Wadau wajadili fursa, changamoto zilizopo sekta ya sukari

Muktasari:

Takwimu za Serikali zinaonyesha mahitaji ya sukari nchini ni tani 630,000 kwa mwaka ambazo kati yake, tani 485,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na tani 145,000 ni malighafi viwandani.

Sekta ya sukari imekuwa ikikabiriwa na changamoto kadhaa ambazo zimeilazimu Serikali na wadau kuchukua hatua kila mara.

Takwimu za Serikali zinaonyesha mahitaji ya sukari nchini ni tani 630,000 kwa mwaka ambazo kati yake, tani 485,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na tani 145,000 ni malighafi viwandani.

Licha ya kuwapo kwa wazalishaji wa ndani, wanaowashirikisha wakulima wadogo, uzalishaji bado hautoshi. Mabadiliko ya tabianchi na sababu nyinginezo bado zimeendelea kuwa kikwazo cha Tanzania kujitegemea kwa mahitaji yake ya bidhaa hiyo.

Alipokuwaa kisoma bajeti ya mwaka huu wa fedha, Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema ukame uliozikumba nchi za ukanda wa mashariki, kati na kusini mwa Afrika mwaka 2017/18 umesababisha Tanzania kushindwa kuzalisha tani 314,000 na kupata tani 300,399 pekee.

Kutokana na upungufu huo, Serikali hutoa kibali cha kuagiza sukari kutoka nje. “Kampuni nne zinazozalisha sukari ndizo zilizopewa jukumu la kuagiza sukari kwa masharti kuwa hakutakuwa na upungufu wa sukari nchini na ni lazima wapanue mashamba ya miwa ili mpaka mwaka 2020 Tanzania ijitosheleze,” alisema Mwijage.

Alipowasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitangaza ongezeko la ushuru wa forodha kwa asilimia 15 kutoka asilimia 25 mpaka asilimia 35 kwenye uingizaji wa sukari kwa lengo la kudhibiti upotevu wa mapato na kuhamasisha uzalishaji wa ndani.

Kudhibiti uingizaji holela wa sukari, Serikali imesema ni kampuni nne pekee zitapewa la kufanya hivyo. Mwijage alizitaja kampuni hizo kuwa ni Kilombero, TPC, Kagera na Mtibwa. Licha ya kibali hicho, kampuni hizo ndizo wazalishaji wa sukari nchini.

Haya yote yanafanyika baada ya Serikali kuendesha vita vya kukabiliana na magendo yaliyokuwa yanafanywa kwenye uingizaji na usambaji wa bidha ahiyo nchini na mataifa jirani yanayotumia Bandari ya Dar es Salaam.

Pamoja na hayo, kuna ujenzi wa viwanda vingine vya sukari unaoendelea maeneo tofauti vinavyotarajiwa kuleta unafuu wa bei na kuongeza upatikanaji wa sukari nchini.

Licha ya kuongeza uzalishajio, viwanda hivyo vitakuza ajira hasa kwa vijana, kuongeza fursa za kibiashara na uboreshaji wa miundombinu kwenye maeneo vinakojengwa.

Changamoto

Sukari ni bidhaa muhimu kwa matumizi ya nyumbani hata uzalishaji viwandani ingawa kwa miaka kadhaa ya nyuma kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hiyo na mfumuko wa bei.

Baadhi ya changamoto hizi huanzia kwenye mashamba ya miwa, kiwandani hata masoko hivyo kusababisha kuadimika kwa bidhaa hivyo kupanda kwa bei.

Kila mwaka, Mfuko wa Maendeleo ya Sukari kwa kushirikiana na Bodi ya Sukari Tanzania (TSB) huandaa mkutano wa wadau kujadili changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wake tena kwa bei nafuu.

Mkutano huo huvihusisha viwanda vya sukari, vyama vya wakulima wadogo wa miwa, taasisi za fedha na watendaji wa Serikali.

Licha ya kupanda kwa ushuru wa forodha kwa bidhaa hiyo inayoagizwa kutoka nje, mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Sukari, Deo Lyatto anasema itaendelea kuwa nafuu ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Lyatto anasema kuwa ushuru hauwezi kuathiri bei ya sukari na kuwatoa wasiwasi wananchi, wafanyabiashara na wadau wengine wa sukari.

Kuhusu sukari inayozalishwa nchini, mwenyekiti huyo anasema: “Ipo salama kwa matumizi kutokana na uangalizi wa mamlaka za udhibiti.”

