Utengenezaji chachandu utakuza kilimo cha pilipili

Muktasari:

Tulibako Minja, mkazi wa jijini hapa, anasema alianza kuwauzia wafanyakazi wenzake ofisini lakini hivi sasa anapata oda kutoka ng’ambo pia.

Dar es Salaam. Baada ya kupika chachandu ya pilipili kwa matumizi ya nyumbani kwa muda mrefu, aliigeuza kuwa fursa inayomuongezea kipato.

Tulibako Minja, mkazi wa jijini hapa, anasema alianza kuwauzia wafanyakazi wenzake ofisini lakini hivi sasa anapata oda kutoka ng’ambo pia.

“Mwanzo nilikuwa napika kwa ajili ya nyumbani lakini kila mgeni aliyekuwa akiionja akawa anaipenda. Nikaanza kuiuza ofisini na watu wakaipokea vizuri, wakawa wanaagiza mara kwa mara. nikaongeza uzalishaji,” anasema Tulibako.

Mwanzo alikuwa anatengeneza kwa maarifa yake binafsi lakini baada ya mahitaji kuongezeka alilazimika kupata mafunzo ya usindikikaji wa bidhaa zake kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).

Aanasema mwanzo alijifunza mwenyewe kwa kusoma na kuangalia baadhi ya video mtandaoni ili kuongeza ujuzi licha ya kuwa ni mhitimu wa shahada ya kilimo.

“Aina ya pilipili ninayoitengeneza ni chakulalishe kwa sababu inachanganywa na viungo mbalimbali ikiwemo, binzari, vitunguu swaumu na mbogamboga ambavyo huimarisha afya ya mlaji,” anasema.

Licha ya changamoto kadhaa zilizopo sokoni, Tulibako anasema wateja wake wameongezeka na sasa anapokea oda kutoka nje ya nchi.

“Wateja kutoka Marekani na Uingereza wanaagiza chachandu hii, tunawapalekea ingawa si kwa wingi mkubwa kutokana na uhaba wa vifungashio,” anasema.

Anafafanua kuwa wanavyotumia hivi sasa wanavitoa Kenya wakati mwingine wanalazimika kuviagiza kutoka China ili kukidhi mahitaji ya wateja pale ukubwa unaohitajika unapokuwa haupatikani Kenya.

Anao uwezo wa kupika hadi chupa 80 kwa siku zenye ujazo wa gramu 400 ingawa huwa anafungwa katika ujazo wa gramu 250 na gramu 100 pia.

“Chupa za gramu 400 tunauza Sh5,000 wakati zile za gramu 250 ni Sh3,000 na za gramu 100 huuzwa kwa Sh1,500. Tunafunga zaidi chupa zenye ujazo mkubwa kwakuwa zinapendwa zaidi,” anasema Tulibako.

Anasema uzalishaji umekuwa ukitegemeana kiasi cha oda anazopokea ingawa huwa anauza mpaka Sh100,000 kwa siku tangu alipoanza biashara hiyo mapema mwaka jana.

Akisaidiwa na mpishi mmoja anayemsaidia, anasema utengenezaji wa makopo 80 ya chachandu huhitaji ndoo tatu kubwa za pilipili zilizoiva.

Ndoo moja ya pilipili hizo hununuliwa kwa Sh10,000 wakati wa msimu wa mavuno lakini zikiadimika hufika mpaka Sh25,000. Anasema mabadiliko hayo husababishwa na kilimo cha kutegemea mvua hivyo kuwafanya wafanyabiashara kutokuwa na uhakika wa kupata malighafi muda wote.

Kukabiliana na ukosefu wa pilipili pindi zinapoadimika, anasema anao mkakati wa kudumu.

“Ukiingia mkataba, , wakulima watazalisha kwa wingi na utakuwa na uhakika wa malighafi muda wote jambo litakalokuepusha na mfumuko wa bei unaotokea wakati fulani,” anasema.