Anatropia: Mtatiro ameacha njia nyeupe Segerea

“Sasa njia nyeupe Segerea” ni kauli ya Anatropia Theonest, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema). Huyu alipata nafasi hiyo baada ya mwaka 2015 kuukosa ubunge katika jimbo hilo ulioangukia CCM baada ya mvutano ndani ya Ukawa baina yake na Julius Mtatiro wakati huo akiwa CUF.

Anatropia na Mtatiro walijikuta katika msuguano wa kuwania kuteuliwa kugombea nafasi. Mtatiro alipendekezwa na Ukawa katika mgawanyo wa viti, lakini mwanamke huyo tayari alikuwa ameteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alichelewa kuondoa jina lake hadi likaingizwa kwenye karatasi za uchaguzi.

Hata hivyo, Mtatiro aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya CUF hivi karibuni alitangaza kujiunga CCM. Pengine hatua hiyo inaweza kuleta afueni kwa Anatropia kutokana na hasimu wake kujiondoa ndani ya Ukawa.

Katika mahojiano na Mwananchi mbunge huyo anasema, “Binafsi ninatamani na nitagombea ubunge kupitia kipenga kikipigwa. Nitaomba chama changu kinipitishe kikiniona ninafaa.”

Anasema ana ari lakini zaidi ana uwezo wa kuwapigania wananchi wa jimbo la Segerea. Pamoja na hayo, anasema pia hataacha kuweka jina lake katika kinyang’anyiro cha viti maalumu.

“Uzuri wa mchakato wetu (Chadema) haukuzuii kugombea jimbo na viti maalumu. Unagombea ukipata sawa, lakini usipofanikiwa, kwa vile mchango na uwezo wako unaonekana, unaweza kuwapigania wananchi kupitia jukwaa la pili,” anasema.

Akizungumzia kwa nini hakumwachia Mtatiro na iwapo hiyo ndiyo sababu ya Ukawa kushindwa Segerea, anasema; “Mtatiro hajawahi kuwa na mizizi Segerea. 2010 aligombea Ubungo kwa hiyo aliendelea kuwekeza zaidi huko. Segerea alikuwa ni mpita njia tu ,akaambiwa kuna dodo akaamua kubadili upepo.

“Alivyokuja athari yake haikuwa kubwa na pengine hata ilipotokea bahati mbaya NEC iliporejesha jina langu haikuwa raHisi kwake kumshinda Bona, ila angekuwa na nguvu angeweza, pamoja ya mimi kuwapo.”

Anasema endapo atagombea ushindi kwake ni mweupe kwa kuwa mbunge wa sasa ameshindwa kuwawakilisha vyema wana Segerea.

“Kuna mambo mengi hayajatekelezwa tuna vimiradi tu kama barabara za ng’ombe. Wananchi wengi ni wa maskini wa kipato cha chini, changamoto ya barabara za mtaani, hakuna makaravati, hali inayosababisha mafuriko mara kwa mara. Kama haitoshi hakuna mifereji, kazi kubwa haijafanyika. Inshallah nitaendelea kuwapigania ili changamoto zipatiwe ufumbuzi.”

Anasema chama chake kimejipambanua katika sera zinazotekelezeka na kuwashirikisha wananchi kwa kupokea maoni.

“Chadema ina timu bora na ukienda hata bungeni utendaji kazi wa wabunge wetu wachache huwezi kuilinganisha na CCM, ukipitia sera zetu ya mambo ya nje, kiuchumi maji na kilimo zinaeleweka na tutaendelea kuziboresha hadi 2020 watu wanaelewa tunaenda kuwafanyia nini.”

Wanaohama vyama

Huku akisema hajawahi kushawishiwa kuhamia chama chochote, Anatropia anasema baadhi ya wabunge na madiwani wanahama kwa sababu CCM imeweka mkakati wa kuyarudisha majimbo yanayoongozwa na wapinzani kupitia watu dhaifu.

“Wamekuwa wanasukuma watu na kuwarudisha CCM na siyo kwamba wanawahitaji hawa, wanachotaka ni jimbo tu.”

“Wanatumia nguvu, vyombo vya dola na ghiliba kwa ajili ya kuchukua majimbo, japo wapo pia waliohama udiwani viti maalumu, sasa sijajua wanaahidiwa nini? Wapo waliohama na kupewa utendaji wa kata au cheo chochote ambacho kinaonyesha kwamba hawaendi bure.”

Mbunge huyo anaamini kuwa kuhama kwa hoja ya kuunga mkono juhudi za Rais ni dhaifu.

Anatoa mfano wa John Shibuda ambaye alikuwa Chadema lakini akijinadi kuunga mkono serikali akiwa upinzani.

“Wanaweza kuunga mkono kama wanataka kwa kusifia sera, mbona Sakaya anaunga mkono na hajahama CUF? Kinachoonekana wana madeni yao, wana msongo wa mawazo na hawajielewi,” anasema.

Mwanasiasa huyo anashauri Rais John Magufuli kuruhusu siasa za majukwaani ili kupambane na CCM kwa hoja kwa kila mmoja kuuza sera zake na kuwaachia wananchi wachague kati ya pumba na mchele.

“Sasa wanapeleka muswada kuzuia siasa za majukwaani mpaka kipindi cha uchaguzi. Wanakimbia vivuli vyao lakini wajue mwisho wao upo,” alisema.

Mbunge huyo anasema hata ndani ya CCM kuna upinzani ambao hauonekani kama unaoonekana kufanywa na wapinzani.

Anasema kinachotakiwa ni uchaguzi huru, la sivyo kwa hali ilivyo ikitokea uchaguzi sasa upinzani watashindwa vibaya kwa kuwa hali ni mbaya.

Akizungumzia tathimini ya miaka mitatu ya Rais Magufuli anasema amefanikiwa kuleta maendeleo ya vitu na kushindwa kuwaletea watu maendeleo; “Mfano rahisi mwaka mmoja tu deni la Taifa limeongezeka kwa kiwango kikubwa.”

“Imekuwa ni kukopakopa, fedha zenyewe hazionekani zinatumikaje; mimi ni mjumbe wa PAC, wanahitaji kujitathimini yeye na wasaidizi wake.

Usiyoyajua kuhusu Annatronoa

Ni mke na mama wa watoto watatu, msomi wa kiwango cha shahada ya pili na mjasiriamali.

Ni shabiki wa Simba lakini kwa soka la nje anaipenda Arsenal na Real Madrid.

Changamoto kubwa ni kugawa muda wake wa siasa na familia. Kwa sasa ana mtoto mchanga jambo ambalo anakiri si jepesi.