Wafanyakazi hawaachi kazi bali wanaachana na bosi wao

Muktasari:

  • Ni nadra kusikia bosi akitajwa kama sababu ya mfanyakazi kuacha kazi.

Mara nyingi ukisikiliza sababu zinazowafanya watu waache kazi, masuala yanayotajwa zaidi ni masilahi duni, mazingira ya kazi yanayokatisha tamaa.

Ni nadra kusikia bosi akitajwa kama sababu ya mfanyakazi kuacha kazi.

Ingawa kuna ukweli kuwa watu huacha kazi kufuata masilahi zaidi, mazingira bora ya kazi, lakini mara nyingi sababu kubwa ya wafanyakazi kuamua kuhama au kuacha kazi ni kukimbia uongozi mbovu katika maeneo ya kazi.

Nandipa Matabane (sio jina lake halisi) anatoa mfano. “Nakumbuka wakati naacha kazi yangu ya kwanza tulipishana sana na bosi wangu. Maisha yangu kazini yalikuwa magumu. Ilifika mahali bosi akawa ananitafutia sababu ya kuniondoa. Ilibidi niache kazi ingawa kwa kweli sikuwa nimejiandaa kufanya hivyo. Nilipata kazi isiyo na kipato kikubwa ikilinganishwa na ya kwanza. Lakini ilikuwa afadhali mara 100 kuliko kuendelea kukaa kwenye mazingira mabovu namna ile.”

Nandipa anataja sababu nyingine kuwa alifika mahali akawa hajifunzi kitu kipya kwenye kazi yake ya awali. Karibu kila alichokuwa anakifanya kila siku hakikuwa tofauti na alichokifanya miaka miwili iliyopita. Hata hivyo, bado anasisitiza namna uongozi mbaya ulivyochangia yeye kuacha kazi.

“Kama uongozi ungebadilika, nina hakika bado ningekuwa kule. Haikuwa kazi mbaya kivile. Kuondoka kwangu kulikuwa ni namna tu ya kuachana nameneja asiyejua uongozi,” anafafanua.

Kama kiongozi wa taasisi au kampuni, bila shaka ungependa kubadilisha timu yako mara kwa mara. Unapokuwa na timu ya watu wenye uzoefu na wasiofikiria namna ya kuachana na wewe, uwezekano wa taasisi au kampuni yako kuzalisha zaidi na kutoa huduma zenye kiwango bora unakuwa mkubwa. Je, unaweza kufanya nini kuhakikisha kuwa wafanyakazi wako hawakukimbii?

Jenga ukaribu na wafanyakazi

Sababu moja wapo inayoweza kufanya watu wakachoka mazingira ya kazi ni ule umbali unaokuwepo kati yao na wewe uliye kiongozi wao. Umbali ni ile hali ya wewe kutokufikika kwa sababu mwenzetu umejizungushia ukuta unaokutenga na watu unaowaongoza.

Hali hii ina athari kubwa mbili. Kwanza, watu huanza kukuona kama mtu usiyejali ustawi wao. Unapoanza kuonekana hujali, maana yake unakaribisha mazingira ya watu kukosa hamasa ya kazi. Lakini pili, umbali huzalisha woga. Watu wanaokuogopa hawawezi kufanya kazi kwa kujituma.

Jaribu kujenga mazingira yanayowawezesha wafanyakazi kujisikia karibu na wewe. Mavazi unayovaa, mathalani, yanaweza kuwafanya watu wakajisikia huru kukufikia. Huna sababu ya kuvaa suti kila siku ili uonekane ni kiongozi. Mavazi ya kawaida hayaondoi mamlaka yako kama kiongozi.

Lakini pia kuna kujichanganya na watu. Mamlaka yako hayategemei namnaunavyoogopwa na watu wa chini yako. Kaa karibu na watu; kula nao, ongea nao kujua yanayoendelea kwenye maisha yao ya kawaida. Kama unaweza jua matamanio yao ya kujikuza kiujuzi fanya hivyo. Unapofanya mambo

kama haya wanawafanya watu waone eneo la kazi ni salama kwao.

