Kibano cha wakuu wa mikoa, wilaya katika ‘kiki za kisiasa’

Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Sophia Mjema akiwa kwenye majukumu yake ya kazi wilayani kwake. Picha ya Maktaba

Baadhi ya wakuu wa wilaya (DC) na wakuu wa mikoa (RC) wamekuwa na kasi katika uwajibikaji kwa wananchi, huku baadhi yao wamelalamikia watendaji wa Serikali au wanasiasa kukwamisha kasi walizonazo katika juhudi za kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

Vivyo hivyo, kumekuwapo na malalamiko dhidi ya baadhi yao kuhusu utendaji, kukuza migogoro na kutoa maamuzi yanayolalia katika marengo yao ya kisiasa.

Hatua hiyo imewafanya baadhi ya wateule hao kwa nyakati tofauti kuwawajibisha hadharani watendaji, watumishi wa umma au wanasiasa wenzao wanapotofautiana nao au wasiporidhika na utendaji wao wa kazi.

Wakati mwingine kupitia wakuu hao hufikia hatua ya kutumia Sheria ya Tawala za Mikoa, inayowapatia mamlaka kuwaweka rumande kwa saa 48 wakidhani ndiyo njia ya kuwarejesha watendaji hao au wanasiasa katika kasi wanayoitaka.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mussa Iyombe wanakemea tabia za wakuu wa wilaya na mikoa wanaotumia vibaya madaraka wakati wa kutekeleza majukumu yao, hususani uamuzi wa kuwaweka watu rumande kwa saa 48.

Katika video iliyosambaa ikimwonyesha Iyombe akizungumza na wateule wa Rais jijini Dodoma, anatoa onyo akieleza kuwa wakuu wa wilaya waliokosa sifa za kutumikia nafasi zao kutokana na maamuzi wanayochukua, ikiwamo kuwaweka rumande watumishi wa umma.

Vilevile, Jafo anakemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kutumia vibaya mamlaka yao, akiwataka pia wakurugenzi wapya kuepuka ugomvi wa kisiasa utakaokuwa chanzo cha kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi.

Desemba mwaka 2016, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Nyanduga aliukosoa utamaduni huo akisema unakiuka wa misingi ya utawala bora kwa madai ya utoaji wa hukumu hadharani bila kufanya uchunguzi na kujiridhisha.

Njia ya kupanda cheo

Dk Abel Kinyondo, mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti Repoa anasema utamaduni huo wa wateule wa Rais kutumia madaraka vibaya, unatokana na sababu tatu ikiwamo kujenga ‘kiki za kisiasa’ ili kuonekana ni viongozi wanaowajibika na kupandishwa cheo.

“Kwa sababu baadhi (ya wakuu wa wilaya) wanaona wapo waliotumia kiki hizo leo hii ni wakuu wa mikoa, mfano ni Alexander Mnyeti na Paul Makonda na wengine. Hawa walikuwa ma-DC ila leo ni wakuu wa mikoa na kwa nyakati tofauti walishiriki kuwaweka ndani watumishi wa umma au viongozi wengine, kwa hiyo DC mwingine ataona ni njia ya kumsaidia apande cheo, nimpongeze waziri Jafo kwa ujasiri huo,” anasema.

Dk Kinyondo anasema hatari iliyokuwa inaonekana ni kwamba hata kwa DC aliyeiva kiuongozi angeweza kubadilika akidhani ndiyo njia nzuri ya kuonekana bora. Anasema CCM na Serikali inayo changamoto ya kuandaa viongozi wanaoweza kuwajibika na siyo kutumia kiki za aina hiyo.

Si hatua sahihi

Akizungumzia suala hilo, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume anasema Sheria ya Tawala za Mikoa inawapa mamlaka wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kuomba Jeshi la Polisi limkamate mtu na kumweka ndani kwa saa 48 endapo tu huyo atakuwa amefanya uhalifu unaotambulika chini ya sheria za nchi.

Anasema Polisi kwa upande wao, pia wanao wajibu wa kumuhoji RC au DC kuhusu sababu za kumkamata na kumweka ndani mtu huyo chini ya Kanuni za Jeshi la Polisi.

