Msajili ataka majina, namba za simu za wajumbe wa vikao vyama vya siasa

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imevitaka vyama vya siasa nchini kuwasilisha orodha ya wajumbe wa vikao vyote vya kitaifa ikiambatana na namba zao za simu na mahali wanakoishi.

Wajumbe wanaolengwa katika agizo hilo ni wa mkutano mkuu wa taifa, halmashauri kuu ya taifa, kamati kuu na vikao vingine vya kitaifa ambavyo hakuvitaja katika maelekezo yake.

Maagizo hayo yalitolewa tangu Februari 19, mwaka huu na kuwekewa msisitizo kwa barua ya Oktoba 4, mwaka huu ambayo Mwananchi imeiona, yanavitaka vyama hivyo kuwasilisha orodha yenye jina kamili la mjumbe, cheo chake katika chama na jinsi yake.

Pia, agizo hilo linataka maelezo ya umri wa mjumbe, mkoa anaoishi, wilaya anayoishi, namba ya kadi ya uanachama, namba ya simu, tarehe ya kuwa mjumbe na tarehe ya ujumbe wake kuisha.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na Naibu Msajili, Sisty Nyahoza, wito huo ni kwa mujibu wa kanuni ya 15 (1) ya Kanuni za usajili wa vyama vya siasa na mtu anayeikiuka anaweza kushitakiwa na akipatikana na hatia atafungwa jela.

Chanzo cha habari kutoka moja ya vyama hivyo, kimeeleza hofu yake kuwa lengo la wito huo linaweza kuwa na ajenda ya siri ya kuwabana au kuwafuatilia wajumbe wa vyama hivyo walipo na wakati wowote.

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

“Kama mtu unaweza namba za siku za wajumbe wote kutoka nchi nzima, hii haiwezi kuwa na lengo zuri,” alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa mambo ya nje, itikadi na uenezi wa Chadema, John Mrema alipoulizwa kuhusu barua hiyo, alisema yeye anaona barua ni ya kawaida na chama hicho kiliipata tangu Septemba mwaka jana.

Vivyo hivyo, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmy Dovutwa alipozungumza na Mwananchi kuhusu barua hiyo alisema hajaipata lakini alipoulizwa kuhusu maudhui yaliyomo, alisema mambo yanayotakiwa ni taarifa za kawaida ambazo zimekuwa zikitakiwa tangu miaka ya nyuma.

Nyahoza alisema barua hiyo iliandikwa kwa vyama vya siasa kutokana na baadhi yao kutotekeleza wito wa msajili na vyama vingine kuwasilisha taarifa ambazo zilikuwa hazijitoshelezi.

Nyahoza alisema ofisi hiyo imeomba taarifa kama hizo kutoka kwenye vyama kwa kuwa msajili ameona ni muhimu kuwa nazo kwa faida ya kiutendaji katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ili kama kuna tatizo au changamoto aweze kuzitatua.

“Tulikuwa tunaziomba kwa kusudi maalumu. Tuliona kuliko kuwaandikia mmojammoja kwa vyama 19, tukaona wale waliokosea warekebishe, maana baadhi ya vikao havikuwapo, lakini pia ilikuwa ni fursa kwa ambao walikwa bado hawajatekeleza agizo hilo kutekeleza,” alisema Nyahoza.

Alisema walikokuwa hawajawasilisha taarifa zao waliotoa sababu kuwa bado hawajafanya mkutano mkuu na wengine walikuwa wakijiandaa na chaguzi ndogo mbalimbali, ndiyo maana tuliwakumbusha kwa barua ya Oktoba 4, kwa kuwa utekelezaji wa sheria unazingatia mazingira ya kibinadamu yaliyopo.

“Kanuni za vyama vya siasa zinasema muda wowote msajili anaweza kuhitaji taarifa za chama au vyama hususani pale anapoona mwenendo wa uendeshaji wa vyama unamtaka awe na taarifa hizo. Baada ya kuwakumbusha wote waliwasilisha,” alisema Nyahoza.

Kuhusu vyama visivyoitikiwa wito huo, Nyahoza alisema kanuni zinaelekeza kuwa msajili anaweza kumshtaki kiongozi anayehusika na uwasilishaji wa hizo taarifa na akafungwa.