Bajeti ya tatu ya Magufuli na mizania ya utendaji wake

Muktasari:

  • Viongozi hao ni pamoja na Deng Tsiaoping wa Jamhuri ya Watu wa China; Dk Mahithir Mohamed (Malaysia), Lee Kuan Yew (Singapore), Park Chung Hee (Korea), Nelson Mandela (Afrika ya Kusini), Quett Masire (Botswana) na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alimwelezea Rais John Magufuli kama kiongozi mashuhuri akimfananisha na viongozi wengine mashuhuri duniani, waliofanikiwa kuongoza mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika nchi zao.

Viongozi hao ni pamoja na Deng Tsiaoping wa Jamhuri ya Watu wa China; Dk Mahithir Mohamed (Malaysia), Lee Kuan Yew (Singapore), Park Chung Hee (Korea), Nelson Mandela (Afrika ya Kusini), Quett Masire (Botswana) na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Dk Mpango anasema viongozi hao walikuwa na sifa muhimu ambazo ni pamoja na dira au maono dhahiri kuhusu maendeleo ya nchi zao, hawasiti kutekeleza dira hizo kwa dhamira kubwa tena bila kusita au kubadili msimamo, ni jasiri, shupavu na wenye kuthubutu kutekeleza jambo wanaloliamini bila kigugumizi.

Sifa nyingine za viongozi hao ni kuwa na kipaji cha kujali maumivu ya wanyonge, waadilifu, wanaochukia rushwa na ufisadi, wenye nidhamu ya kazi ya hali ya juu, wanaoongoza kwa vitendo na kuvumilia magumu ili kuiletea nchi mabadiliko chanya.

“Napenda niwaambie Watanzania kwamba Mwenyezi Mungu ametutunukia kiongozi mkuu wa nchi, mheshimiwa Dk John Pombe Joseph Magufuli mwenye sifa hizo zote nilizotaja,” anasema Dk Mpango.

Mambo 10 aliyofanya

Akifafanua zaidi, Dk Mpango anataja mambo 10 ambayo Rais Magufuli ametenda na kuiletea nchi mafanikio ambayo ni pamoja na kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma.

“Ametekeleza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na uamuzi wa Chama Tawala wa mwaka 1972 wa kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma. Aidha, kwa mamlaka aliyonayo amepandisha hadhi ya Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji kuanzia tarehe 26/4/2018,” anasema Dk Mpango.

Anataja pia suala la kujenga ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite Mirerani wenye mzingo wa kilomita 24.5 kuzunguka machimbo ya madini ya Tanzanite katika Wilaya ya Simanjiro uliogharimu Sh5.42 bilioni.

Anasema lengo ni kudhibiti uchimbaji na uuzaji holela wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee na kuliingizia Taifa mapato.

“Katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, 2018 Serikali imefanikiwa kukusanya mrabaha wa Sh714.6 milioni,” anasema.

Anataja pia hatua ya kudhibiti uuzaji wa makinikia nje ya nchi na kutunga sheria kuwezesha nchi kunufaika na rasilimali zake, pia kuzuia usafirishaji wa makontena 277 ya makinikia nje ya nchi yenye thamani ya kati ya Sh829.4 bilioni na Sh1,438.8 bilioni na kuagiza kutungwa kwa sheria mpya za mfano katika Afrika kuwezesha nchi zenye maliasili kunufaika na rasilimali hizo.

Anazitaja sheria hizo kuwa pamoja na ile ya Mamlaka ya nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili ya mwaka 2017, Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi ya Mwaka 2017 na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2017.

Jambo lingine alilolitaja Dk Mpango ni kutoa elimu msingi bila ada na kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa zaidi ya mara nane.

Anasema katika kutoa elimu msingi bila ada, kila mwezi Serikali inalipa Sh20.8 bilioni. Kutokana na hatua hiyo, uandikishwaji wanafunzi wa darasa la kwanza umeongezeka kutoka watoto 1,568,378 mwaka 2015 hadi watoto 2,078,379 mwaka 2018.

“Uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha kwanza nao umeongezeka kutoka wanafunzi 448,826 mwaka 2015 hadi wanafunzi 562,695 mwaka 2017,” anasema.

Anaongeza kuwa fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo mgao uliotolewa mwaka 2017/18 ni Sh409.9 bilioni ikilinganishwa na matumizi halisi ya Sh367.4 bilioni mwaka 2015/16.

“Idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hiyo imeongeza kutoka wanafunzi 96,589 mwaka 2015 hadi 122,623 mwaka 2017.”

Katika sekta ya afya, Dk Mpango anasema Rais ameongeza bajeti kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kufikia Sh269 bilioni mwaka 2017/18 kutoka Sh31 bilioni mwaka 2015/16, hivyo kuimarisha huduma za afya.

Lingine ni ununuzi wa ndege ili kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambapo Rais Magufuli amenunua ndege mpya tatu aina ya Bombardier Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja ambazo tayari ziko nchini na zinafanya safari za ndani.

