Bashiru amesema kweli ila hakutaja maigizo yote

Muktasari:

  • Hoja ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kuhusu kupungua kwa idadi ya wapigakura imeleta mjadala mkubwa kwa wadau wa siasa nchini. Hata hivyo, hoja hiyo ingekuwa na nguvu zaidi kama Dk Bashiru kabla ya kuitoa nje na kupaza sauti, angeanza kusahihisha yaliyo ndani ya chama chake cha CCM ikiwamo kufuata utaratibu wa kura ya maoni kwa wagombea ubunge hasa katika wimbi la sasa la hamahama ya wabunge wa upinzani.

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally hivi karibuni alikuwa gumzo kutokana na kauli yake kuhusu kupungua kwa idadi ya wapigakura.

Alisema hivi sasa wananchi wanaona uchaguzi ni kituko na maigizo. Alionyesha kutopendezwa na idadi ya kura ambazo CCM inapata.

Dk Bashiru alitoa mfano wa Uchaguzi Mkuu wa 2010, akisema kwa mara ya kwanza Tanzania ilipata kiongozi asiye na uhalali wa kisiasa. Hili ni kweli, maana idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa watu milioni 20, waliopiga kura za urais ni milioni 8.63, sawa na asilimia 42.8. Waliopiga kura za ubunge walikuwa milioni 7.99, sawa na asilimia 39.7.

Hesabu hiyo ni kuonyesha kwamba asilimia 57.2 ya waliojiandikisha hawakumchagua Rais. Asilimia 60 hawakuchagua wabunge kwenye majimbo yao. Kumbe sasa, si tu kwamba Rais alikosa uhalali wa umma kisiasa, bali pia wabunge hawakuwa na hadhi stahiki, maana wananchi wengi hawakuwachagua. Ni sawa na kusema, mihimili miwili, Serikali na Bunge, haikubeba uhalali mahsusi kisiasa.

Bashiru apewe sifa kwa hoja yake. Hata hivyo, namkumbusha kutandika kitanda.

Kamanda wa zamani wa Jeshi la Majini la Marekani, William McRaven (Admiral), aliandika kitabu chake kinachoitwa “Make Your Bed”, yaani tandika kitanda chako. Katika kitabu hicho, McRaven anaeleza kuwa ukitaka kuibadili dunia, anza kwanza kutandika kitanda.

Anasema ukiamka asubuhi na kutandika kitanda, unakuwa umemaliza kazi namba moja katika siku. Baada ya hapo unaweza kutekeleza nyingine kwa mafanikio. Usipotandika kitanda utarukia kazi nyingine, hivyo utaacha kiporo na matokeo yake utalazimika kutandika wakati wa kulala au utalala bila kutandika.

Anasema ukitandika kitanda, hata ukifanya kazi zako na zikawa hazijaenda vizuri, siku ikawa mbaya, ukirejea nyumbani na kukuta kitanda kilichotandikwa, utalala ukiwa na matumaini ya kufanikiwa siku inayofuata.

Hata wewe fikiri, siku imekuwa ngumu, ghasia nyingi, halafu unakutana na kitanda kisichotandikwa.

Msingi wa McRaven ndani ya kitabu chake, “Make Your Bed” ni kuwa kama huwezi kuzingatia masuala madogo na kuyafanyia kazi kikamilifu, maana yake hutamudu yale makubwa zaidi.

Huwezi kuruka kazi iliyo mbele yako, ukimbilie nyingine. Kamilisha kwanza ya mbele yako. Ifanyie kazi inavyotakiwa. Baada ya hapo ndiyo uendelee na za mbele. Hapa ndipo napatumia kumkumbusha Dk Bashiru, kwamba alisema maneno mazuri lakini hajatandika kitanda. Yaani hajaanza na kazi namba moja.

Ni kweli wananchi wanaona uchaguzi ni kiini macho. Hata hivyo, kabla ya kutoka nje na kupaza sauti, Bashiru anapaswa kuanza kusahihisha yale yaliyopo kwenye ngazi yake. Kwa nafasi yake, yeye ndiye bosi wa sekretarieti ya CCM. Ndiye mtendaji mkuu wa chama.

Hivi sasa kuna wimbi la wabunge na madiwani kuhama vyama vya upinzani na kujiunga CCM, kisha haohao wanasimamishwa kugombea tena nafasi zao bila kupigiwa kura za maoni na wanachama wa majimbo yao au kata zao. Hii ni kinyume na Katiba ya CCM na linawakatisha tamaa wapigakura, lakini yeye haoni kama hiki ni kituko na maigizo.

