MIAKA MITATU YA JPM: Amethubutu kwenye uchumi, demokrasia bado kuna changamoto

Muktasari:

  • Tathmini ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano kuhusu siasa na uchumi, limebainisha Serikali ya Dk John Magufuli imeweza kuthubutu kwenye uchumi kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, lakini imeonyesha changamoto kwenye siasa hasa suala la demokrasia.

“Rais ameonyesha uthubutu wa kutekeleza miradi mikubwa na kiuchumi tupo katika mkondo sahihi.” Ni kauli ya Dk Richard Mbunda ambaye ni Mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mbali na uthubutu katika utekelezaji wa miradi ya kiuchumi Dk Mbunda pia anasema; “Kwenye siasa kidogo ningekuwa na mawazo tofauti nilitegemea Rais mwenyewe awe anajifanyia tathmini kama mambo yapi yanasaidia utawala wake.”

Dk Mbunda anasema hayo kutokana na tathmini aliyofanya kwenye kongamano la siasa la uchumi lililofanyika wiki hii UDSM, lililokuwa na lengo la kuangalia miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano. Tunatoka wapi na tunakwenda wapi.

“Tunapozungumzia utawala unaoacha alama hata baada ya miaka 50 baada ya kuondoka, kwenye siasa sana sana haki za binadamu ikiwamo watu kukamatwa kamatwa, kuzuia mikutano ya kisiasa, nilikuwa nadhani angekuja na majibu ya masuala hayo baada ya kujifanyia tathmini yeye mwenyewe, ” anasema.

Anasema kuwa Rais ameonyesha ujasiri katika kutekeleza miradi mikubwa kama reli na umeme na katika kongamano hilo alieleza sababu za kutekeleza mradi wa kufua umeme unaotokana na nguvu ya maji Stiegler’s gorge, licha ya wengine kuuona una utata.

Anafafanua kuwa kwenye masuala ya uadilifu, kupambana na rushwa, kuwawajibisha wasiotimiza majukumu yao, amethubutu na amefanikiwa kurudisha ari ya viongozi na wateule wake kuchapa kazi.

Anasema badala yake pamoja na kelele zinazopigwa watu wakidai haki ya kusikilizwa, kupata uhuru wa kujieleza lakini alivyomsikia akizungumza ni kama anajiona yupo sahihi.

“Kauli zake za jana (Alhamisi) zinanipa shaka kama anajitathmini,” anasema Dk Mbunda.

Anaeleza kuwa kama kiongozi wa nchi ni muhimu kujifanyia tathmini ili uone kama unatimiza matakwa ya jamii, unaiongoza na yenyewe inapaswa iwe inakupa mrejesho na usonge mbele kwa sababu lengo kubwa la kutaka maendeleo lifanyike.

“Cha kushangaza hayo mambo yanayopingwa na kupigiwa kelele yasiwepo hayakinzani na maendeleo anayoyahubiri badala yake yanasisimua chachu ya kupatikana kwake,” anasema Dk Mbunda.

Akichangia mada kwenye kongamano hilo Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Charles Kitima anasema kuwa mambo yanayoendelea kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanakatisha tamaa na kuvunja ‘legitimacy’ (uhalali) ya utawala.

Alisema amesimama kwenye kongamano hilo kuwasemea wasiokuwa na sauti kutokana na kuwapo kwa tatizo kwenye tume ya uchaguzi ambapo mambo yanayoendelea yanavunja ‘legitimacy’ ya utawala.

Utawala wa sheria

Alifafanua kuwa utawala wa sheria una tatizo kwa watendaji wa chini wakiwamo baadhi ya wakuu wa wilaya baadhi na wakuu wa mikoa, ambapo wamekuwa wakiwadhalilisha watendaji wa Serikali hadharani tena wengine ni wanawake.

“Sidhani kama Rais aliwatuma kufanya hayo, ”anahoji na kujiuliza.

Akijadili kilichosemwa na Profesa Humphrey Moshi aliyekuwa akizungumzia mada ya hali ya uchumi na maendeleo ya viwanda, Kitima alisema kuwa licha ya uchumi kukua hakuna mabadiliko ya wananchi masikini.

Moshi anasema uchumi umekuwa lakini wananchi ni masikini, hawaonekani kupanda kutoka kwenye umasikini na kuwa na hali ya kati ya kiuchumi.

Kitima pia alishauri sekta binafsi ijengwe mpya itakayosaidia Serikali kumiliki mitaji, kutoka ile iliyokuwa imeshikiliwa na waliovishika vyama vya siasa.

Kwa upande wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mstaafu, Profesa Rwekaza Mukandala ambaye ni mwanasayansi wa siasa aliyebobea alisema Siasa ni mchezo mgumu wa mahesabu ya kimkakati.

