Upimaji wa viwanja watakiwa kutambua wanyonge Nchini

Muktasari:

  • Kwani imebaninika kwamba wananchi wanajitahidi kujenga nyumba za kisasa, za kudumu na zenye vivutio vingi kutosheleza mapumziko ya wamiliki, wengi hawana hati. Nyumba, viwanja na mashamba mengi nchini hayana hati.

Binadamu tunatofautiana kwa mapato, na kila kitu ndio maana Serikali ikasema kwamba gharama za upimaji viwanja itambue wanyonge.

Kwani imebaninika kwamba wananchi wanajitahidi kujenga nyumba za kisasa, za kudumu na zenye vivutio vingi kutosheleza mapumziko ya wamiliki, wengi hawana hati. Nyumba, viwanja na mashamba mengi nchini hayana hati.

Hivi karibuni alipokuwa anazungumza na wawakilishi wa kampuni za upimaji wa viwanja na watendaji wa mitaa na vijiji vya kanda ya mashariki, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alizitaka kampuni hizo kuhakikisha wanatoa hati kwenye kila mradi watakaokuwa wanautekeleza.

Hati ambazo kiongozi huyo alikuwa akisema ni zile za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwani kuanzia hapo nyumba, kiwanja au shamba.

Alisema kwamba ikiwa kila mtu atakuwa na hati inakuwa rahisi hata thamani mbele ya taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba.

Amesema mpango huo pia unawahusisha wote waliojenga na wanaoishi kwenye makazi holela. Waziri ameagiza kurasmishwa kwa nyumba zote kwenye maeneo hayo kwa gharama isiyozidi Sh250,000.

Urasmishaji huo, pamoja na mambo mengine, unakusudia kuwapa wamiliki uwezi wa kukopa kutoka benki za biashara zinazotoa mikopo ya nyumba ingawa takwimu zinaonyesha uwiano wa wananchi wanaonufaika nayo ni chini ya asilimia moja ya pato la Taifa.

Kuharakisha upimaji, Serikali imeshusha mamlaka kutoka wizarani kwenda kwenye ofisi za kanda ambazo zitahudumia mikoa yote nchini. Kwa sasa kuna kanda nane zilizopo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara, Moshi, Simiyu, Mwanza, Dodoma na Tabora.

Pamoja na mipango mingine, ofisi hizo zinatakiwa kurahisisha urasmishaji wa makazi holela yaliyopo mjini katika halmashauri zote nchini. Utekelezaji wake uishirikishe sekta binafsi.

“Halmashauri zitoe zabuni kwa kampuni itakayokuwa na gharama ndogo zaidi. Hivi sasa nyingi zinawatoza wananchi kati ya Sh300,000 mpaka Sh850,000 jambo linalowaumiza,” anasema waziri huyu.

Takwimu zinaonyesha kuna kampuni 48 za upangaji miji na 42 za upimaji ardhi. Watalaamu wa kampuni hizi wana-takiwa kushirikiana na idara ya ardhi na mipango miji kuhakikisha wananchi hasa wenye kipato cha chini wana-rasmishwa.

Mpango wa Mkurabita ulidhamiria kurasimisha rasilimali za wanyonge ili kuukimbia umasikini. Mkurabita ulioanzishwa na kuanza kutekeleza miaka 15 iliyopita, ulikusudia kuongeza thamani ya ardhi, nyumba na majengo tofauti.

Kampuni za upangaji na upimaji miji ,watendaji wa Serikali za mitaa na ngazi ya wilaya kwa pamoja ushirikiano na wananchi ndio wataweza kufanikisha zoezi hili la urasimishaji.

Kwa mujibu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa kampuni ya Makazi Solution(T)LTD Ally Rashid alisema kwamba wamefurahishwa na uamuzi wa Serikali kupitisha uboreshaji wa miji(Town Planing) kuishia kwenye kanda kwani awali kulikuwa na changamoto upotezaji wa muda na kuzorotesha zoezi zima la upimaji.

Amesema kampuni yao hiyo imekuwa ikitoza gharama za urasimishaji wa kiwango kisichozidi Sh200,000 huku akizitaka kampuni nyingine kujali wananchi wa hali ya chini.

Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuna uhaba wa nyumba milioni tatu nchini na kila mwaka kunakuwa na ongezeko la mahitaji ya nyumba 200,000.

Kutokana na ukweli huo, mikopo ya nyumba inakuwa suala muhimu ambalo hata hivyo, Waziri Lukuvi anasema linakabiliwa na changamoto ya waendelezaji wa uhakika.

“Wananchi wengi huwa hawapewi nyumba bali maneno. Nimeiagiza BoT kutoiruhusu benki yoyote kutoa mkopo wa nyumba kabla mteja hajakabidhiwa nyumba,” anasema Lukuvi.

Kwa mujibu wa waziri huyo, wateja wengi wanaonunua nyumba zinazojengwa na taasisi zenye mamlaka hayo nchini hulazimika kusubiri mpaka miaka mitatu kabla ya kukabidhiwa fedha zao jambo linalowaumiza kwani licha ya kukatwa mishahara yao kutokana na mikopo waliyochukua benki, hulazimika kulipa kodi ya nyumba.

“Kuanzia sasa, nataka kampuni ziuze nyumba. Si mwananchi anakatwa na benki na bado analipa kodi kwenye nyumba aliyopanga,” anasisitiza.

Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC) huzikopesha benki za biashara ili nazo ziwakopeshe wananchi ili kuharakisha uboreshaji wa makazi nchini.

Pamoja na jukumu hilo, changamoto iliyopo ni uchache wa wananchi wenye hati za ama maeneo wanayoyamiliki au nyumba walizonazo suala linalosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mmoja wa maofisa wa TMRC aliyekuwa anatoa elimu kwenye maonyesho ya Sabasaba yaliyokamilika mwishoni mwa wiki iliyopita, anasema kwa wananchi wenye hati, hawapati usumbufu wowote kupata mkopo.

“Ukiwa na hati mbona utagombewa. Kila benki itataka kukukopesha,” anasema ofisa huyo ambaye si msemaji wa TMRC.

Kumbukumbu zinaonyesha kampuni hiyo yenye benki wanachama 33 ina zaidi ya Sh54 bilioni ilizokopeshwa na Benki ya Dunia ambazo zinapaswa kukopeshwa mpaka Juni mwakani.

Kufanikiwa kupata mkopo wa ama kujenga, kununua au kukarabati nyumba, mteja anahitaji kuwa na hati ya kiwanja au nyumba anayotaka kuinunua au kuikarabati.

Uratibu

Kuhakikisha wananchi wengi wanapata hati kutoka kwa kampuni binafsi zitakazoshirikiana na maofisa wa idara ya ardhi na mipango, kuanzia Julai Mosi halmashauri ndizo zinatakiwa kuratibu shughuli zote za upimaji, uendelezaji na urasmishaji wa maeneo badala ya mitaa kama ilivyokuwa zamani.

Utaratibu utakaotumika ni kila mtaa au kijiji kuwasilisha mahitaji yake halmashauri ambayo itapokea na kutangaza zabuni ya upimaji kwa kampuni binafsi kulingana na mipango iliyopo.

“Licha ya upimaji, halmashauri izungumze na kampuni husika kuweka gharama ya hati. Upimaji wowote utakaofanywa kuanzia Julai Mosi ni lazima umpe mwananchi hati yake,” anaaagiza waziri huyo.

Kuongeza hamasa kwa wananchi kurasmisha maeneo yao, Serikali imetangaza kupunguza tozo ya hati kutoka asilimia 2.5 mpaka asilimia moja. Punguzo litakalowahusu wanaotaka kurasmisha makazi yao hasa waishio kwenye makazi holela.

“Serikali inawatambua wananchi masikini hawana uwezo wa kuwafikiwa maofisa ardhi. Hawa wamepunguziwa ili nao wasiikose fursa ya kumiliko hati ya nyumba,” anasema.

Vifaa

Miongoni mwa vitu vinavyoongeza gharama za upimaji na upangaji miji ni vifaa vinavyotumika kufanikisha suala hilo. Kampuni nyingi binafsi, hulazimika kukodi baadhi kutokana na kutokuwa navyo vyote.

Gharama hizo huwarudisha nyuma baadhi ya wahitimu wa fani husika wenye uwezo wa kuanzisha kampuni na kusaidia kufanikisha upimaji na upangaji miji.