Mambo mengine ni pamoja na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi, ujenzi wa reli ya kati ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge railway – SGR), ujenzi wa mradi wa umeme katika Bonde la Mto Rufiji, kuimarisha usimamizi wa mapato ya ndani na kuendeleza umeme vijijini na kusitisha miradi ya wazalishaji binafsi wa umeme (IPPs).

Sifa hizo zimechambuliwa na vyama vya upinzani na wasomi wa masuala ya siasa na utawala wakizitazama na kipimo cha uongozi wa kiongozi huyo ndani ya miaka yake mitano.

Mapema mno kutoa sifa

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Profesa Mwesiga Baregu anasema ni mapema mno kumsifia Rais Magufuli kwa mambo hayo kwani bado yako kwenye hatua za mwanzo na mengi hayajaonyesha mafanikio ya kupigiwa mfano.

Profesa Baregu ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema anasema bajeti ya mwaka 2018/19 imeendeleza maneno matupu bila utekelezaji.

Anasema bajeti hiyo imepitwa mbali na ya nchi ya Kenya kwa kulinganisha kiwango anachopata kila mwananchi.

“Ukiangalia ‘budget per capita’ ya Kenya utaona ni Dola 625 kwa mwaka, Tanzania ni Dola 254, Uganda Dola 195 na Rwanda ni Dola 166. Tumepitwa mbali mno,” anasema.

“Kuna tatizo la kusifia tu kila kitu bila kupima utekelezaji. Ujenzi wa barabara, reli ya kisasa, ununuzi wa ndege au mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge bado vyote viko kwenye hatua za awali kabisa. Kwa nini tusingoje kwanza vifanyike ndiyo tusifie?”

Maamuzi ndani ya muda mfupi

Hata hivyo, mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Bubelwa Kaiza anasema Rais Magufuli anasifiwa kutokana na maamuzi yake ndani ya muda mfupi.

“Mafanikio hayapimwi kwa vitendo bali kwa muda uliotumika. Ukiangalia kipindi cha Rais (Ali Hassan) Mwinyi hakuna mambo makubwa aliyofanya tukayaona hapohapo, bali alikuwa akiendeleza yale ya Mwalimu Nyerere. (Benjamin) Mkapa alichofanya kikubwa ni kuuza na kubinafsisha mashirika ya umma, jambo lililoleta matatizo wakati wa Kikwete,” anasema.

“Mambo yaliharibika kwa mfano Shirika la ndege likafa. Lakini sasa Rais Magufuli amelifufua na amefanya maamuzi yaliyokuwa yamelala kwa muda mrefu.”

Msimamo wa Kaiza unapingwa na Waziri Kivuli wa Fedha, David Silinde anayesema mambo 10 anayosifiwa Rais Magufuli ni mchezo wa siasa.

“Sisi tutasoma bajeti yetu mbadala tuwaeleze wananchi kinagaubaga. Zile ni siasa tu, kwa mfano elimu bure bado kuna matatizo lukuki. Au huko kukamata makinikia tumepata nini sasa? Kuhamisha makao makuu Dodoma nalo ni jambo la kujisifia?” anahoji Silinde ambaye pia ni mbunge wa Momba kupitia Chadema.

Lakini mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana anaunga mkono kauli ya Kaiza akisema kiongozi hupimwa kwa maamuzi aliyofanya kulingana na muda aliokaa madarakani.

“Ukiangalia kwa mfano suala la kuhamia Dodoma lilikuwepo tangu mwaka 1972, lakini yeye alisema inyeshe mvua, mawingu yaje lazima atahamia. Mwinyi alikuja akaondoka hivyohivyo, Mkapa alikuja hakufanya kitu, Kikwete naye alizungumzia tu lakini hakutekeleza,” alisena na kuongeza:

“Hata hili la kununua ndege, tangu ilipovunjika Jumuiya ya Afrika Mashariki hatukuweza kununua ndege kama sasa. Leo tunanunua ndege sita tena kwa fedha za ndani bila mikopo, huo ni uamuzi mgumu.”

Kwa upande mwingine, hoja ya Silinde inaungwa mkono na mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro anayesema kwa maoni yake ni kama nchi haina bajeti kwa sababu Bunge haliheshimiwi.

“Hakuna bajeti katika nchi hii, ni kiini macho tu kwa sababu pamoja na Bunge kujadili na kupitisha, fedha hazipelekwi. Unakuta wizara inapelekewa asilimia 30 ya fedha za maendeleo na nyingine hazipelekwi kabisa,” anasema Mtatiro.

“Bajeti ya kweli ni pale unapotenga kwa mfano Sh10 bilioni kwa Wizara ya Kilimo, halafu mwaka unapoisha unasema tulitoa Sh9.8 bilioni, hapo utaeleweka. Lakini hiki kinachofanyika ni kiini macho. Fedha hazipelekwi kama inavyoamuliwa na Bunge na nyingine zinapelekwa bila ruhusa ya Bunge.”