KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Maprofesa, Elimu-Afya na Kiswahili

Ndimara Tegambwage

Inawezekana hukuwepo, hukusikia, hujasoma wala kusimuliwa yaliyotokea nchini Tanzania, tarehe 28 Juni mwaka huu ambayo yanathibitisha umuhimu na nguvu ya Kiswahili.

Gazeti hili limekuwa likichapisha habari na makala juu ya tukio la Juni 28.

Kwa hiyo, kama una taarifa, hapa ninakuongezea utamu wa siku ile. Kama uliishasahau, hapa ninakukumbusha. Kama huna taarifa, kaa sawa nikupashe.

Usiku wa Juni 28 katika ukumbi wa Kisenga, Jengo la Millennium Tower, jijini Dar es Salaam, watu 427 waliketi vitini katika eneo la ukumbi mkuu; na wengine 150 waliketi roshani – wanaita ubaraza wa ghorofani. Jumla watu 577.

Miongoni mwa waliohudhuria kulikuwa na viongozi wa serikali, watunga sera, wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wawakilishi wa jumuia ya kikanda na kimataifa, watendaji wakuu wa mashirika na kampuni, wasomi wanafunzi, mateka wa “afya mbaya,” na wananchi kwa jumla.

Mkusanyiko huu, kwa saa tatu – kuanzia saa tatu hadi sita “usiku wa manani,” ulielekeza fahamu zake kwa wataalamu waliokuwa wakijadili Afya ya Binadamu. Hii ilikuwa kwa njia ya kuwasilisha hoja na kutoa majibu kwa maswali mbalimbali juu ya maradhi yasiyoambukiza.

Hili lilikuwa kusanyiko la kwanza lililoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) – wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti chini ya mradi wake unaoitwa Jukwaa la Fikra.

Makusanyiko mengine ya aina hii, yakishirikisha wataalamu na wananchi kwa jumla, yanatarajiwa kuandaliwa juu ya hoja mbalimbali zinazogusa maisha na ustawi wa watu na jumuia zao. Kwa mujibu wa MCL, lengo ni kushirikisha wananchi katika kujadili changamoto na matatizo yanayowakabili ili kupata suluhisho.

Kwenye idadi ya waliokuwa ukumbini, ukiongeza idadi ya waliokuwa wakisikiliza redio na kuangalia televisheni nchi nzima, utagundua kuwa ujumbe uliowasilishwa, hakika ulipenya.

Hii ni kwa kuwa, kwanza, mjadala ulikuwa umetangazwa kwa kipindi kirefu; pili, uliwekwa muda ambapo wanaojali tayari walikuwa nyumbani au popote pale karibu na redio au televisheni; na tatu, somo lenyewe lilihusu afya ya kila mmoja – uhai. Ukumbi, maarifa yaliyotolewa na mjadala kwa jumla, vilikuwa “Darasa la Umma.” Hebu nirudie hili: Darasa la Umma, juu ya somo la sayansi, lililoendeshwa na mabingwa wa afya – madaktari, watafiti, walimu wa vyuo vikuu vya tiba na afya, watunga sera na waandaaji mipango ya afya – kwa Kiswahili.

Isipokuwa mwakilishi mmoja au wawili kutoka nchi za nje, wale wote kutoka nchini walitoa michango yao kwa lugha ya Kiswahili; kujibu maswali yote kwa Kiswahili; kutoa maelekezo na ushauri kwa Kiswahili na bila shaka kueleweka kwa Kiswahili.

Hadi Jumatatu wiki hii – siku 17 tangu kufanyika mjadala wa afya kuhusu maradhi yasiyoambukiza, Meza ya Mhariri wa Jamii imepokea maoni ya wasomaji 271 wakieleza furaha yao kupata maarifa juu ya afya zao kutoka wataalamu wanaotumia walichoita “lugha nyepesi.”

“Sasa nimegundua kuwa kutotumia Kiswahili vyuoni ni kutaka mbwembwe za Kiingereza tu. Mfano tumeuona kwa maprofesa hawa wanaotamba na sayansi kwa Kiswahili, ” anaandika Abbas Mulamula wa Isevya, mjini Tabora.

Msomaji mwingine, Justina Msosa anaandika, “Tumefunzwa na maprofesa juu ya afya zetu; tena kwa Kiswahili na tumeelewa jinsi ya kulinda afya zetu.”

Msomaji aliyejitambulisha kuwa mwanafunzi wa udaktari Muhimbili ameandika, “Ningejua kujieleza kwa Kiswahili kama Profesa Andrew Swai, ningekuwa daktari bora huko niendako… anaongea mambo makuu kwa lugha nyepesi sana.”

Profesa Andrew Swai ndiye alichokoza wataalamu-wawasilishaji mada ili wajitupe uwanjani kuelezea, pamoja na mengine, athari za maradhi yasiyoambukiza; tishio lake, ukubwa wake, utafiti juu yake na jinsi ya kukabiliana nayo.

Ni utamu ulioje kumsikiliza Prof esa Swai akieleza kwa Kiswahili tu umuhimu wa chumvi, sukari na mafuta mwilini; na madhara yake pale vinapokuwa vimezidi viwango vinavyohitajika.

Umuhimu wa kula matunda – tena bila kuyakamua juisi; umuhimu wa anachoita “vyakula vya mbogamboga” na ugali unaotokana na mahindi yasiyokobolewa – dona.

Katikati ya wasilisho anaulizwa: Tutumie kiwango gani cha sukari? Anajibu: Kwa afya bora, “vijiko vitano vidogo vya sukari kwa siku” (ukumbi unaangua kicheko).

Afya ya jamii ni eneo mtambuka. Matunda ya darasa la umma yakisambazwa na wote waliohudhuria ukumbini na kwenye televisheni; wizara, ofisi zote za umma, binafsi na vyombo vya habari, maradhi ya yasiyoambukiza yanaweza kupungua kwa kiwango kikubwa au kutokomezwa.