4-4-2 ilivyozihukumu Croatia, Ufaransa

Muktasari:

  • Ufaransa chini ya kocha Didier Deschamps, ilitumia mfumo huo kuanzia katika mechi za hatua ya makundi hadi fainali. Deschamps alinufaishwa zaidi na mfumo huo ingawa aliutumia kwa makini akitambua udhaifu kwenye safu yake ya ulinzi.

Mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia baina ya Ufaransa na Croatia, ulikuwa na maajabu yake kwa kuzikutanisha timu zinazotumia mfumo sawa 4-4-2.

Ufaransa chini ya kocha Didier Deschamps, ilitumia mfumo huo kuanzia katika mechi za hatua ya makundi hadi fainali. Deschamps alinufaishwa zaidi na mfumo huo ingawa aliutumia kwa makini akitambua udhaifu kwenye safu yake ya ulinzi.

Washambuliaji wake walilazimika kurudi nyuma kusaidia ulinzi kabla ya kufanya mashambulizi machache ya kushitukiza ambayo yaliwapa matokeo mazuri huku Paul Pogba na N’golo Kante wakitumika kupenyeza mipira mirefu mbele. Mfumo huo ulichagizwa na kasi ya kinda Kylian Mbappe na Antoine Griezmann wenye uwezo mkubwa wa kukimbia na mpira langoni mwa adui.

Akifahamu anakutana na timu yenye safu nzuri ya ulinzi na mfumo sawa na wake, Deschamps, aliwaandaa washambuliaji wake kufanya kazi mbili kurudi nyuma kuzuia na kushambilia kwa kushituliza.

Croatia

Zlatko Dalic ni kocha mwenye uwezo wa kuwasoma wapinzani ndio maana aliziondoa Denmark, Russia na England, katika 16 bora, robo na nusu fainali.

Dalic enzi zake alicheza nafasi ya beki hatua iliyomuwezesha kujua namna ya kudhibiti mbinu za wapinzani na namna ya kuwakabili. Aliamini mfumo wa 4-4-2 tangu hatua za awali, akiwa na kikosi imara kwenye ulinzi na kiungo, hakuwa na washambuliaji wenye uwezo wa kufunga mabao, lakini mbinu zake zilificha udhaifu huo.

Kutokana na aina ya wachezaji alionao alibainisha tangu mwanzo wa fainali hizo kuwa alitua Russia akiwa na malengo ya kufika 16 bora.

Ingawa aliyasema hayo mapema hakuna aliyefikiri au kuamini kama angetimiza malengo hayo.

Dalic alifanya maajabu na mbinu zake zikakifikisha kikosi hicho fainali licha ya kufungwa mabao 4-2 na Ufaransa katika mchezo uliokuwa na ushindani mkali.