Bei ya mafuta yaibua mambo mazito Kenya

Sunday September 16 2018

 

Kenya inadaiwa kobe si wake. Hii ni kwa sababu ya tabia ya kuombaomba kutoka katika mataifa yaliyoendelea kama vile China ambako inadaiwa takriban fedha za Kenya Sh1 trilioni. Japan nayo inaidai Kenya mabilioni ya fedha.

Serikali pia imefika mlango wa Ubelgiji na Ufaransa na bakuli mkononi la kuomba. Sasa hatujui madeni hayo yatalipwa vipi na lini. Lakini, Serikali ya Jubilee ilitega sikio ilipokutana na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) linaoongozwa na Christime Lagard hivi majuzi na kutekeleza ushauri wake bila kujali athari za ushauri huo kwa Wakenya wanaojikakamua kuishi maisha magumu.

Ingawa Mahakama Kuu ya Jimbo la Bungoma imesimamisha ongezeko la bei za mafuta, uamuzi huo utatekelezwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini ama kukataa mabadiliko yaliyofanyika katika muswada wa fedha wa 2013 na wabunge.

Serikali iliongeza bei za dizeli, mafuta ya taa na petroli kuanzia Septemba Mosi baada ya ushuru wa bidhaa hizo bila kuzingatia ukweli, kwamba wananchi hawana uwezo wa kuzinunua kwa sababu ya uchumi unaodorora.

Kufuatia malalamiko ya Wakenya kuhusu kuongezwa kwa mafuta, wabunge walijadili hatua ya serikali kuongeza bidhaa hizo na wakaamua kuiahirisha hadi 2020. Waziri wa Fedha, Henry Rotich hakutaka kusikia uamuzi wa Bunge wa kuahirisha bei za mafuta kwa miaka miwili.

Sababu ya ongezeko la bei

Sababu ya kuongeza bei ya mafuta ni madeni. Serikali haiwezi kulipa madeni yake bila fedha, hivyo iliona heri iongeze bei iweze kulipa madeni.

Wakenya wanahisi vibaya kulipa madeni ambayo hayakuwasaidia. Asilimia 70 ya madeni huporwa na maofisa wa vyeo vya juu katika serikali na kuacha fedha kidogo ya kuweka hapa na pale kuwadanganya Wakenya kwamba wanafaidika ilhali si kweli.

Madeni hayo si mazuri kwa afya ya nchi. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba madeni hayo yanaongezeka.

Rais Uhuru alizuru Marekani wiki jana ambako Serikali ya Rais Donald Trump ilimpa mkopo wa Dola380 bilioni za kupanua barabara kuu ya Nairobi–Mombasa. Mara aliporejea kutoka Washington DC, alisafiri tena kwenda China kuomba msaada wa mabilioni ya kujenga reli hadi Jiji la Kisumu katika eneo la Nyanza.

Wakenya wanahoji kwa nini Jubilee inaangazia barabara ilhali wananchi hawana fedha mifukoni. Nani atatumia barabara hizo kama umasikini unawanyonga Wakenya? Jubilee ilipochukua hatamu ya uongozi, Kenya ilikuwa na deni chini ya trilioni moja lakini sasa inazama katika bahari ya madeni.

Wananchi lazima walipie uamuzi wa viongozi wao. Hali hii ya kusikitisha imewalazimu Wakenya kuwa wakimbizi wa mafuta katika nchi jirani. Wakenya wanaoishi mipakani huvuka mipaka kununua mafuta nafuu. Wakazi wa Busia na Malaba sasa wananunua mafuta kutoka Uganda huku wale wa Moyale katika eneo la Kaskazini mwa Kenya wanavuka mipaka hadi Ethiopia ambapo mafuta ni nafuu.

Uganda ni nchi isiyopakana na bahari na hutumia bandari ya Mombasa, kuagiza bidhaa za mafuta. Ni kimzungumkuti kwamba mafuta ni bei rahisi Uganda na ni ghali nchini Kenya.

Katika bara hili la Afrika, Kenya ndio nchi inayouza mafuta kwa bei ya juu. Nchini Uganda petroli inauzwa Ush3,750 (Ksh110) huku dizeli ikiuzwa kwa Ksh 102. Petroli katika miji ya Busia na Malaba petroli inauzwa kwa Ksh131 huku dizeli ikiuzwa kwa Ksh118.

Huku hasira za kuongezewa kwa mafuta ikiendelea kupanda, kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga amesema Rais Uhuru atatatua tatizo hili. Makamu wa Rais, William Ruto pia amesisitiza kuwa suluhisho la bei ya juu ya mafuta litapatikana. Kwa kuvuka mipaka, Wakenya wanaokoa Ksh20 (Sh440 za Tanzania) kwa kila lita ya mafuta wanayonunua katika nchi jirani.

