Adhabu mbadala zitumike kupunguza msongamano jela

Muktasari:

  • Agizo hilo la Serikali lilitolewa baada ya kuwepo kwa msongamano mkubwa wa wafungwa katika magereza mengi nchini.

Serikali imewataka wakuu wa magereza ngazi ya wilaya na mkoa nchini kuwatumia wafungwa kujenga magereza kwenye wilaya ambazo hazina magereza ili kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza ya mkoa.

Agizo hilo la Serikali lilitolewa baada ya kuwepo kwa msongamano mkubwa wa wafungwa katika magereza mengi nchini.

Mathalani mkoani Tabora kunadaiwa kuwepo kwa ongezeko la wafungwa 509 katika magereza yake yote. Kwa mujibu wa Mkuu wa magereza Mkoa wa Tabora, Hamza Rajab, mkoa huo una wafungwa 1,869 badala ya 1,360 ambao ndio uwezo wa magereza yake.

Mbali na mkoa huo, pia inadaiwa magereza mengi nchini yamejaa mahabusu badala ya wafungwa na kwamba ujenzi wa magereza kwenye wilaya kutasaidia wahalifu kupata haki yakufikishwa mahakamani mapema lakini pia itapunguza gharama zinazotumika kusafirisha wahalifu mbali na kosa lilikotendeka.

Takwimu zilizowahi kutamkwa bungeni na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe zilionyesha uwezo wa magereza wa kuhifadhi wafungwa na mahabusi nchini hadi kufikia mwaka 2014 ulikuwa 29,552.

Chikawe pia alisema kuanzishwa kwa kamisheni mpya ya intelejensia ya jinai na kamisheni ya uchunguzi wa jinai ya kisayansi ndani ya Jeshi la Polisi, kumeongeza kasi ya upelelezi wa kesi mahakamani hadi asilimia 12.4 kwa mwaka 2013.

Lakini, Septemba mwaka jana Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamad Yusufu Masauni wakati akijibu swali bungeni kuhusu msongamano wa wafungwa magerezani, alisema idadi ya wafungwa na mahabusi imepungua.

Masauni pia, alizungumzia tatizo la magereza kuwa wilaya 43 nchini hazina magereza, japo kuna juhudi zilizofanywa na Serikali za kujenga magereza katika wilaya 12 kwa kipindi cha mwaka 1996 hadi 2010.

Pamoja na juhudi hizo bado kasi inahitajika kupunguza msongamano wa wafungwa, hii itasaidia kuokoa afya za wafungwa na mahabusu na haki zao kama binadamu.

Pia, tunavyofahamu sheria na sera za kitaifa kuhusu uboreshaji wa magereza kama zilivyoridhiwa na maazimio mbalimbali ya kimataifa, vifungo siyo njia pekee ya kumrekebisha mhalifu.

Kwa mantiki hiyo, tunaamini adhabu mbadala ni bora zaidi kuliko kifungo na Serikali ilikwishaweka adhabu hizo kwa mujibu wa sheria zikiwamo kulipishwa faini, kuachiliwa kwa masharti, kuachiliwa kwa uangalizi, kifungo cha nje na huduma kwa jamii.

Lakini, mbali na wafungwa kuna mahabusi wanaosubiri kesi zao mahakamani, hawa sababu kubwa ya kutokamilika mashauri yao mahakamani ni kuchelewa kwa upelelezi kutoka upande wa mashtaka.

Msongamano magerezani hauumizi tu Serikali, hata wafungwa na mahabusi nao wanaathirika kiafya na kisaikolojia, hawako humo kuteseka na kukomolewa nao ni binadamu wanaostahiki utu na heshima.

Ninaamini lengo zuri la Serikali la kupunguza msongamano magerezani litaongezwa kasi ikiwamo kuongeza idadi ya wanaonufaika na parole na msamaha wa Rais kwa mujibu wa sheria.