CCM kila zama na vita mpya vya wenyewe kwa wenyewe

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally hivi karibuni alituma wito hadharani kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akimtaka aende ofisini kwake ili wazungumze na amhoji kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Alisema Membe anatuhumiwa kufanya jitihada za kumkwamisha Rais John Magufuli. Tuhuma hizo zilianzia kwa mtu aliyejipa jukumu la kutambua na kutaja majina ya watu hatari kwa nchi na ambao wanamhujumu Rais Magufuli.

Tangu wahusika waanze kutajwa, hakuna yeyote aliyewahi kuhojiwa na jeshi la polisi. Hata mtaja majina hajawahi kusikika ameitwa mahali ili vyombo vya usalama viweze kufanyia kazi tuhuma zake.

Katika orodha ya watu aliowatuhumu kumhujumu Rais Magufuli, limo mpaka jina la aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulraham Kinana. Angalau alipoguswa Kinana, mtaja majina aliitwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, lakini baada ya hapo ni kimya.

Ajabu ni kuwa wanaotajwa hawajawahi kuchukua hatua yoyote dhidi ya anayewataja.

Wanaotajwa kuhusika

Waliotajwa ni wengi, ila Bashiru amemwita tu Membe. Aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro pia aliwahi kutajwa ni mtu hatari na anayemhujumu Rais Magufuli. Hivi sasa Mtatiro yuko CCM na muunga juhudi za Rais. Je, CCM ilimpokea mtu hatari kwa nchi na anayemhujumu mwenyekiti wa chama au alitubu?

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alitajwa pia kuwa mtu hatari. Aliyemtaja ndiye huyohuyo aliyewataja Membe, Mtatiro, Kinana na wengine. Hivi karibuni Bashiru alimsifu Zitto kuwa huibua hoja nzuri za kiuchumi na akamkaribisha CCM.

Je, Bashiru anampuuza aliyemtaja Zitto kuwa ni mtu hatari? Anamuona Zitto ni mtu mzuri? Mbona Membe kamwita? Anachagua ukweli wa kuuamini kutoka kwa mtaja majina?

Mazoea CCM

Jinsi Bashiru alivyomwita Membe ni wazi ameshaingia kwenye mtego na sasa ni dhahiri CCM kunafukuta. Iwe kwa ukweli au hisia, CCM ina makundi mawili yanayohasimiana.

Kama ukweli huo au hisia hizo zisingekuwepo, Bashiru angepuuza maneno ya mtaja majina na asingemwita Membe. Wito ni dalili kuwa ama ni kweli au hisia kuwa CCM ipo vipande viwili.

Hivyo ndivyo imekuwa kwa CCM miaka yote. Makundi ya watu wenye kupingana ndani kwa ndani huibuka nyakati zote za uchaguzi. Kuelekea mwaka 2015 yalikuwepo makundi ya akina Membe, Samuel Sitta (marehemu) na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Kipindi hiki kukiwa na makundi au kuwepo kwa hisia za uwepo wa makundi, moja likimuunga mkono Rais Magufuli na lingine likituhumiwa kumhujumu, wakati wa Jakaya Kikwete kulikuwa na kundi la walioitwa mafisadi na wengine wapambanaji dhidi ya ufisadi.

Makundi ya watuhumiwa wa ufisadi dhidi wapambanaji dhidi ya ufisadi, yalisababisha CCM ipitie nyakati ngumu. Nyakati za majaribio ya kufukuzana kwa kile ambacho walikiita ni kujivua gamba.

Mnyukano huo ndio ulisababisha makatibu wakuu wawili wa CCM wasidumu. Yusuf Makamba aliyekivusha chama kwa mbinde kwenye Uchaguzi Mkuu 2010, akafuata Wilson Mukama aliyekaa mwaka mmoja.

Historia hiyo imwonyeshe Bashiru kuwa kuuingia mtego wa makundi ndani ya CCM gharama yake ni kubwa. Vipi mtaja majina akiwa anatumika kuleta uchonganishi ndani ya chama?

Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela, kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu 1995 alidaiwa kabadili dini kuwa Muislamu na kwamba nchi za Kiarabu zilitaka kumtumia.

Kuelekea mwaka 2005, aliyekuwa Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye aliandamwa kuwa alijimilikisha mali nyingi za umma. Hiyo ndiyo CCM, kila zama na makundi ya vita vya ndani wenyewe kwa wenyewe.