Baba wa Diamond atoa hisia kali

Muktasari:

  • ‘Natamani siku moja nikutanishwe na Diamond na mama yake ili kila mmoja atoe alilonalo moyoni’

Ilinichukua muda kumshawishi na baadaye kufanya mahojiano na Abdul Juma Isack ambaye ni baba wa msanii wa maarufu wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz.

Ungeweza kukata tamaa ya kuendelea kumshawishi kwa sababu ana hoja nyingi na pengine nzito.

“Sioni mabadiliko kwangu,” anasema baba huyo mwenye umri wa miaka 52 wakati akieleza sababu za kukataa kufanya mahojiano.

“Tangu nianze kuhojiwa, nilikuwa nikiamini kuwa ningeweza kubadili msimamo wa mwanangu anayetajwa kuwa msanii tajiri namba moja Tanzania.

“Badala yake naonekana kama nalilia kusaidiwa na mtoto wangu. Pamoja na kuwa na mtoto maarufu ndani na nje ya nchi, maisha yangu ndio kama hivi unavyoyaona. Naishi Magomeni Kagera na nyumba yangu ya kawaida tu, ambayo naamini hata siku Diamond akikwama kimaisha atakuja kuishi kwa kuwa hapa ni kwao, japokuwa simuombei hilo.”

Abdul anasema kwa muda mrefu Diamond amekuwa hafanyi mawasiliano naye na hajui sababu .

“Najiuliza ni nini kikubwa namna hiyo nilichomkosea?” anahoji baba huyo.

“Ninatamani siku moja nikutanishwe katika mahojiano na Diamond na mama yake ili kila mmoja atoe alilonalo moyoni.

“Huyu mtoto kanipa majina mengi kutokana na yanayoongelewa mtaani kwamba nilimtelekeza, wakati hakuna ukweli wowote. Mimi niliachana na mama yake wakati akiwa kidato cha kwanza.

Kwa umri hu alikuwa anajielewa na anajua sababu za kuachana kwetu. Kama kuna jingine wanalolijua wao kwamba nimewakosea, basi tuhojiwe hata mbele za watu ili lifahamike na kuyamaliza kuliko hiki wanachofanya kwangu.

“Kasababisha kila kona ninayopita nanyooshewa vidole kuwa niliwatosa. Ifike mahali haya mambo tuyaweke sawa kwa kuwa naumia sana, hawajui tu. Si kwamba, labda ni kwa kutaka msaada wao, hapana. Bali kila mtu awe ameitakasa nafsi yake na kuondokana na vinyongo.”

Baba huyo wa Diamond anasema hata mawasiliano na mzazi mwenzake ni pale anapojisikia.

“Tena wakati mwingine na maneno ya karaha, lakini ana afadhali kuliko mtoto ambaye mara ya mwisho tuliwasiliana akiwa na Wema Sepetu ambaye alikuwa akija naye hapa mara kwa mara kunisalimia,” anasema.

Kwa sasa maisha si mazuri

Abdul anajihusisha na biashara ya viatu. Huchukua viatu kwa malikauli katika soko la Karume na kuvipeleka kwa wateja wake mahali walipo.

“Lakini maisha kwa sasa si mazuri kwa kuwa nasumbuliwa na tatizo la miguu. Inanifanya wakati mwingine nishindwe kutembea muda mrefu,” anasema mzazi huyo.

“Kama unavyoniona miguu inaniuma na wakati mwingine nashindwa kuinuka hata kitandani.

“Naona ni wakati sasa na mimi kuwa na eneo la kufanya biashara hii, lakini ndio hivyo uwezo, walau ningekuwa na gari ningeweza kuzunguka nalo hata kwa kuendeshwa ili nisiwapoteze wateja wangu, lakini sina namna.”

Anasema hata uwezi wa kugharimia matibabu, hana. “Labda ningekuwa na bima ya afya ingekuwa msaada kwangu lakini ndio hivyo sina,” anasema.

Apata msaada mtandaoni

Hata hivyo, msaada wake mkubwa uko kwa mtoto wake wa hiari anayeishi London, Uingereza anayeitwa Zubeda. Walijuana na mtoto huyo katika mitandao ya kijamii baada ya kuona mahojiano yake akielezea maisha anayoishi.