Matokeo yake idadi ya wapigakura ambao wamekuwa wakijitokeza kwenye uchaguzi mdogo, imekuwa ndogo mno. Sasa inatakiwa Bashiru ashughulikie tatizo hilo ambalo lipo ndani yake.

Isionekane kuna mipango au mazungumzo kwa wenye kuhama ili wapewe upendeleo. Ionekane kweli wanahama wenyewe, kisha wanachukuliwa sawa na wanachama wengine waliowakuta.

Kuzuia wanachama wengine kuomba nafasi ya kugombea ubunge au udiwani kwenye majimbo au kata zao ni dhuluma ya kikatiba. Uchaguzi unapofanyika pia unabeba sura ya upande mmoja. Vyama vya upinzani vinalalamika hujuma. Hapo lazima wananchi waone kiini macho na wasusie kupiga kura.

Tutandike shuka safi

Hapa ni kumweleza Dk Bashiru kuwa si kutandika kitanda tu, bali kutandika kwa shuka safi. Malalamiko kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa haipo huru na haitendi haki, lazima yaangaliwe. Sheria za uchaguzi zinapaswa kuonekana zinatoa ushindani sawa. Siyo chama fulani kuonekana kinapendelewa.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar Oktoba 25, 2015 yalipofutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), uchaguzi wa marudio Machi 20, 2016 ulisusiwa na wapigakura wengi. Sababu ni wananchi kuona hakukuwa na usawa.

Bashiru kwa nafasi yake, anaweza kuchangamsha mchakato wa kupata sheria mpya na bora za uchaguzi. Chama chake ndicho chenye wabunge wengi. Anaweza kufanikisha.

Vinginevyo kama sheria za uchaguzi hazitafanyiwa mabadiliko chanya, kisha CCM ikiendelea kupokea wabunge na madiwani kisha kuwasimamisha kugombea nafasi zao bila kura za maoni, wananchi wataendelea kuona kauli ya Bashiru ni kiini macho kama ambavyo yeye amesema uchaguzi unaonekana ni kiini macho, maana sheria zilizopo zinalalamikiwa kukibeba chama chake.

Mfano wa Venezuela

Kuhusu sheria za uchaguzi zinavyoweza kuvutia au kukimbiza wapigakura, nitatoa mfano wa Venezuela.

Desemba 2015, muungano wa vyama vya upinzani nchini Venezuela, unaoitwa Democratic Unity Committee (MUD), ulishinda theluthi mbili ya wabunge, wakati chama tawala, United Socialist Party of Venezuela (PSUV) na muungano wao wa Great Patriotic Pole (GPP), ukiambulia theluthi moja.

Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti Marekani, taarifa ya Brookings ya Januari 8 iliyoandikwa na Harold Trinkunas, ushindi wa MUD kwenye uchaguzi wa wabunge, ulimfanya rais aliye madarakani, Nicolas Maduro apoteze umaarufu.

Brookings waliandika kuwa kila kura za maoni zilipofanyika, Rais Maduro alitajwa chanya kwa asilimia 30 na wananchi wa Venezuela wakati asilimia 70 zikiwa hasi. Hata kutukuzwa kwa mtangulizi wa Maduro na ambaye ni muasisi wa mapinduzi na Serikali ya Bolivarian, Hayati Hugo Chavez, kulipungua hadi kufikia asilimia 30.

Anguko hilo la umaarufu wa Rais Maduro na Serikali ya Bolivarian, lilizidishwa na ongezeko la umaskini uliofikia asilimia 81 mwaka 2017 kutoka asilimia 48 mwaka 2014. Idadi ya watoto waliopatwa na utapiamlo ilikua kwa kasi na watu wengi walikufa njaa.

Wakati huohuo, familia ya Rais Maduro ikawa inakabiliwa na kashfa kubwa ya dawa za kulevya. Novemba 2015, Flores de Freitas na Campo Flores ambao ni wapwa wa mke wa Rais Maduro, Cilia Flores, walikamatwa Haiti walipokuwa kwenye harakati za kuingiza dawa za kulevya Marekani.