Anasema kwa sasa uzalishaji wa sukari nchini ni tani 535,000 kwa mwaka kiasi kitakachoongezeka hadi tani 580,000 mwaka 2021 kipindi ambacho matumizi ya sukari ya viwandani itaongezeka kutoka tani 160,000 hadi 175,000.

Ongezeka hilo la uzalishaji linatokana na uanzishwaji wa viwanda vya sukari kikiwamo cha Mbigiri na Mkulazi vilivyopo mkoani Morogoro na kingine huko Bagamoyo mkoani Pwani.

Uingizaji wa sukari ya nje anasema ni changamoto inayoathiri soko na kutishia kufa kwa viwanda vya ndani endapo udhibiti makini hautafanywa.

Mwenyekiti wa muungano wa vyama vya wakulima wa miwa nchini (Tasga), Dk George Mlingwa anasema viwanda vinavyoanzishwa hivi sasa vinaweza vikashindwa kukua ama kujiendesha endapo sukari ya nje itaingizwa na kupatikana kwa wingi kisha kuuzwa kwa bei ya chini.

“Iwepo mipango madhubuti ya kuvilinda viwanda vya ndani kwa kutoruhusu uingizaji wa sukari ya nje ambayo huathiri kipato cha wakulima wa miwa kwa namna moja au nyingine,” anapendekeza mwenyekiti huyo.

Miongoni mwa vilivyopo kwenye hatua za ujenzi ni pamoja na kiwanda cha sukari Mkulazi cha Wilaya ya Morogoro.

Utekelezaji wa mradi huo unakwenda sambamba na ujenzi wa bwawa kubwa la Kidunda ambalo litatumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika mashamba ya miwa ya Mkulazi.

Mikakati

Kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wa uhakika, wataalamu wameweka mkakati wakufanya utafiti wa maeneo yote muhimu yanayogusa kilimo cha miwa mpaka upatikanaji wa masoko ya uhakika ya sukari.

Utafiti huu unafanywa kuanzia kwenye udongo unaofaa kwa kilimo cha miwa, mbegu zinazostahimili hali ya hewa na kufaa kwenye udongo husika, magonjwa na wadudu wanaoshambulia miwa pamoja na dawa zinazoweza kuangamiza wadudu hao waharibifu.

Mtafiti kiongozi wa Kituo cha Utafiti Kibaha, Dk Hildelita Msita anasema kwa sasa wanaendea na utafiti wa mbegu bora zenye zitakazoongeza tija pamoja utafiti wa wadudu waharibifu na dawa za kukabiliana nao.

“Kwa sasa tupo kwenye utafiti wa kubaini dawa sahihi itakayoua wadudu wanaojulikana kama vidung’ata wa njano ambao wanatishia miwa,” anasema.

Wadudu wengine waharibifu wanaotafutiwa dawa ni aldana, magamba meupe na funza wa miwa. Katika hatua za awali, wadudu hao wameweza kudhibitiwa kwa kutumia mbegu za miwa inayokinzana nao.

Katika hatua nyingine wakulima wa miwa wamelalamikia kupanda kwa bei ya dawa na mbolea kwa zaidi ya mara mbili.

Mmoja wa wakulima wa miwa kutoka Kilombero, Bakari Mkangamo anasema kilimo cha miwa kinahitaji mtaji na elimu ya kutosha hivyo taasisi za fedha hasa benki za biashara zina wajibu wa kuwawezesha wakulima kukuza uwezo wao ili walime kisasa.

“Zipo baadhi ya benki zinatukopesha lakini ushindani ukiongezeka tutapata unafuu. Mkulima mwenye mtaji wa kutosha ana uhakika wa kuvuna kwani anamudu kila kinachohitajika wakati wa kilimo,” anasema Mkangamo.

CRDB ni miongoni mwa benki zinazotoa mikopo kwa vikundi vya wakulima wa miwa wilayani Kilombero. Meneja kilimobiashara wa benki hiyo, Ngenzi Sylivester anasema wametenga Sh1 trilioni kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda.

“Kiasi hicho kitatolewa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2018 hadi 2022. Kwenye sekta ya sukari, benki hiyo imetenga Sh100 bilioni,” anabainisha.

Baada ya vyama vya wakulima kuwa ushirika, meneja huyo anashauri vianzishe kampuni na kutafuta wataalamu wa kusimamia kilimo na uandaaji wa mashamba.