Ambacho ungefanya baada ya mazoezi

Muktasari:

Dondoo hizi zimekuwa zikishauriwa na wataalam wa afya wa Tiba za wanamichezo kutumika ili kuwasaidia wanamichezo kupata ahueni baada ya kazi ngumu ya mazoezi au mechi.

Kwa wanamichezo walio wengi hukumbana na majeraha ya mwili wakati wanashiriki michezo au mazoezi. Zipo dondoo muhimu ambazo huwa ni sehemu ya matibabu rahisi ya majeraha madogo madogo.

Dondoo hizi zimekuwa zikishauriwa na wataalam wa afya wa Tiba za wanamichezo kutumika ili kuwasaidia wanamichezo kupata ahueni baada ya kazi ngumu ya mazoezi au mechi.

Dondoo hizi ndizo zinazowasaidia wanamichezo wengi wakimataifa au wakulipwa uponaji wa haraka wa vijeraha vidogo dogo vilivyojitokeza wakati wa kushiriki mechi au mazoezi.

Vile vile huwasaidia kuupunguza maumivu/uchovu wa mwili na kupunguza hatari ya kupata majeraha.

Dondoo zifuatazo ndizo ambazo zimeonekana kuwa na tija katika kurudisha utimamu wa mwili wa mwanamichezo baada ya kumaliza mazoezi au mechi ngumu.

Ulaji wa vyakula vidogo vidogo ikiwamo matunda nusu saa tangu kumaliza mazoezi ni jambo muhimu kwani vitu hivyo vinaupa mwili nguvu na maji kwa haraka sana.

Ulaji wa mlo mchanganyiko wanga na protini. Vyakula vya wanga vinakurudishia nguvu iliyotumika kwa haraka wakati protini inasaidia kujenga mwili ikiwamo misuli.

Vyakula hivi vinakusaidia kupunguza hatari ya kupata majeraha na kama umepata majeraha inasaidia kuongeza kasi ya kupona.

Uogaji wa maji ya uvuguvugu na ya baridi ni moja ya tiba rahisi za kuupa mwili nafuu baada ya mazoezi magumu, inatakiwa baada ya kuumwagia mwili maji ya moto una malizia kuoga na maji baridi.

Kwa wenzetu waliopiga hatua wana mabafu maalum yenye kutoa maji moto au mvuke na maji ya baridi. Maji ya moto huifanya mishipa ya damu kutanika na kupeleka damu zaidi kutoka katika viungo vya ndani kwenda katika ngozi.

Wakati maji ya baridi yanaifanya mishipa ya damu juu ya ngozi kusinyaa kidogo hivyo damu nyingi hutoka katika ngozi na kuelekea kwa wingi katika ogani za ndani ya mwili hivyo kuvifanya viungo hivi kuwa salama na kupata jotojoto hivyo kuongeza ufanisi wa viungo hivyo.

Kunywa maji mengi ni muhimu sana ili kurudishia maji na chumvi chumvi zilizopotea kwa njia ya jasho. Hivi sasa katokana na kupiga hatua kimaendeleo kuna vinywaji maalum kwa ajili ya wanamichezo ambavyo ndani yake huwa na maji, chumvi(sodiamu) na wanga.

Kupata mapumziko baada ya mazoezi/mechi ngumu inatakiwa kwa wachezaji kupumzisha mwili kwani kwa misuli.

Mchezaji anaweza kufanya mazoezi mepesi ikiwamo kunyoosha misuli ya mwili ili kuondoa mkazo wa misuli na kuifanya misuli iwe tepetepe.

Usingaji wa mwili (massage) ni kitu kizuri kwani ni tiba rahisi ya kuondokana na uchovu na maumivu ya misuli, vile vile humfanya mwanamichezo kuwa na utulivu wa kimwili na kiakili.