Ingawa kununua kwao mafuta katika mataifa jirani kunainyima serikali ushuru, Wakenya wanajaribu kujiokoa kutokana na sera zinazowapora fedha.

Rais Uhuru hajaweka saini uamuzi wa wabunge wa kuahirisha ongezeko la bei za mafuta. Wakenya wanatumaini atafanya hivyo mapema.

Kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, nauli za magari ya umma zimepanda na kuleta taharuki kwa Wakenya ambao tayari wamezidiwa na ugumu wa maisha.

Bei ya umeme pia imekuwa ghali huku serikali ikisema haitaendelea kuongeza bei ya nishati hiyo.

Gharama za usafiri

Wasafirishaji wa bidhaa za mafuta wanatishia kugoma hadi Serikali ishushe bei ya mafuta. Tayari, vituo vya mafuta vinakabiliwa na uhaba wa mafuta kwa sababu hii.

Tume inayosimamia masuala ya mafuta nchini (ERC) imeghadhabishwa na hatua ya wasafirishaji hao na imetupilia mbali leseni zao za biashara. Hii si hatua nzuri kwa sababu itachochea walanguzi wa mafuta na bidhaa nyingine zinazohusishwa nayo.

Madereva wa teksi wanalalamika kwamba wamepoteza wateja wao kwa sababu ya kuongezeka kwa nauli. Huku waendeshaji wa pikipiki za kusafirisha abiria wakiendelea kwenda Uganda kwa sababu ya bei nafuu, wamiliki wa matatu (daladala) wanasema hawajavuka mpaka kununua mafuta rahisi Uganda. Hii ni kwa sababu mzigo wa nyongeza ya mafuta umehamishiwa kwa abiria wao.

Pia, magari yanafaa kulipa ada za kuingia Uganda na hii inaongeza masahibu ya kutafuta mafuta na kuleta hasara badala ya faida. Vilevile, kwa kuwa maofisa wa kulinda mpaka wanajua kwamba mafuta yameongezwa Kenya, hawawezi kukubalia magari ya umma kuvuka na kuingia nchi hiyo.

Hatua hii ya serikali, imepanda mbegu za uhasama kati ya wasafiri na wamiliki wa matatu. Abiria wanasema wamiliki wa matatu wanawapora kwa kuongeza nauli. Kwa mfano, nauli kutoka Busia hadi Mumias ambapo wasafiri wamekuwa wanalipa Ksh150, sasa mambo ni mengine; wanalazimishwa kulipa Ksh200.

Kutoka Busia hadi Kisumu, wasafiri sasa wanalipa Ksh350 kutoka Ksh300.

Shirika la kuwatetea wafanyakazi, Cotu imeishtaki serikali huku matatu zikigoma katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Siasa yaingizwa

Wafuasi wa upinzani wanawasuta wale waliowachagua Uhuru na Ruto wakiwaambia wakabiliane na hali yao kwa sababu kama wangemchagua Raila, shida hii haingetokea.

Jiji la Nairobi sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta baada ya malori ya kusafirisha mafuta kukataa kubeba bidhaa hiyo kutoka kwa vituo vya kugawa mafuta yanayosafirishwa kwa kila pembe ya Kenya.

Baada ya mkutano wao wasafirishaji wanasema wameamua kuunga mkono wamiliki wa magari ya umma na ya kibinafsi kususia mafuta. Hali ni hiyohiyo katika Jimbo la Mombasa.

Mwanaharakati mkuu wa Kenya, Okiya Omtatah amewasilisha ombi mahakamani akitaka ushuru huo wa asilimia 16 ukomeshwe mara moja.

Katika jimbo la Nakuru, usafirishaji uliathiriwa vibaya baada ya wamiliki wa matatu kugoma kufuatia kutekelezwa kwa ushuru huo ambao sasa imekuwa adui ya Wakenya.

Wamiliki wa matatu wanamtaka Waziri Rotich ajiuzulu mara moja kwa kuongezeka kwa bei za mafuta.

Mnamo 2013, sheria ya kuongeza mafuta iliahirishwa hadi 2016 na tena ikaahirishwa hadi 2018. Mabadiliko yaliyofanyiwa Muswada wa Fedha wa 2013 hivi majuzi bungeni yanasubiri uamuzi wa Rais ambaye ataamua kama ataweka saini au la.

Rais pia anaweza kurudisha Muswada huo bungeni ukiwa na mabadiliko ama atie saini iwe sheria. Kama Uhuru anapenda Wakenya hana budi kuweka saini yake kwa mabadiliko hayo na kushusha bei ya mafuta.

Wale wanaotaka Rotich ajiuzulu wajue kuwa tatizo hili haliko mbele yake bali ni Rais Uhuru tu ambaye anaweza kuokoa Wakenya.

Liwe liwalo, Wakenya hawana budi ila kuvumilia kuwa Wakenya. Kama unafua nguo, maji lazima uyashike.

Advertisement