Ulaji huu utakuongezea mvuto wa ngozi yako

Muktasari:

Katika ulaji ni vyema tunapokula vyakula kuchagua vile ambavyo vina virutubisho sahihi ili kuweza kuimarisha afya pamoja na ngozi ya mwili wako.

Urembo hautokani tu na vitu tunavyopaka, bali huanzia hata kwenye aina ya vitu tunavyokula kila siku.

Katika ulaji ni vyema tunapokula vyakula kuchagua vile ambavyo vina virutubisho sahihi ili kuweza kuimarisha afya pamoja na ngozi ya mwili wako.

Vyakula hivyo si vingine, bali ni vile vya kijani ambavyo vina uwezo mkubwa katika kuponya magonjwa na kusaidia pia kulinda, kujenga mwili na kuimarisha siha.

Hakuna asiyefahamu kuwa ngozi ni sehemu muhimu ya mwili ambayo inatakiwa kulindwa na kukingwa kwa kula vyakula vizuri na hata kulindwa na jua ambalo linaweza kupenya kwenye ngozi na kuifanya kukunjamana vyema.

Katika suala la vyakula unaweza ukajijengea mazoea ya kutumia asali mara kwa mara, mayai kwa kuwa hata kiini chake kina vitamini ‘A’ na ‘B’ huku sehemu yenye ute ikiwa na protini nyingi ambazo ni muhimu pia kwa ngozi.

Pia unatakiwa kula vyakula au matunda mengi yenye vitamin ‘C’ kama vile machungwa, limao, mapapai, maparachichi yenye protini kwa wingi, bila kusahau mbogamboga ni muhimu katika kuimarisha afya ya ngozi kwa sababu husaidia kutengeneza aina ya protini inayoitwa collagen inayotengeneza ubora wa ngozi.

Vitamini ‘C’ inasaidia kuondoa uvimbe na mikunjo ya ngozi na hivyo kuilinda ngozi isizeeke mapema.

Chakula kingine muhimu kwa ngozi ni shayiri ambayo ina kirutubisho kinachosaidia mafuta yanayolainisha ngozi.

Hivyo ukiwa mrembo ni vyema vyakula hivyo ukawa unavitumia mara kwa mara bila kusahau matunda yawe kwa wingi na hata unaponunua mafuta ya kupaka, hakikisha ndani yake kuna vitu hivyo.