Mwanga wa mabadiliko unavyoitikisa Ethiopia

Muktasari:

  • Mwanzoni mwa Aprili, Waziri mkuu mpya, Abiy Ahmed Ali aliapishwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Haille Mariam Desalegn aliyejiuzulu katikati ya Februari.

Wiki hii kumekuwa na habari za mwendelezo wa mabadiliko makubwa yanayoendelea nchini Ethiopia, ambayo kwa hakika yanawaacha vinywa wazi wafuatiliaji wa siasa za nchi hiyo na kama si kihoro kwa madikteta ndani ya Muungano wa vyama vya kisiasa vinavyoongoza nchi hiyo –Ethiopian Peoples Revolutionary Democratic Front (EPRDF) na hasa wale wanaotokea Jimbo la Tigrey na chama chao cha Tigrayan Peoples Liberation Front (TPLF).

Mwanzoni mwa Aprili, Waziri mkuu mpya, Abiy Ahmed Ali aliapishwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Haille Mariam Desalegn aliyejiuzulu katikati ya Februari.

Abiy Ahmed Ali ni Waziri Mkuu wa 16 na wa kwanza kutoka katika kabila lenye idadi kubwa ya watu la Oromo.

Desalegn alijiuzulu kwa kile alichokiita kutoa nafasi kwa chama chake kumtafuta mrithi ambaye ataiongoza nchi hiyo kuelekea katika utawala wa kidemokrasia utakaojali haki za kibinadamu kwa sababu yeye alikuwa ameshindwa.

Lakini, kwa wanaojua mfumo wa utawala wa nchi hiyo, hasa ndani ya EPRDF, waliona dhahiri kuwa kilichomwondoa msomi huyu katika nafasi yake ni kule kushindwa kudhibiti umma wa nchi hiyo ambao ulikuwa umeamua kupaza kilio cha kudai mabadiliko ya kidemokrasia, haki za kiuchumi na za kibinadamu kwa njia ya maandamano na migomo.

Alipoapishwa Abiy, ambaye ni mwanajeshi mwenye cheo cha Luteni Kanali, msomi mwenye shahada ya uzamivu na mtaalam wa mambo ya mawasiliano na ujasusi, aliahidi kuwa atafanya kila awezalo kutimiza matakwa ya wananchi wa nchi hiyo ambao walikuwa wakiisha chini ya utawala wa kidikteta ambao katika siku zake za mwisho ulijiwekea sheria za utawala wa hali ya hatari na hivyo kuzidisha nguvu ya mkono wa chuma iliokuwepo awali.

Hata kabla ya miezi miwili kupita amelishawishi Bunge la nchi hiyo ambalo kwa sehemu kubwa ni la wanachama wa EPRDF kuondoa hali ya hatari ambayo ilitakiwa kufikia kikomo Agosti.

Pia, Bunge lilikubali kuondoa hali ya uhasama iliyokuwepo kati yake na nchi jirani ya Eritrea ambayo ilikuwa sehemu ya shirikisho la Ethiopia kabla ya kujiondoa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuitambua hukumu iliyotolewa na Mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya mipaka kati ya nchi na nchi, iliyoamua kuhusu eneo la mpaka lililokuwa likigombaniwa kati ya nchi hizo na ambalo lilipelekea vita kamili mwaka 1998.

Matokeo ya mabadiliko

Katika kile kinachoitwa makubaliano ya Algiers ya mwa 2000, Ethiopia itaukabidhi mji wa mpakani wa Badme kwa Eritrea ili kumaliza uhasama na kutoaminiana miongoni mwao.

Waziri mkuu amekwenda mbali zaidi kwa kuwaachia mamia ya wafungwa wa kisiasa, waandishi wa habari na wanaharakati ambao walikuwa katika magereza mbalimbali ya nchi hiyo.

Amewaruhusu wale waliokuwa uhamishoni kurejea nchini humo, kuanzisha majadiliano ya maridhiano kati ya upande wa Serikali na wapinzani na kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ambayo yaliathiriwa sana na maandamano na migomo ya kupinga serikali huku akiomba msamaha kwa madhira yaliyowakuta wananchi wa maeneo hayo.

Kwa upande wa kiuchumi, amewashawishi wenzake katika kamati kuu ya EPRDF kukubali kuyaingiza katika ubia na ushindani mashirika makubwa kama lile la ndege, Ethiopian Airlines, Shirika la simu, Ethio Telecom na lile la reli, jambo ambalo lilikuwa halifikiriki kabisa katika siku za hivi karibuni.

Kwa sababu walio ndani ya Serikali wamekuwa wakiyachukulia mashirika hayo kama ng’ombe wao wa maziwa wasiotakiwa kuguswa na yeyote.

Baadhi ya Waethiopia waliozungumza na vyombo vya habari wameonyesha kushangazwa na kasi hii ya mabadiliko ambayo inaendelea kupenya ndani ya nchi hiyo na kujiuliza ilikuwaje mtangulizi wake alishindwa ingawa alikuwa akiahidi angefanya hivyo?

