Anatoka Harvey anaingia Omotola katika tuzo za Oscar

Muktasari:

  • Weinstein aliondolewa katika tuzo hizo baada ya kukumbwa na kashfa ya unyanyasaji wa kingono kwa wanawake katika kipindi cha miaka tofauti.

Unaikumbuka kashfa iliyomuondoa bilionea wa filamu Harvey Weinstein katika tuzo za Oscar? Huenda imeleta neema kwa mwigizaji wa Nigeria, Omotola Jalade ambaye amekula shavu.

Weinstein aliondolewa katika tuzo hizo baada ya kukumbwa na kashfa ya unyanyasaji wa kingono kwa wanawake katika kipindi cha miaka tofauti.

Wakati Weistein akilia kwa kukabiliana na mkono wa sheria na kuondolewa katika tuzo hizo kubwa za filamu duniani, Omotola anacheka baada ya kuangukiwa na bahati ya mtende.

Omotola au Omosexy kama anavyoitwa na mashabiki wake, mapema wiki hii ameteuliwa kuwa mmoja wa wanachama wanaopiga kura katika tuzo hizo.

Mwigizaji huyo mwenye umri wa miaka 41 anakuwa mmoja kati ya watu 928 wanaopiga kura kupendekeza filamu, watayarishaji na waigizaji waliofanya vizuri katika tasnia hiyo.

Omotola amepenya katika orodha hiyo kutokana na kazi zake nzuri alizofanya katika tasnia ya filamu nchini Nigeria.

Jopo la majaji lilimteua Omotola baada ya kupitia kazi zake mbili alizofanya ambazo ni ‘A Private Storm’ na ‘Last Flight to Abuja’.

Filamu ya ‘A Private Storm’ aliyoitengeneza kwa kushirikiana na Imasuen na Ikechukwu Onyeka, ilishinda tuzo tatu za Africa Movie Academy Awards.

Na filamu ya ‘Last Flight to Abuja’, iliyoandikwa na Tunde Babalola ilishinda tuzo moja ya Africa Movie Academy Awards award for ‘Best film by an African based abroad’.

Tangu aingie kwenye filamu mwanzoni mwa mwaka 1995, Omosexy ameigiza katika filamu zaidi ya 300 zilizouza mamilioni ya nakala.

Mwaka 2013 alitajwa kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi duniani sambamba na Michelle Obama, Beyonce na Kate Middleton.