ajira zaidi ya milioni 1.9 .

Mifumo ya Tehama imekuwa chachu ya ongezeko la mapato kwa nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea. Mwaka 2013 wastani wa ongezeko la GDP kwa nchi zinazoendelea ulikuwa asilimia 0.8 na asilimia 0.3 kwa nchi zilizoendelea. Nchi kadhaa duniani zimeakisi faida ya kutumia mifumo ya Tehama katika ukusanyaji wa mapato ikiwemo Tanzania.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), makusanyo yamekuwa yakiongeza mwaka hadi mwaka. Moja ya sababu ikielezwa ni matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama. Kabla ya kuimarishwa kwa mifumo ya Tehama makusanyo yalikuwa shilingi 4.4 trilioni mwaka 2009/2010. Mwaka 2010/2011 Mamlaka ilipoanza kutumia mifumo ilikusanya shilingi 5.3 trilioni.

Uwekezaji kwenye mifumo ya Tehama imeendelea kusaidia makusanyo kuongezeka, hadi kufikia mwaka 2016/2017 makusanyo yalifikia shilingi 14.2 trilioni kutoka shilingi 6.5 trilioni mwaka 2011/2012.

Ili kuthibiti upotevu na kuimarisha ukusanyaji wa mapato, Serikali imeanzisha mfumo wa kukusanyia mapato yote ya Serikali uitwao Government e-Payment Gateway (GePG) ambao mifumo ya kukusanyia mapato ya taasisi zote za Serikali inatakiwa kuunganishwa na mfumo huo.

Serikali pia ilianzisha mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato ya ndani kwa mamlaka za Serikali za Mitaa (LGRCIS) mwaka 2014 ambao hadi sasa umeonesha mafanikio makubwa katika kuinua kiwango cha makusanyo.

Mifumo ya Tehama imeweza kuthibiti upotevu wa mapato ya Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato kupitia vituo vya afya, zahanati, shule za msingi na sekondari kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa matumizi ya fedha ngazi za vituo (Facility Financial Accounting and Reporting System – FFARS).

Kwa upande wa hospitali mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato na usimamizi wa hospitali (Government of Tanzania Hospital Management Information System - GoT-HoMIS) umeweza kuongeza mapato katika hospitali za Serikali baada ya kuanza kutumika.

Pamoja na mifumo ya Tehama kuwa na uwezo mzuri wa kuhifadhi kumbukumbu na kutoa takwimu zinazoaminika pia imekuwa ikutumia vizuri rasilimali zilizopo ikiwemo muda, watu na vifaa.

Serikali imeendelea kuhakikisha inaepuka miamala inayohusisha malipo ya fedha taslimu. Ulipaji wa ankara kwa kutumia malipo ya fedha taslimu ulikuwa ukigubikwa na rushwa na vitendo vingine visivyo vya kimaadili.

Serikali kupitia taasisi zake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutumia mifumo ya Tehama katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Hii inasaidia kwa kiasi kikubwa kutunza takwimu na kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali chache zilizopo.

Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa zinatumia mfumo wa mipango na bajeti (PlanRep) kuandaa mipango na bajeti na kuiwasilisha kwenye mamlaka zinahusika kupitia mfumo bila ya wataalam kusafiri kwenda kuwasilisha mipango na bajeti. Mfumo unatajwa kupunguza gharama kwa Mamlaka za Mikoa na Serikali za mitaa kutoka 8.3 bilioni kabla ya kuanza kutumia mfumo hadi kufikia 4.0 bilioni kwa mwaka 2017/2018.

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano inabadilika kila siku, ni vyema Serikali ikawekeza rasilimali za kutosha ikiwemo fedha, wataalam na vifaa ili taasisi za Serikali ziweze kuhimili kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Serikali inahitaji fedha ili iweze kutoa huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi. Ili kuthibiti upotevu wa mapato na kutunza kumbukumbu ni vyema ikawekeza vya kutosha katika mifumo ya Tehama.

Mwandishi ni Mtakwimu, ofisi ya Rais – TAMISEMI.