Sunday, June 10, 2018

Anavyotamani vazi lake la ungo liwe la Taifa

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi nabdallah@mwananchi.co.tz

Kati ya fani zinazokuja juu kwa sasa hapa nchini, ya ubunifu mavazi huwezi kuacha kuitaja.

Fani hii imeanza kukua kutokana na wabunifu kuwatumia wasanii maarufu kuonyesha kazi zao kwa kuwavalisha.

Mmoja wa watu hao ni mbunifu wa mavazi ya asili, Jocktan Makeke aliyekuja na vazi linalotokana na ungo alilolipa jina la’ Lupahero’ linalomaanisha shujaa.

Makeke anasema kwamba aliingia katika fani hiyo miaka mitano iliyopita kubuni mavazi japokuwa watu walikuwa wagumu kumuelewa na wameanza kumuelewa sasa bada ya kuja na vazi la ungo mwaka huu.

Mbunifu huyo mwenye shahada ya sanaa na ubunifu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, anasema kwamba sababu ya yeye kuingia katika sanaa hiyo ni kutokana na baba yake kuwa fundi wa kuchomelea vyuma ambapo alikuwa akishinda naye muda mrefu kufanya kazi hiyo.

Yeye ameamua kubadilisha ufundi huo na kuuweka katika mavazi huku mojawapo likiwemo hilo la ungo.

Mavazi hayo tayari ameshawavalisha wasanii mbalimbali akiwemo Mrisho Mpoto wakati wa tuzo za filamu zilizofanyika mapema mwaka huu pale Mlimani City.

Mwingine aliyemvalisha vazi hilo ni rapa Claudia Lubao ’Chemical’ kwenye nyimbo ya ‘Urithi Wetu’, na pia Ivonny Cherry ‘Monalisa’ ambaye amekuwa akirushia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ubunifu huo.

Anasema kwamba baada ya kuanzisha vazi hilo la ungo mwaka huu, amepata ‘madili’ mbalimbali na sasa anatarajia kuzunguka katika baadhi ya nchi kulitangaza.

“Wito wangu kwa Watanzania ni vyema wakajivunia mavazi yanayotokana na malighafi zinazowazunguka ambapo na kwa upande wangu natamani vazi hili la ungo siku moja liwe vazi la Taifa kwa kuwa linajitofautisha na mavazi mengine.

“Pia niwaondoe wasiwasi vazi hilo sio zito kama watu wanavyoliona kwa macho na wala haliumizi kwa kuwa limechanganywa na kitambaa katika maeneo ambayo yanashika ngozi,” anasema Makeke ambaye pia ni Mkurugenzi wa Makeke International.

Anaongeza kuwa vazi hilo wakati mwingine linatumika kama ngao ya kujikinga na adui, kwani kuna nyungo tofauti tofauti ngumu na pamoja na laini.

Wito wake kwa vijana amewataka wasibweteke na kufanya kazi kwani kuna fursa kibao zilizowazunguka ambazo wakizitumia vema zinaweza kuwatoa walipo.

Pia kwa upande wa viongozi amewashauri kuachana na mavazi ya kimagharibi, na kuanza kutumia mavazi ya wabunifu wa hapa nchini kwa kuwa wao wana nafasi kubwa ya kutangaza utamaduni wetu.

Mbali na vazi la ungo, Makeke amekuwa akitengeneza nguo zake kutokana na malighafi za ngozi, mifupa, miti, vifuu, makopo ya maji, vizibo, mifuko ya plastiki yote kwa pamoja akiyaita Otosim na kumtangaza vyema kwenye fani ya ubunifu wa mavazi.

Ameshawahi kupata tuzo mbalimbali ikiwemo ile ya Day to Day African Designer kwenye maonyesho ya Mpingo Fashion yaliyofanyika mwaka jana.

-->