Kukamatwa kwa wapwa hao wa First Lady, kuliipa afya minong’ono kuwa Serikali ya Bolivarian chini ya Maduro na tangu wakati wa Chavez, ilikuwa ikijineemesha kwa biashara ya dawa za kulevya, ikimiliki genge kubwa na lenye nguvu Amerika Kusini. Desemba 2017, vijana hao walihukumiwa kifungo cha miaka 18 jela na mahakama ya Manhattan, Marekani.

Kimsingi MUD ilikuwa imembana Rais Maduro kila upande na ilitarajiwa mwaka huu PSUV ingekabidhi hatamu ya uongozi kwa muungano huo wa vyama vya upinzani. Kinyume chake, Rais Maduro alishinda kwa kishindo kwenye uchaguzi uliofanyika Mei 20, mwaka huu.

Hata hivyo, mwaka 2017 Rais Maduro alicheza mpira mgumu ili kubaki madarakani. Msukumo mkubwa ulitokana na ukweli kwamba endapo angeng’oka kwenye urais, moja kwa moja angefikishwa mahakamani kwa kashfa za rushwa, ufisadi na kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Alichezea sheria za uchaguzi. Hilo ndilo liliwakatisha tamaa wapinzani. Waligundua ingekuwa vigumu kushinda na kuchukua madaraka kwa njia ya uchaguzi mikononi mwa Maduro. Kilichofuata ni MUD kugawanyika, baadhi ya vyama vikageuka vikundi vya waasi na vingine vilifanya siasa kila kimoja kivyake.

Uchaguzi wa Mei 20, ulikuwa na idadi ndogo ya wapigakura. Ni asilimia 46 tu ya waliojiandikisha ndiyo walijitokeza. Maana yake asilimia 54 hawakupiga kura. Tafsiri ni moja tu kuwa sheria za uchaguzi zinapoonekana kutoa upendeleo, hukatisha tamaa wananchi na hasa ya kupiga kura.

Katika uchaguzi wa mwaka 2013, idadi ya wapigakura waliojitokeza kuchagua rais wa Venezuela ilikuwa asilimia 79. Wingi huo ni kwa sababu sheria za uchaguzi zilionyesha hali ya ukaribu wa kutenda haki. Na mchuano ulikuwa mkali, ilidhaniwa Rais Maduro angeshindwa lakini alishinda kwa tofauti ndogo.

Alipata asilimia 50.6, wakati mpinzani wake, Henrique Capriles wa MUD alipata asilimia 49.1.

Mfano wa mwaka 2015

Uchaguzi Mkuu 2015 una majibu ya karibu kuhusu nini Watanzania hutaka kukiona ili wajitokeze kwa wingi kupiga kura. Wananchi hutamani kuona ushindani wa kisiasa. Siyo kwenda kupiga kura wakati mazingira yanaonyesha moja kwa moja mshindi ni nani.

Katika watu milioni 23 walioandikishwa kupiga kura mwaka 2015, zaidi ya milioni 15.6, sawa na asilimia 67, walipiga kura. Rais John Magufuli (CCM) alipata kura 8.9 milioni, asilimia 58, Edward Lowassa (Chadema) 6.1 milioni, asilimia 40. Hapa Lowassa aliwajengea imani wapigakura kura kwamba angepata kura za kutosha na angetangazwa mshindi.

Na aliutangazia umma kuwa wapige kura kwa wingi, akasema kuhusu Tume ingemtangaza nani mshindi, hilo aachiwe yeye. Na kwa vile Lowassa ni kiongozi aliyeshika madaraka makubwa, ilionekana kweli angeweza kuchaguliwa na kutangazwa. Hiyo ikawa hamasa ya watu wengi kujitokeza kupiga kura.

Pamoja na Lowassa kuwa Chadema na muungano wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), nguvu yake ya ushawishi ilivutia mpaka CCM kujitokeza kupiga kura kwa wingi ili kumchagua Magufuli, maana ilionekana wangezembea Lowassa angechukua kiti, Ofisi ya Rais, Ikulu.

Kipimo hicho pia kinatoa majibu kwamba wananchi wanapenda uchaguzi ambao unatoa sura ya ushindani.

Hawataki uchaguzi wa upande mmoja, kwamba mgombea wa chama fulani lazima ashinde. Dk Bashiru afanyie kazi hili ili chama chake kiwe kinaingia kwenye uchaguzi kama mgombea na siyo mtawala wa uchaguzi. Vinginevyo uchaguzi utaendelea kuwa kiini macho.