Ajira isikufanye kuwa mtumwa

Muktasari:

  • Unapoingia kwenye ajira kwa kutoa rushwa utafanya kazi ukitege-mea uwepo wa mtoa ajira ambaye ulimhonga. Akiondoka maana yake usalama wa ajira yako ni mdogo.Unatakiwa kufahamu kuwa anayeomba rushwa naye anakuwa amewekwa tu, kwa hiyo anaweza kuondolewa kwa kufanya makosa au kuhamishwa sehemu nyingine

Ukosefu wa ajira ni changamoto ya dunia nzima. Kinachotofautisha kati ya nchi moja hadi nyingine ni ukubwa wa tatizo.

Kila binadamu hubanwa na mahitaji ya lazima ya kimaisha ambayo kuyatimiza bila pesa haiwezekani. Pia, kupata fedha bila vyanzo ni vigumu. Chanzo kikuu cha mapato kwa watu wengi ni kuajiriwa, ama serikalini au taasisi binafsi.

Hali hiyo ndiyo husababisha watu wengine wawe tayari kufanya chochote ili wapate ajira. Wakiombwa rushwa ya fedha hutoa, wapo ambao hulazimika kutumia miili yao kama zawadi kwa mtoa ajira.

Wasio na fedha wanaahidi mishahara ya miezi kadhaa kulingana na makubaliano. Unakuta mtu kaanza kazi, badala ya hali yake iwe bora kwa sababu ana kipato cha ukakika, maisha ndiyo yanazidi kuwa magumu. Kumbe anamfanyia kazi mtu.

Wapo wanaogeuzwa watumwa wa mapenzi. Kila mtoa ajira anapohitaji kutimiza matakwa ya mwili wake, anaagiza tu. Ndani ya ofisi moja unakuta wapo watu hata watano wenye kuchangia penzi la mtoa ajira kwa sababu wamepewa kazi kwa mtindo wa aina moja.

Kutoa rushwa ili kupata kazi ni matokeo ya juu ya kutojitambua. Unapaswa kuelewa kuwa unapoajiriwa maana yake umefuzu vigezo vya ajira, yaani umeonekana unaweza kutekeleza kazi ambayo umeomba na kutengeneza matokeo, sasa rushwa ya nini?

Zipo hasara ambazo utaandamana nazo ikiwa utaingia kazini kwa kutoa rushwa. Ukizielewa zitakuongoza kukataa rushwa.

Utumwa wa ajira

Unapoajiriwa kwa kutoa rushwa maana yake hiyo kazi umepewa na siyo kwamba umefuzu kutokana na vigezo vyako vya kwenye wasifu wa kitaaluma na uzoefu pamoja na jinsi ulivyojibu maswali ya wasaili.

Uliyempa rushwa anakuweka kwenye daraja la watu ambao amewapa kazi, kwa hiyo atakushurutisha kikazi kwa namna anavyotaka kwa sababu ya kiburi kuwa bila yeye usingepata kazi.

Unaweza kudhani rushwa uliyompa ni kigezo cha yeye kukuheshimu na kukupa thamani. Hapo unajidanganya, kwani mlipokuwa mnapeana rushwa kuna mahala popote mliandikishiana na kutiliana saini?

Ni kwa sababu hakuna makubaliano ya kimaandishi ndiyo maana anakuwa na kiburi kuwa huwezi kumkamatisha kwa chochote. Zaidi, utaishia kuwaambia watu kuwa bosi fulani ulimpa fedha akuajiri lakini anavyokunyanyasa kazini utadhani uliingia kazini bila kumpa chochote.

Kuhusu rushwa ya kuutumia mwili wako, ikatae kabisa. Kama kawaida, anapokutumia hakuna makubaliano mnayoandikishiana. Baada ya siku mbili akikugeuka hutakuwa na ushahidi wowote.

Maswali muhimu ya kukuongoza ni haya; je, ajira na mwili wako wapi kwa wapi? Unaomba kazi ya uratibu wa zabuni, mtu mmoja kwenye jopo la watoa ajira anaamua kuutumia mwili wako, je, huko mwilini ndiyo atauona ufanisi wako wa kazi uliyoomba?

