Zijue siku 21 za kupata vifaranga kwenye mayai-2

Muktasari:

Pengine kuna maswali mengi juu ya muda wa mayai kuanguliwa. Mtu anaweza asijue kuwa kila aina ya ndege ana siku zake za kuangua mayai.

Ni mwendelezo wa mada ya kuzalisha vifaranga kutoka kwenye mayai ya kuku.

Makala yaliyopita yaligusia sehemu m uhimu katika utototeshaji, lakini mambo mengine mengi hayakuguswa.

Pengine kuna maswali mengi juu ya muda wa mayai kuanguliwa. Mtu anaweza asijue kuwa kila aina ya ndege ana siku zake za kuangua mayai.

Kwa mfano, mayai ya bata, njiwa, kware na kuku huanguliwa kwa siku tofauti. Njiwa huangua vifaranga baada ya siku 17 za kulalia mayai.

Kuku huangua baada ya siku siku 21 kulalia mayai, huku bata akiangua vifaranga baada ya siku 28 za kulalia mayai.

Wafugaji wanaotumia mashine kuangulisha wanatakiwa kufuata maelekezo kulingana na aina ya mayai ya ndege wanayotaka kutotolesha.

Iandae mashine vizuri kulingana na aina ya mayai unayotaka kuangulisha. Soma mwongozo wa mashine husika kwa sababu kila mashine huuzwa pamoja na mwongozo wake. Au pata ushauri wa kina kutoka kwa mtaalamu au mtu mwenye uzoefu wa mashine husika kwa muda mrefu.

Kama unatotolesha kwa njia ya asili, hakikisha aina ya ndege husika ndiye anayelalia mayai hayo. Ikiwa unatumia aina nyingine ya ndege kulalia mayai, hakikisha ndege anayelalia mayai ana asili ya kulalia kwa muda unaofanana na ndege mwenye mayai au zaidi.

Kwa mfano, bata anaweza kulalia mayai ya kuku, lakini kuku hawezi kulalia mayai ya bata, kwa kuwa atayaacha kabla hayajaanguliwa, kwa sababu kuku hulalia kwa siku 21, ilhali bata hulalia hadi siku 28 au 30.

Mambo muhimu katika utotoleshaji

Baada ya kuona tofauti hizo za uanguaji, tuangalie mambo mengine muhimu katika utotoleshaji baada ya kuona mambo matatu kwenye makala yaliyopita ikiwamo umuhimu wa mbegu ya jogoo kwenye mayai ya kuangulisha.

Jambo la nne ni maambukizi. Magonjwa huathiri afya ya kuku na ukuaji wa vifaranga walioko kwenye mayai. Ni jambo la kawaida kwa mayai kushindwa kuanguliwa hata kama yana mbegu za jogoo ndani endapo kuku waliotaga mayai hayo ni wagonjwa.

Yapo magonjwa ambayo huzuia ukuaji wa vifaranga kwenye mayai kabla hawajaanguliwa na mengine hushambulia vifaranga baada ya kuanguliwa.

Tano ni lishe. Kuku wenye lishe duni hawana virutubisho kwenye mayai vya kutosha, hivyo matokeo yake vifaranga hukosa nguvu na kufia kwenye mayai kabla ya kutoka.

Mfugaji anatakiwa kulisha chakula bora kwa kuku wanaotaga na kuwapa vitamini mara kwa mara hasa ikiwa ni kuku wanaofungiwa ndani.

Sita ni joto la mashine ya kuangulishia. Mfugaji anayeangua kwa njia ya asili, anategemea kuku wapashe joto mayai

Lakini kwa mtu anayetumia mashine, inatakiwa mashine itoe joto na unyevu unaotakiwa. Kupanda au kushuka kwa joto kuliko inavyotakiwa, kutasababisha mayai kutoanguliwa.

Ongezeko la joto kidogo zaidi ya kiwango mara nyingi huwahisha vifaranga kuanguliwa siku moja au mbili kabla ya siku ya 21 kwa mayai ya kuku.

Aidha, kupungua kwa joto kidogo chini ya kiwango huchelewesha mayai kuanguliwa. Vilevile unyevu ukipungua sana vifaranga hutoka wakiwa wadogo wadogo au pengine hushindwa kuvunja ganda la yai ambalo kifaranga hulazimika kulitoboa kwa kuligonga na mdomo wake.

Saba ni ukubwa wa mayai. Mayai makubwa sana hayafai kuangulisha. Mayai haya mara nyingi huwa na viini viwili ndani yake ambavyo hutoa mapacha.

Hata hivyo, sio rahisi vifaranga wawili kuishi hadi kuanguliwa wakiwa kwenye yai moja; mara nyingi hufia ndani kwa kukosa lishe, hewa na nafasi. Hivyo mayai yenye viini viwili hayafai kuanglisha.

Mbali na mayai yenye viini viwili, mayai yenye ganda gumu kama vile mayai ya kuku wazee hutagwa yakiwa na ganda gumu, hivyo vifaranga huchelewa kutoka ikilingalishwa na mayai ya kuku wanaoanza kutaga.

Nane ni kugeuza mayai. Mayai yanahitaji kugeuzwa mara kwa mara yakiwa yanapata joto la kuku au joto la mashine.

Ni kama mtu anayekaanga chapati kila baada ya muda anageuza chapati jikoni. Hivi ndivyo hata kwa kuku akiwa amelala kwenye mayai kila baada ya muda hugeuza mayai yote.

Kazi hiyo ya mayai kugeuzwa hufanyika pia kwenye utotoleshaji kwa njia ya mashine. Kila baada ya muda mashine hugeuza trei za mayai nyuzi 45 kulia na kushoto.

Mayai yakikaa bila kugeuzwa, hushindwa kuanguliwa hivyo vifaranga hugandia kwenye ganda walikolalia na kufa.

Tisa ni usafi. Safisha mashine kila mara kwa kuondoa mabaki ya mayai na vifaranga waliokufa. Pia puliza dawa kuondoa mazalia ya vimelea vya magonjwa. Safisha mashine kwa maji safi na sabuni na kuacha ikauke kabla ya kuweka mayai mengine mapya. Zingatia kanuni zote za afya ikiwemo kuwa na sehemu maalumu ya kufukia uchafu na kuchoma mabaki yote. Toa chanjo kwa vifaranga walioanguliwa kulingana na kalenda ya utoaji chanjo. Weka vitu vya kuzuia baridi na vipasha joto kwa vifaranga ili wasife kwa baridi.