Heshimu kazi za waliochini yako

Kama kiongozi, utendaji wako, kwa kiasi kikubwa, unategemea namna gani walio chini yako wanavyofanya kazi zao kwa ufanisi. Kipimo cha uongozi ni tofauti na kipimo cha utendaji wa mfanyakazi wa kawaida.

Unapokuwa mfanyakazi wa kawaida, utendaji wako unapimwa kwa uwezo wako wa kutekeleza majukumu yako binafsi. Wakati mwingine majukumu haya hayaingiliani na majukumu ya wenzako. Ukikamilisha kazi zako, inatosha.

Unapopata nafasi ya kuwa kiongozi, mambo yanabadilika –wakati mwingine ghafla. Badala ya utendaji wako kuangaliwa kwa vile unavyotekeleza kazi zako zisizowategemea wengine, kazi yako inabadilika na kuanza kutegemea namna gani unawawezesha watu wa chini yako kutekeleza majukumu yao.

Bahati mbaya ni kwamba ufanisi wako mzuri kama mfanyakazi unaweza usikusaidie unapokuwa kiongozi. Kama kiongozi unahitaji ujuzi mpya wa namna ya kuweka mazingira rafiki yanayowahamasisha watu kufanya kazi zao.

Mara nyingi watu wanaoteuliwa kupata nafasi za uongozi hawapati mafunzo yanayowawezesha kupata ujuzi wa namna ya kuongoza watu.

Watu hawa wanaotegemewa kuongoza watu wengine wanakuwa

hawajaandaliwa kuwa viongozi. Hali hii inaweza kuzalisha misuguano isiyo na sababu.

Kama kiongozi lazima kutambua kuwa sehemu kubwa ya muda wako inakuwa ni kuwawezesha watu wengine kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Achana na mazoea ya ‘kupambana’ kivyako vyako ili kujipatia sifa binafsi.

Jifunze kuwawezesha wengine kufanya kazi kama timu.

Wawezeshe kujifunza ujuzi mpya

Moja wapo ya malalamiko ya wafanyakazi wengi ni tabia ya viongozi wao kutokuvumilia makosa. Ingawa ni kweli yapo makosa yasiyovumilika, lakinikutokutegemea kuwa walio chini wanaweza kufanya makosa ya kawaida kama namna ya kujifunza, ni kukosa sifa za uongozi.

Niliwahi kufanya kazi na kiongozi mmoja aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuvumilia. Kiongozi huyu si tu alinivumilia lakini pia alihakikisha anakuwa mwalimu wangu wa kazi. Kila alipoona mapungufu kwenye utendaji wangu,alinielekeza mahali pa ninakoweza kujifunza zaidi.

Nikajifunza kuwa uongozi bora katika maeneo ya kazi unahitaji uwezo wa kuvumilia makosa. Kiongozi si mviziaji anayetafuta wakosaji. Kiongozi ni mwalimu anayewasaidia anaowaongoza kuwa watu bora zaidi.

Wakati mwingine majukumu yale yale kwa muda mrefu yanaweza kumfanya mtu akafika mahali hana jipya kazini. Kama kiongozi, kazi yako sio kutafuta namna ya kumtoa. Fikiria unavyoweza kumsaidia kujifunza mambo mapya kwa ama kumbadilishia kazi itakayomlazimisha kujifunza ujuzi mpya, au kumwendeleza kiujuzi kwa kumpeleka kwenye mafunzo.

Usiwe kiongozi unayekaa kusubiri watu wafanye makosa. Hupati faida kutafuta timu mpya kila mara. Weka mfumo mzuri unaowawezesha watu wako kujifunza. Ukifanya hivyo, watu hawatageuza eneo lako la kazi kuwa sehemu ya kutafuta uzoefu na kupita.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu chaKikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya Simu:0754870815