Anasema madhumuni ya vifungu vya saba na 15 vya sheria hiyo havilengi kuwapatia mamlaka ya kumweka ndani mtu kwa saa 48 tu, badala yake vifungu hivyo vinatumika pale ambapo RC na DC ataona mtu akitenda uhalifu.

Anafafanua akisema baada ya saa 48 kulala rumande, mtu huyo aliyekamatwa atatakiwa apelekwe mahakamani vinginevyo anatakiwa kuachiwa huru.

Baada ya hapo RC au DC atalazimika kuwasilisha ripoti mbele ya hakimu inayoeleza ni kwa nini alitoa amri ya kukamatwa na kuwekwa ndani kwa mtu huyo.

“Kwa hiyo kutokukubaliana na maelekezo ya RC au DC si uhalifu, kuchelewa kwenda katika mkutano si uhalifu, lazima mtu awe kafanya uhalifu chini ya sheria zetu,” anasema Karume wakati akizungumzia tukio la hivi karibuni la kuwekwa ndani kwa saa 48 mwanachama wa TLS, Wakili Meidard D’Souza kwa amri ya RC Manyara.

Anasema kutokana na mwendelezo wa matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi hao, TLS imeshafungua kesi mahakamani kwa ajili ya kutoa tafsiri ya sheria hiyo ili kukomesha utamaduni wa kukamata watu na kuwaweka ndani saa 48 kinyume cha haki na mamlaka ya wakuu hao wa wilaya na mikoa.

Kuhusu polisi, mwanasheria huyo anasema, “Jeshi la Polisi linatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maelekezo ya Kanuni za Polisi namba 1, inayosema maofisa wa polisi katika ngazi yoyote wanapaswa kuongozwa na sheria katika utekelezaji wa majukumu yao na kwamba mashinikizo ya kisiasa, kidini au vinginevyo, hayapaswi kuruhusiwa katika kufanya maamuzi yoyote.”

Yaleta mabadiliko

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe anasema amefarijika kusikia agizo la Waziri Jafo na tayari ameshaagiza kukutana na wakurugenzi pamoja na wakuu wa wilaya wote wa mkoa huo ili kutoa maelekezo ya utekelezaji.

Dk Kebwe licha ya kutokutoa ufafanuzi wa dhana ya ‘kiki za kisiasa’, anasema utawala wa sheria ni lazima uheshimiwe kwa kutoa nafasi ya kujitetea pale mtumishi anapodaiwa kutenda kosa.

“Waziri ametoa maagizo, wakuu wa mikoa tunatakiwa kusimamia. Maamuzi hayo (kumweka rumande) inamnyima mtu haki ya kujitetea, waziri amekumbusha jambo la muhimu sana.”

Katibu Tawala Wilaya ya Kilombero, Robert Selasela kwa maoni yake kuhusu suala la mbunge na DC kutunishiana misuli, anasema ni jambo linaloepukika. Anasema ni busara inayohitajika licha ya mamlaka aliyonayo DC.

Kuhusu watumishi wa umma kuwekwa ndani, Selasela anasema watumishi wote nchini wana vyombo maalumu vya kushughulikia matatizo yao, hivyo ni sahihi kufuata njia hizo.

“Kwa mfano mtumishi akifanya kosa atapewa chaji (mashtaka) na afisa utumishi, atajibu na akijibu barua yake itapelekwa kwenye kamati maalumu katika halmashauri, baada ya hapo baraza la madiwani linabadilika kuwa baraza la utumishi na kupitia maoni ya ile kamati imesema nini juu ya tuhuma za mtumishi huyu na baada ya hapo anachukuliwa hatua, ukienda kwa mwalimu pia kuna hatua zake,” anasema.

Kuhusu suala la ‘kiki za kisiasa’, Selasela anasema siyo kila tukio linatakiwa kuandikwa kwenye vyombo vya habari. Anasema kukomesha tabia kama hizo ni pamoja na vyombo vya habari kugomea kuripoti matukio ya namna hiyo, mkiendelea kuandika wanaona hiyo ni sehemu ya kupata kiki,” anasema.