Anayetaka kuutumia mwili wako akupe kazi huyo hakuheshimu na hathamini utu wako. Unapaswa kujiuliza ameshawatumia wangapi kwa njia hiyo? Matokeo yake unapata ajira kisha mnajikuta 10 mliotumiwa na bosi mwenye tamaa.

Yeyote anayekuomba rushwa akupe kazi maana yake amekudharau. Amekuona huna viwango vya kuajiriwa kwa nafasi ambayo umeomba, kwa hiyo anaamua kukutumia kwa faida yake.

Usalama wa ajira

Unaweza kutoa fedha na hata mwili kisha ukapata ajira. Uliyemhonga fedha au mwili ndiye anayeweza kutoa mapendekezo ya wewe kusitishiwa ajira, na huwezi kupata msaada wowote hata kama utaamua kusema ulichonacho.

Kwanza rushwa ni kiapo cha siri. Huwezi kujitangaza kuwa ulitoa rushwa kama ambavyo mpokeaji hawezi kukiri kuwa alipokea. Rushwa ni dhambi na ni kosa kubwa, kwa hiyo hubaki siri ya mtoaji na mpokeaji.

Unaweza kutoa rushwa na ikapokelewa kisha ukanyimwa ajira. Huwezi kushitaki popote kuwa ulitoa rushwa, maana utakuwa unajipeleka matatizoni mwenyewe.

Unapopata ajira baada ya kutoa rushwa, siku zote utakuwa kwenye presha kila unaposikia taarifa za ukaguzi wa wafanyakazi. Maana utakuwa unahofia ubora wako kama unakidhi viwango vya kiofisi.

Ajira ya uhakika ni ile ambayo umeajiriwa baada ya kuonekana utakuwa msaada kwa taasisi husika. Nawe utajiamini kwa sababu ulitolewa mapendekezo bora baada ya kujibu vizuri maswali ya usaili.

Unapobebwa kuingia kazini huwezi kujiamini. Hivyo, utakuwa na wasiwasi kila masuala ya uhakiki wa wafanyakazi yanapofanyika. Ukiambiwa tu uwasilishe vyeti halisi vya chuo utaanza kuhaha hata kama vyote unavyo.

Utegemezi wa mtoa ajira

Unapoingia kwenye ajira kwa kutoa rushwa utafanya kazi ukitegemea uwepo wa mtoa ajira ambaye ulimhonga. Akiondoka maana yake usalama wa ajira yako ni mdogo.

Unatakiwa kufahamu kuwa anayeomba rushwa naye anakuwa amewekwa tu, kwa hiyo anaweza kuondolewa kwa kufanya makosa au kuhamishwa sehemu nyingine.

Mwenye taasisi yake hawezi kukubali kuhongwa ili atoe ajira, maana anataka wafanyakazi wazuri ambao watamfanya apate mafanikio. Anayekubali kuhongwa maana yake anataka mtu yeyote ilimradi ampe anachotaka.

Kwa maana hiyo ukiona mtu anaomba rushwa ujue huyo siye mwenyewe. Anatumia tu vibaya nafasi ambayo amepewa. Kwa maana hiyo tambua kuwa kama alivyowekwa, basi anaweza kuondolewa na kuwekwa mwingine.

Dunia haina siri

Katika taasisi yoyote mchakato wa ajira hautekelezwi na mtu mmoja. Ikiwa aliye juu zaidi alitoa maagizo ya wewe kupokelewa kazini kinyume na utaratibu kwa sababu ya hongo uliyompa, hiyo haiwezi kuwa siri tena.

Maneno yatazungumzwa na yatasambaa. Ulishaambiwa kuwa hakuna siri ya watu wawili. Usambaaji wa maneno hayo ni harabu ya ajira yako pamoja na mtoa ajira uliyemhonga.

Watu watazungumza na mtasema hayo ni majungu, hata hivyo yatakua na kuushtua uongozi wa juu ambao ukiamua kuchukua hatua wewe hutobaki salama.