Alisema kila mwanasiasa hususani Rais ana malengo makuu matatu, yakiwamo kupata madaraka na kudumu ofisini kwa kipindi mwafaka, kutawala na kuongoza kwa ufanisi na mafanikio na kujenga chama cha siasa makini na tiifu kwake.

Alisema pamoja na hayo lazima kuangalia madaraka yanatumiwa vipi kwa manufaa ya nani? Na kwa kufuata sheria na katiba au la.

Profesa Mukandala akizungumzia utendaji wa Rais Magufuli alisema wapo watu wanaoshabikia matokeo ikiwa pamoja na kununua ndege na kujenga barabara.

“Kuna vitu vingine haviwezi kuwa ‘quantified’ (kuonekana). Kwa mfano watu wanavyojisikia, watu wanafurahi? watu wameridhika? Watu wana morali? watu wanapendana?” Anahoji.

Anasema: “Unaweza ukawa baba nyumbani unaleta chakula, nyama na samaki kila siku, lakini mama, watoto hawana raha, sasa huwezi kusema wewe una mafanikio makubwa katika hilo.”

Katika tathmini yake Profesa Mukandala anahoji maswali matano ikiwamo uelewa wa ulimwengu na changamoto zake, pamoja na kuainisha mfumo huu wa kimataifa na uchambuzi na uelewa wa hali ya nchi na namna ya kuzitatua.

“Rais kama kiongozi mkuu wa siasa, ameweza kuongoza kuwa mstari wa mbele kwa mawazo na vitendo? Ameweza kuhamasisha wananchi wamfuate? Je, ameweza kubuni lugha mahsusi na mwafaka inayochangamsha na kujenga upendo, utashi na utiifu wake?” alihoji na kuendelea;

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

“Kuhusu chama, je ameweza kuimarisha, kujenga kuongoza chama ili kiwe kitiifu kwake na kiunge mkono juhudi zake? Kuhusu Dola: Je, Serikali na taasisi zake zimeimarishwa? Mifumo na taasisi zake zimeimarishwa, utawala wa sheria unazingatiwa? Haki za kijinsia, haki za binadamu, walemavu, haki ya kukusanyika na uhuru wa kujieleza unalindwa?

Akifafanua kuhusu tathmini ya maendeleo yaliyopatika katika awamu ya tano, Profesa Mukandala alitaja kundi jingine la wanaosema mafanikio ya utendaji lazima uchukue nchi kwa ujumla wake ikiwa pamoja na amani.

“Je, kuna ulinzi, je unajinafasi kiasi gani kikanda na kimataifa, je kuna heshima, je inalinda vizuri rasilimali zake?”

Alitaja pia kigezo kinachotumika kupima matokeo yanayochukua muda mrefu kujulikana, akisema kinachopaswa kuangaliwa ni mchakato.

“Kwa mfano Mwalimu Nyerere tunampenda sana, lakini siyo kwamba aliondoa umasikini au alituletea maji, lakini nia na dhamira ilikuwepo,” alisema.

Alitoa pia mfano vita dhidi ya rushwa akisema inayoangaliwa ni dhamira maana rushwa haiishi kabisa.

Rais Magufuli na Katiba mpya

Akizungumza katika kongamano hilo mara baada ya watoa mada kumaliza Rais Magufuli alifunga rasmi mjadala wa mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.

Alisema anafahamu kiu ya Watanzania ni kupatikana kwa Katiba mpya, lakini mlolongo uliopo katika kuifikia hatua hiyo ndio unaomfanya aache mawazo hayo na kujikita zaidi kwenye shughuli za kuleta maendeleo.

Rais Magufuli alieleza kuwa anashindwa kuelewa kuipata Katiba mpya mchakato uanzie kwenye hii rasimu ya Katiba ambayo imepita miaka minne tangu itayarishwe au mchakato uanze upya.

“Badala ya kubishania haya acheni tufanye kazi, ”alisema na kuongeza: “Nafahamu kiu ya Watanzania kuwa na Katiba mpya ila sasa tunafanyaje tuende na Katiba pendekezwa au rasimu ya (Jaji Joseph) Warioba hapo ndipo ninapoona tuache kupoteza muda kulumbania hilo, tuchape kazi,” anasema.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alitumia kongamano hilo kueleza mafanikio aliyoyafanya Rais John Magufuli, akisema ametekeleza ahadi zake kwa kipindi cha miaka mitatu.

Profesa Kabudi anasema malengo makuu ya Serikali ya awamu ya tano ni pamoja na kuendelea kukuza uchumi na kupunguza umasikini, kujenga mazingira wezeshi na uwekezaji, kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii, kujenga nidhamu ya utendaji kazi na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

“Uchimbaji wa madini umeongezeka mpaka asilimia 14.5, mawasiliano asilimia 13.8 na kasi ya ukuaji wa kilimo inayoajiri asilimia 60.3 na asilimia 30 ya pato la taifa,” anasema Profesa Kabudi.

