Waitara anavyoitofautisha demokrasia ya CCM, Chadema

Aliyekuwa Mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Mwita Waitara (kushoto) akizungumza wakati wa mahojiano na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Kelvin Matandiko alipokuwa akitoa ufafanuzi sasabu ya kuachana na Chadema na kujiunga na CCM, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Picha ya Maktaba

Julai 28, mwaka huu, aliyekuwa mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alitangaza kujivua uanachama na kujiunga na CCM, akieleza sababu kadhaa ikiwamo kuvutiwa na kasi ya uongozi wa Rais John Magufuli. Mwita amekuwa mwanachama wa CCM kati ya 1998 hadi 2008 alipohama chama hicho na kujiunga Chadema. Chadema amedumu nayo hadi mwaka huu alipoamua kurejea CCM.

Sababu nyingine, Mwita alitaja kuwa ni udhaifu na ukandamizaji wa demokrasia ndani ya Chadema uliomfanya kuwa katika wakati mgumu wa kuwatumikia wananchi wa jimbo lake akiwa upinzani.

Licha ya kushambuliwa maneno juu ya uamuzi huo, anasema ameamua kutafuta mahali ambapo atapumua na kufanya kazi kwa uhuru kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kutekeleza ilani ya CCM.

Hoja nyingine ya Waitara ni kwamba, amechukua uamuzi huo kwa kuwa CCM ndiyo yenye Ilani na imekuwa ikichukua sifa katika uzinduzi wa miradi ya jimbo licha ya kutumia juhudi zake wakati akiwa mbunge wa Chadema.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili Agosti 15, 2018, Waitara ambaye ni miongoni mwa wabunge watatu wa Chadema waliojiunga na CCM, anasema kuna maovu yanafanyika ndani ya Chadema ambayo CCM haiwezi kuyafanya.

Anasema viongozi wa CCM hawezi kutengeneza njama za kumuhujumu mbunge katika jimbo lake, lakini hali hiyo imeonekana ndani ya Chadema.

“Mwenyekiti wa wilaya au mkoa wa CCM hawezi kutengeneza makundi ya WhatsApp kwa ajili ya kumkashifu mbunge, lakini hali hiyo imeonekana Chadema.

Kwa hiyo kuna mambo mabaya yalikuwa yamejificha (Chadema), naamini maovu hayo yamechangia kuhamia CCM, ndiyo maana wanahisi wapinzani wananunuliwa, CCM wamefanya uchunguzi, mie nina mifano mingi ya watu wameenda (CCM) kwa sababu hiyo. Mahojiano yalikuwa kama iifuatavyo:

Mwandishi: Unasema ndani ya Chadema kuna ukandamizaji wa demokrasia, unawezaje kujiunga na CCM ambayo inatuhumiwa kuendesha Serikali kwa ukandamizaji wa demokrasia, upinzani wanazuiliwa kufanya maandamano na siasa ilihali yenyewe ikifanya, mbona mazingira yanafanana?

Waitara: Mwanzoni sikuelewa lakini baadaye nimekuja kuelewa kwa nini Rais John Magufuli alisema uchaguzi umeisha, kwa wenzetu walioendelea uchaguzi ukiisha siasa inahamia bungeni, wabunge wanasema kwa niaba ya wananchi na kujenga hoja kinzani. Huku mtaani kila mbunge, kata na mtaa una wawakilishi, kila mwenye dhamana afanye kazi.

Hii nchi ina sheria inayozuia mambo kadha wa kadha yasifanyike, huwezi kuita mikutano tu bila kufuata utaratibu. Na mie sikuunga mkono mambo yale (maandamano).

Mwandishi: Lakini ulionekana kushiriki siyo!

Waitara: Mimi sikushiriki na ndiyo maana sina kesi. Mie nina kesi kwa maeneo fulani, hata kama ungekuwa Chadema, CCM, huna chama, mkristo au mpagani, kama unaenda kinyume utakamatwa tu. Sheria haziangalii kwa hiyo wapinzani wamekuwa wakifanya makosa mengi hadharani na wanasingizia habari ya demokrasia. Demokrasia nini? Watanzania wanataka mtu atukane kutwa nzima au wanataka maendeleo?, uchaguzi umeisha.

Mwandishi: Kwa hiyo inawezekana, ulipokuwa upinzani uliwahi kushiriki kwenye hila za kisiasa dhidi ya CCM?

Waitara: Siasa ni siasa tu, siasa ni mchezo mchafu kama nina kwenda mahali ninawaambia wananchi huyu mgombea wa CCM hafai, na hawezi kuwasaidia na wakati mwingine unasema vitu ambavyo siyo vya kweli, ndiyo siasa yenyewe.

Ni sawa na mchezo wa Simba na Yanga. Haiwezekani Simba wakataka Yanga ishinde, wakigundua kwamba Simba wanazo mbinu za kuwashinda kwenye mechi fulani, watahakikisha ile mbinu inaondolewa ili washinde wao kwa hiyo huu mchezo hautaki hasira, watu warelax wajenge hoja.

Siasa ni mchezo mchafu. Sishangai kuona vyama vya upinzani pamoja na CCM wakipambana kwa mbinu zozote zile ikiwamo hila ili kuhakikisha mmoja anajenga ushawishi kwa wananchi.