Licha ya kutoka katika kabila kubwa la Oromo, kuwa kwake mwanajeshi kunaweza kumsaidia kuleta ushawishi bila kupata upinzani mkubwa kutoka kwa wenzake ambao kwa hakika ni wanajeshi waliojibadili na kuwa wanasiasa, tofauti na Desalegn ambaye alikuwa ni raia kwa asilimia mia.

Ali ni kiongozi wa chama cha Oromo Peoples Democratic Organisation (OPDO) na vilevile EPRDF ambapo kiutaratibu anakuwa Waziri Mkuu. Vyama au vikundi vinavyounda EPRDF ni vinne ambavyo ni Tigrayan Peoples Liberation Front (TPLF), Southern Ethiopian Peoples Democratic Movement (SEPDM), Oromo Peoples Democratic Organisation (OPDO) na Amhara National Democratic Movement (ANDM).

Chama cha EPRDF kinaundwa na vikundi vya waasi waliokuwa wakimpinga mtawala wa wakati huo aliyeegemea mfumo wa Kikomunisti Mengistu, Haille Mariam ambaye alimwondoa mfalme Haille Selassie mwaka 1974 na yeye kuondolewa mwaka 1991.

Waasi hao kutoka jimbo la Tigrey wakiongozwa na Meles Zenawi walimtimua akakimbilia ukimbizini Zimbabwe anakoiishi mpaka sasa.

Majimbo yanayounda Shirikisho la nchi ya Ethiopia ni pamoja na Oromo, Afar, Somali, Gambela, Tigrey, Amhara, Harari, Southern Nationalities na Benishangul-Gumuz.

Waziri Mkuu mpya amewanyooshea kidole cha tahadhari watu wa makabila ya Tigrinya na Amhara ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiwadharau Waoromo kuwa hawana uwezo wa kuongoza Serikali na hii kwa kiasi kikubwa ilitokana na tabia ya enzi ya watu wa kabila hili ya kujishughulisha zaidi na kilimo na ufugaji ambayo ilisababisha waliokuwa wakishikilia mamlaka ndani ya serikali kuwakandamiza na kuwabagua.

Upande wa Ethiopia

Mabadiliko haya yanatoa mwanya kwa wananchi wa Eritrea kudai haki zao za kidemokrasia kutoka kwa Rais Isaias Afeweki, ambaye ameiweka nchi yake katika hali ya kivita kwa kisingizio cha uhasama na Ethiopia na hivyo kudumaza demokrasia.

Majeshi ya nchi mbili hizi yamekuwa mpakani yakiwa katika hali ya tahadhari kwa muda mrefu.

Vilevile ujio wa Ali kumeonyesha jinsi ambavyo nia na dhamira ya umma pale inapotaka mabadiliko hakuna cha kuzuia hata kama kwa vifaru na mitutu ya bunduki kwani kwa kipindi cha miaka mitatu wananchi wa taifa hili waliendesha migomo na maandamano ambayo yalisababisha mamia ya watu kufa na maelfu kukamatwa.

Licha ya mafanikio ya kipindi kifupi, lakini Ali anakabiliwa na changamoto mbalimbali ndani ya chama chake na uongozi wa juu wa jeshi ambao unashikiliwa na Watigrinya ambao wengi wamekuwa wakiona amekuwa na haraka katika kufanya mageuzi.

Wao wanapendelea kuendelea na utawala wa mgongo wa chuma na mpango wake wa kuliondoa jeshi katika shughuli za kisiasa nao unaonekana kuwa mwiba mkali kwa wahafidhina ndani ya EPRDF.

Katiba ya nchi ilipotengenezwa ilijikita katika kuyatambua makabila na majimbo kama mfumo rasmi wa kiutawala ambao kwa bahati mbaya umeshindwa kuunganisha wananchi wa taifa hili.

Maandamano na migomo ambayo ilimwondoa mtangulizi wake ilitokana na sababu nyingi, lakini zilizo kubwa ni pamoja na ubaguzi wa wazi katika nafasi za kazi na kiuchumi ambapo upatikanaji wa ajira katika ofisi za serikali, kampuni binafsi na taasisi zisizo za kiserikali umekuwa kwa kiasi kikubwa ni wa kujuana kikabila, kijimbo na hata kindugu zaidi.

Hivyo, makundi makubwa ya vijana ambao wengine wamefanikiwa kupata elimu ya chuo kikuu waliachwa nje ya mfumo wa ajira. Vijana wengi wanajitahidi kuihama nchi kwa kwenda nchi za nje kwa kutumia kila aina ya mbinu ili mradi waondoke.

Mgawanyo wa raslimali za nchi hii ni moja ya malalamiko ya watu wa taifa hili ambao wanaona kuwa kuna kikundi cha wachache walio karibu na watawala na ndiyo wanaofaidi keki ya taifa ili hali walio wengi wakiachwa nje.

Hivyo ni kusubiri na kuona namna Ali atakavyojitahidi kupambana na changamoto zinazolikabili taifa hili na kwa kuwa hakujipa muda kama walivyo wengine basi ana nafasi nzuri ya kutohojiwa mapema.

Waethiopia wametoa somo kubwa kwa wakazi na viongozi wa bara hili kuwa vyovyote iwavyo nguvu ya umma ikisimama katika kudai haki si mtutu wa bunduki wala vifaru vinaweza kuuangamiza.

[email protected], 0783165487