MAONI YA MHARIRI: Elimu kwa umma inahitajika kupambana na usonji

Kwa walio wengi, usonji unaweza kuwa msamiati mpya masikioni ama machoni.

Hata hivyo, watu wengi hasa wazazi wameshakumbana na hali hiyo pasipo kujua kuwa wanakabiliana na tatizo tete la kiafya kwa watoto wao.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kati ya watoto 160 duniani, mtoto mmoja yupo kwenye hatari ya kuugua usonji.

Kama tulivyobainisha hapo awali, usonji unaweza kuwa msamiati mgeni, lakini ukweli ni kuwa kadri siku zinavyokwenda, watoto zaidi nchini wanakabiliwa na tishio lake.

Bahati mbaya ni kuwa wengi wakiwamo wadau wa masuala ya afya hawauzungumzii ugonjwa huu kwa mapana yake, hali inayowafanya wazazi wengi kubabaika wanapokumbana na hali hii kwa watoto wao, kiasi cha kuufananisha na magonjwa ya akili.

Huu ni udhaifu unaotusukuma kuziomba mamlaka husika katika sekta ya afya, taasisi na wadau kwa jumla kuwa na mkakati madhubuti wa kupambana na ugonjwa huu, huku tukihamasisha zaidi elimu kwa jamii. Ni vyema sasa tukaeleza kwa undani kuhusu ugonjwa huu.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa usonji ni tatizo linalojitokeza mapema utotoni, ambapo mtoto hujenga tabia ya kupenda kujitenga na kutotaka kuwa karibu na watu, hupata matatizo ya lugha na shida ya mawasiliano na huwa na tabia ya kurudia rudia kitu anachokifanya mara nyingi.

Mara nyingi wazazi makini hugundua watoto wao wana tatizo hili katika kipindi cha miaka miwili ya umri wa mtoto. Chanzo halisi cha tatizo hili la usonji hakijulikani ingawa matatizo ya kijenetiki yanatajwa kuhusika na tatizo hili.

Lakini pia matumizi ya pombe na dawa za kulevya aina ya coccaine wakati wa ujauzito na hata sababu za kimazingira; vyote hivi vinahusishwa na tatizo hili la usonji.

Wataalamu wanaeleza kuwa watoto wa kiume wako katika hatari zaidi ya kuathirika na usonji kuliko wenzao wa kike. Kwa kila watoto watatu wenye usonji, ni mtoto mmoja tu wa kike anayeweza kuathirika.

Ili uweze kumtambua mtoto mwenye usonji, zipo dalili zinazoonyeshwa na mtoto huyo.

Miongoni mwa tabia hizo ni pamoja na kushindwa kuonyesha uwezo wake wa kuelewa na kutafsiri hisia za watu wengine.

Wataalamu wa afya wanasema mtoto mwenye usonji anaweza kuwa na upungufu kwenye kutambua hali ya kukasirika inayoonyeshwa na mtu mwingine.

Wanasema jambo hilo linaweza kuonekana na wengine kuwa huenda mtoto huyo ana dharau, mtukutu au hajali kitu.

Mtoto mwenye usonji mara nyingi hupendelea kucheza peke yake, hapendi kushirikiana na wengine na hata akishirikiana na wenzake, bado uwezo wake unakuwa wa kiwango cha chini ambao hauwezi kumwezesha kuwaruhusu wenzake hao watumie au kuchezea vitu vyake. Hali kama hii ndiyo mara nyingi huwafanya watu wamchukulie kuwa ni mchoyo. Tunasisitiza kuwa elimu kwa umma ni mkakati bora zaidi kwa kuwa itasaidia kutuweka mbali na vyanzo vya ugonjwa huu.

Ni kupitia elimu hii, pia wazazi watabaini haja ya kuwapa fursa za kielimu watoto wao wenye usonji, kwa kuwa wana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kielimu na hata kujifunza stadi muhimu za kimaisha.