Hawa Chadema watapambana kwa maneno ya uongo na ukweli ili CCM ionekane haifai mbele ya Watanzania kwa uchaguzi ujao, au chaguzi ndogo lakini hivyohivyo na CCM watapambana kwa gharama yoyote ile kuhakikisha kwamba wanabakia madarakani, ili waendelee kutawala, kwa hiyo hizi nguvu ni sawa na Simba na Yanga.

Mwandishi: Sasa ni demokrasia unayoizungumzia ndani ya Chadema, ina tofauti gani na ile ya Chadema?

Waitara: Mimi sijui demokrasia unayoizungumzia wewe. Mimi ninachosema ni kwamba, kama uchaguzi kama umetangazwa Ukonga, kila chama kimepewa nafasi ya kupeleka mgombea, ndiyo demokrasia. Hakuna demokrasia ukakae pale (jimboni) ukamtukane mwenzio wee halafu uachwe tu. Haiwezi kuwa nchi, itakuwa uhuni.

Kama demokrasia haipo CCM, si wamenipenda? mwenyekiti ni rais si wangetangaza niwe mbunge? lakini demokrasia inatoa nafasi ya uchaguzi unafanyika.

Chanzo cha ugomvi ndani ya Chadema ni uenyekiti. Ingawa ningeweza kugombea lakini mjadala haukuwa kwangu, Nilionekana miongoni mwa watu wanaotaka mabadiliko ya mwenyekiti na hasa tulimtaka Lissu (Tundu Lissu) agombee na (Freeman) Mbowe alitakiwa kuruhusu wanachama wagombee, hakupaswa kuwa na hofu yoyote.

Mwandishi: Lakini, pia tumeshuhudia changamoto nyingine ya demokrasia ndani ya CCM, mwenyekiti wa CCM aliwahi kutishia kuwafuta wabunge wote wa kusini?

Waitara: Mimi siwezi kuzungumza habari ya rais kwa sababu mie siyo msemaji wa rais, miye nilikuwa bungeni, mwenyekiti anajisemea yeye. Niulize masuala yanayonihusu mimi, siyo msemaji wa mwenyekiti. Mimi siyo mtu wa kusini ila bungeni nilikuwapo, waziri alisema sheria hiyo haipo, ilikuwa ni huruma tu ya Serikali.

Lakini, hata wewe ni mfanyakazi wa Mwananchi, siku ukikiuka utaratibu utafukuzwa siku hiyohiyo, kwa hiyo. Unapokwenda kuomba kazi, usiende na mikono nyuma. CCM kuna katiba na taratibu zao, inabidi ufuate.

Mwandishi: Kwa maoni yako, unazungumziaje mchango wa upinzani hapa nchini?

Waitara: Mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini umesaidia kuimarisha demokrasia na uhuru wa mawazo mbadala, umeibua viongozi wapya ambao wasingeweza kuonekana chini ya mfumo wa chama kimoja.

Vyama vya upinzani vimetoa fursa ya watu kupata upana mkubwa wa kufanya siasa, yaani kwa mfano wakati wa chama kimoja, wangebanana humohumo, kwa hiyo kwa sababu ya ufinyu wa nafasi watu wengi wangekosa fursa.

Pili, kuna mambo ambayo yamezungumzwa kwa uwazi huenda katika mfumo wa chama kimoja yasingeweza kuzungumzwa, yako mengi hata hiyo demokrasia tunayoizungumzia ina maana kuna mambo ambayo watu wasingepata nafasi ya kusema ila sasa wanasema.

Hata Rais John Magufuli alikuwa bungeni kwa miaka 20 akiwa mbunge, akisikiliza hoja za wapinzani, bajeti kivuli na ndiyo maana alipoingia madarakani mambo mengi ambayo yapo (upinzani) ameyaingiza humu (akionyesha Ilani ya CCM 2015/20).

Lakini, kuna hasara pia, vyama vya siasa vimeiingiza nchi katika matumizi makubwa ya fedha. Fedha ambazo anapewa Chadema, CUF na CCM kwenye ruzuku ni kodi za wananchi, kwa hiyo kuwa na vyama vingi, bajeti ya Serikali inaongezeka.

Faida nyingine ni kuongezeka kwa idadi ya wabunge wenye mawazo mbadala, akisema huenda kuna watu wasingekuwa wabunge nchi hii kwa sababu ya ufinyu wa nafasi ila leo wamekuwa wabunge, siyo kila linalofanywa na upinzani ni baya sana, hapana, yako mabaya ya upinzani na yako mazuri.

Mwandishi: Kwa nini usingebakia kuendeleza mapambano ndani ya upinzani?

Waitara: Huwezi kufanya kazi ya kuibua tu, mimi nimekuja kuongeza nguvu (CCM), kwa mambo niliyokuwa naamini yanafanyiwa kazi, niliibua mengi upinzani naamini wako wengine wataibua mengine na yataendelea kufanyiwa kazi.

Kwa hiyo siwezi kusema lazima niwe hapa tu (upinzani) , hapana mimi nilifanya kazi yangu kwa kiwango hicho, nimeona nimekwazika na sijasema upinzani ufe ,ila mimi nataka upinzani safi.