UCHAMBUZI: Uamuzi wa JPM kwenye korosho uende mbali zaidi

Muktasari:

  • Kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2015/16 na 2016/17 mazao yaliyoongoza katika mauzo kwenye soko la nje na kuchangia kwa sehemu kubwa Pato la Taifa ni matano yaliyoingiza Dola za Marekani 793.4 milioni kwa mwaka 2015 na Dola za Marekani 895.5 milioni kwa mwaka 2016.

Ni wazi kuwa mazao yanayolimwa Tanzania na kuingiza fedha nyingi za kigeni kama tumbaku, kahawa, pamba na chai kwa sasa yanaongozwa na korosho. Miaka ya nyuma mazao kama mkonge yamewahi kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2015/16 na 2016/17 mazao yaliyoongoza katika mauzo kwenye soko la nje na kuchangia kwa sehemu kubwa Pato la Taifa ni matano yaliyoingiza Dola za Marekani 793.4 milioni kwa mwaka 2015 na Dola za Marekani 895.5 milioni kwa mwaka 2016.

Mwaka 2017/18 uliwashangaza watu wengi baada ya zao la korosho kutia fora kwenye mapato lilipoingizia shilingi 1.08 trilioni baada ya kuvunwa kutoka kwenye mikoa minne, Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma.

Mapato ya korosho ya mwaka 2017/18 yalizidi mapato ya mazao mengine hata kama yangeliweka matatu kiushindani.

Uamuzi wa Serikali ya JPM

Novemba 12, 2018, Rais John Magufuli aliamua kuwa korosho yote itanunuliwa na serikali na kisha serikali itaweka utaratibu wa kuiuza na kufidia fedha ambazo zitakuwa zimetumika.

Uamuzi huu wa JPM ulikuja baada ya serikali yake kujiridhisha kuwa ikiendelea kusubiri urasimu wa wanunuzi wa ndani na nje korosho zitawaharibikia wakulima majumbani na maghalani. Uamuzi huu wa umeanza kutekelezwa mara moja chini ya uangalizi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Uamuzi huu umeleta mjadala mtaani, wapo wanaosema uamuzi huo una maana ya serikali kuingilia biashara na masoko na kwamba kwa nini serikali haifanyi hivyo kwenye mazao mengine. Kwanza inapaswa kueleweka kwamba serikali zote duniani ndizo msimamizi mkuu wa biashara za kitaifa na kimataifa.

Wafanyabiashara wa kitaifa na kimataifa hufanya biashara zao ndani ya wigo uliojengwa na serikali za dunia na jambo hilo halina mjadala.

Pili, mataifa yote duniani mara zote hayakwepi jukumu la kuingilia biashara ikiwa mataifa hayo yanaona kuna kuyumba kutakaopelekea wafanyabiashara au watu wake kupata hasara. Mathalani, miaka ya hivi karibuni wakati Rais Barack Obama akiongoza Marekani, kulitokea mdororo na anguko kubwa kwenye sekta ya fedha na mabenki ambao ulianzia Marekani. Uchumi wa Marekani ukayumba na mabenki makubwa yakajiandaa kufilisika.

Marekani ilipoona hali ile haraka ikakimbilia kwenye hazina kuu yake na kuchota matrilioni ya fedha na ikayamwaga kwenye mabenki na taasisi kubwa za fedha ambazo zilikuwa zinaelekea kufilisika. Mchakato huu ulifanywa haraka na hakukuwa na mivutano, ilikuwa ndiyo njia ya pekee ya kuokoa mabenki na sekta ya fedha Marekani na kwa hiyo duniani.

Serikali kuwalinda wakulima

Uamuzi huu wa JPM kwa zao la korosho unaungwa mkono kwa sababu, kama ilivyokuwa kwa Marekani, njia ya pekee ya kuokoa zao hilo na kuwaokoa wakulima kwa haraka ilikuwa ni kuwadhamini kwa kununua mazao yao na kisha kuyauza. Kwenye mchakato wa kuuza korosho wanaweza kujitokeza wafanyabiashara wakubwa au makampuni makubwa ya korosho duniani yakaja kununua, hayatanunua kwa wakulima tena maana muda huo korosho itakuwa imebanguliwa na imo mikononi mwa serikali, wafanyabiashara hao watanunua korosho iliyobanguliwa kwa serikali na maisha yataendelea.

Baada ya serikali kumaliza zoezi hili la kununua tani zaidi ya 200,000 na kuzibangua ambapo itakuwa na korosho iliyobanguliwa tani takribani 70,000 na ikiendelea na mikakati ya kuziuza, tunao wajibu na hasa serikali, wa kujielekeza zaidi kwenye intelijensia ya kiuchumi na kimasoko.

Intelijensia ya nchi yetu lazima ifanye kazi usiku na mchana kubaini na kutambua au kubashiri ni wapi duniani ambako mazao fulani yatahitajika sana mwaka unaofuatia ili kuwaandaa wakulima wetu wayazalishe sana na wakati huohuo tukiwasiliana na serikali na wafanyabiashara wa maeneo hayo watuandalie masoko.

Ni wazi kuwa uamuzi wa serikali wa kununua korosho mwaka huu 2018 hautafanyika kila mwaka na pia hautafanyika kwa mazao mengine. Uamuzi huu ni wa kuokoa hali ya mambo. Uamuzi wa muda mrefu unapaswa kuwa ni kuweka mikakati ya muda mrefu ya kuzalisha korosho za kutosha na kujenga viwanda vya kubangua korosho hapa kwetu na ikiwezekana kuzipakia kama bidhaa ya kupeleka kwa mlaji moja kwa moja nje ya nchi.

Wizara za Kilimo, Viwanda

Tunao wajibu wa kuachana na hii kasumba ya kuzalisha mazao halafu tunayasarifisha yakiwa ghafi na yanakwenda kuongezewa thamani nje ya Tanzania. Tunao wajibu wa kuendelea kujenga ajira na asilimia kubwa ya ajira za nchi yetu zinaweza kutengenezwa kwenye eneo linalohusiana na ardhi, yaani kilimo.

Watendaji wa serikali wafanya kazi kufa na kupona ili tuwe na viwanda vya korosho vya uhakika, msimu ujao wakulima walime korosho wakijua inaweza kubanguliwa hapahapa na kuuzwa bei ya juu zaidi ikishaongezwa thamani.

Wizara za Kilimo na ile ya Viwanda na Biashara zisisubiri tena mwakani korosho zinunuliwe na serikali, mwakani tunataka kuona korosho ikiongezewa thamani hapahapa Tanzania.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera, mtafiti, mfasiri, na mwanasheria. Simu +255787536759 [email protected])