Anataja pia kuongezeka kwa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ambapo alisema mapato ya ndani ya kodi yameongezeka kutoka Sh12,334 bilioni hadi Sh15,191 bilioni, huku makusanyo ya kodi kwa jumla yakifikia wastani Sh1.2 trilioni kwa mwezi mwaka 2018 ikilinganishwa na Sh800 bilioni mwaka 2015.

Kuhusu mradi wa kufua umeme unaotokana na nguvu ya umeme Stiegler’s gorge, Profesa Kabudi alisisitiza kuwa utafanyika licha ya kukosolewa na wadau wa mazingira na utalii.

“Niseme bila tashwishi utatekelezwa, ije mvua lije jua, utatekelezwa. Wapende wasipende utatekelezwa, watake wasitake utatekelezwa. Kelele zitakuwa nyingi lakini utatekelezwa,” anasema.

Anaeleza kuwa wakati wa Mwalimu Nyerere mradi huo ulishindikana ka ajili ya ukosefu wa fedha na kwamba sasa zimepatikana zinakuja hoja nyingine, lakini utafanyika. Alisema reli ya zamani haitang’olewa itabaki kama ilivyo.

Alifafanua kuwa licha ya kubezwa na baadhi ya watu lakini zimenunuliwa ndege mbili aina ya Airbus A 220300 zinatarajia kuingia Novemba, huku ile Dreamliner ya pili iliyotarajiwa kufika mwaka 2020 inaweza kufika mapema zaidi.

Alitaja pia bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga akisema, Ujenzi na madaraja makubwa Mfugale Flyover na ujenzi wa interchange ya Ubungo.

Serikali imerithi changamoto

Akichangia mada katika kongamano hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo alisema Serikali ya awamu ya tano imerithi changamoto za kibiashara kwa uongozi wa siasa, rushwa, ufisadi na maisha ya ujanja ujanja kutoka Serikali ya awamu ya nne.

“Tunafahamu katika kipindi hiki changamoto iliyotokea ni ‘kubiasharishwa’ (kufanywa biashara) kwa uongozi wa siasa, rushwa na ufisadi na maisha ya ujanja ujanja yaliyokuwa sehemu ya utamaduni wa Watanzania. Kulikuwa na kulegalega kwa mazingira ya uwajibikaji. Katika ubora tuliyumba,” anasema Profesa Kitila.

Alitaja pia changamoto ya kiuchumi akisema ukuaji wa uchumi uliokuwepo haukuweza kuondoa umasikini.

Hata hivyo, akitaja mafanikio, Profesa Kitila alisema Rais mstaafu Jakaya Kikwete atakumbukwa kwa kulinda yale mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya tatu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Akielezea mafanikio ya awamu ya tano, Profesa Kitila alitaja mapambano ya rushwa ambapo alitoa mfano wa kashfa ya mradi wa umeme wa IPTL, akisema ilidumu kwa miaka 25, lakini Rais Magufuli ameimaliza ndani ya mwaka mmoja.

“Katika kujenga uwajibikaji katika utumishi wa umma, hili nalo halina shaka. Kubwa ni kupambana na rushwa, soma suala la IPTL. Limekuwepo tangu wakati wa Mwinyi mwaka 1985. Lakini mheshimiwa Rais ameshughulikia ndani ya mwaka mmoja, kashfa imejifia na watu wamekwenda mahakamani. 25 years lakini imekwisha,” anasema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), Profesa Humphrey Moshi amesema kwa miaka 15 uchumi wa Tanzania unakua, lakini hautoshi kuondoa umasikini.

Profesa Moshi ambaye ni mhadhiri wa muda mrefu wa chuo hicho amesema hata hivyo uchumi wa Tanzania unaokuwa kwa asilimia sita hadi saba si mbaya.

“Pamoja na kukua huko bado haukuwa shirikishi kwa sababu nne, kwanza kilimo kilikuwa chini ya ukuaji wa jumla wa ukuaji wa jumla wa Taifa, pili zile sekta za madini zilikuwa kwa asilimia 12 hadi 17 hazikuweza kupunguza kasi ya umasikini na ukosefu wa ajira,” anasema Profesa Moshi.

Ametaja sababu ya tatu kuwa ni kudumaa kwa sekta ya viwanda iliyokuwa ikikuwa kwa asilimia nane hadi tisa.

“Hayo yote yanaonyesha kuwa bado mfumo wetu wa uchumi haujabadilika. Bado hakujakuwa na ‘structural transformation’ (mfumo mbadala),” alisema.

Anasema mfumo mbadala ni ule unaohamisha rasilimali kwenye sekta kubwa kama kilimo kwenda kwenye viwanda.

“Ni ule unaohamisha nguvukazi kutoka kwenye kilimo kwenda kwenye viwanda, sekta ya kilimo inayochukua nguvu kazi ya asilimia 70 ishuke hadi 20 lakini iwe na tija kubwa inayopeleka rasilimali kwenye viwanda,” anasema.