Chadema yasaka kilichowanyima kura Kanda ya Ziwa mwaka 2015

Muktasari:

  • Chama hicho kimeanza kujijenga kupitia vikao hivyo baada ya serikali kufuta mikusanyiko na mikutano ya hadhara, lengo likiwa ni kurejesha uungwaji wa mkono katika majimbo na kata ilizopoteza mwaka 2015.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mikoa ya Kanda ya Ziwa, kimeanza mkakati wa kujiimarisha kupitia vikao vya ndani na makongamano kuelekea uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Chama hicho kimeanza kujijenga kupitia vikao hivyo baada ya serikali kufuta mikusanyiko na mikutano ya hadhara, lengo likiwa ni kurejesha uungwaji wa mkono katika majimbo na kata ilizopoteza mwaka 2015.

Katika uchaguzi uliopita Chadema ilitetea majimbo matano ya uchaguzi Kanda ya Ziwa, huku majimbo mengine iliyokuwa imeshinda mwaka 2010 yakichukuliwa na CCM.

Kabla ya uchaguzi huo, Chadema ilikuwa ikiongoza majimbo karibia 10 ya uchaguzi Kanda ya Ziwa kati ya majimbo 43, lakini ilipokonywa na kusaliwa na Ukerewe, Bukoba Mjini, Tarime Mjini, Tarime Vijijini na Bunda.

Majimbo yaliyochukuliwa na CCM kutoka mikononi mwa Chadema ni Ilemela, Nyamagana, Maswa Mashariki na Maswa Magharibi, Bukombe, Biharamulo, Meatu na Musoma Mjini.

Akizungumza katika kikao cha ndani cha chama hicho Kata ya Igogo ikiwa ni ziara yake ya kutembelea majimbo yote ya uchaguzi Kanda ya Ziwa, Katibu wa Chadema Kanda ya Ziwa, Rehema Mkoha alisema chama hicho kimejipanga vizuri na kitaendelea kusimamisha wagombea kwenye mitaa yote ya majimbo ya uchaguzi.

Anawataka viongozi kuongeza juhudi za kukijenga chama hicho, licha ya kuwapo baadhi ya wanachama waliochaguliwa kutetea majimbo na kata kuhamia chama kingine.

Anasema watumie changamoto hizo na vikwazo ndani ya chama kujiimarisha tayari kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Anataja moja ya nguzo zitakazosaidia kufikia malengo kwamba ni kila mtaa na tawi kuwa na uongozi utakaojenga msingi imara wa kuwasaidia kupata ushindi katika uchaguzi ujao.

Katibu huyo anasema njia nyingine itakayosaidia kuongeza ushindi ni kuhakikisha wanaorodhesha watu wanaohitaji kadi na kuhakikisha wanatembea nyumba kwa nyuma kuongeza wanachama.

Kilichowakwamisha

Bila kutaja moja kwa moja, Rehema anasema miongoni mwa sababu zilizokwamisha chama hicho kushinda viti vingi kwenye uchaguzi uliopita ni pamoja na kukosa ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wagombea na wanachama.

Lakini pia anataja sababu nyingine kuwa ni usaliti.

“Wanachama wanashindwa kumuunga mkono kiongozi aliyesimamishwa kugombea kiti hicho badala yake wanampigia kura mtu mwingine,” anasema.

Uchache wa viongozi na wenye ushawishi kwenye kata na mitaa pia ni sababu nyingine ambapo akitolea mfano kwenye Kata ya Igogo pekee, mbali na wanachama wa kawaida katika kikao cha ndani, kungekuwepo na viongozi wa mitaa, matawi na wajumbe wasiopungua 400.

Akifafanua zaidi alisema kata hiyo yenye jumla ya mitaa tisa ilitakiwa kuwa na misingi 27, na tawi moja linatakiwa kuwa na watu 15, hivyo Kata ya Igogo ilitakiwa kuwa na matawi manne, mabalozi 135 na wajumbe 135.

Ukandamizani demokrasia

Katibu huyo pia akaelezea kukandamizwa kwa demokrasia kwa kusitisha mikutano ya hadhara huku baadhi ya viongozi wa upinzani wakikamatwa na kufunguliwa mashtaka ndani na kudai kuwa jambo hilo limewapa fursa ya kufanya vikao vya ndani ambapo awali havikupewa na nguvu kubwa ilielekezwa kwenye mikutano hiyo.

Lakini pia kiongozi huyo alisema kinachofanywa na serikali si tu ukandamizwaji na uminywaji wa demokrasia bali ni wanahakikisha wanaua kabisa upinzani.

“Kinachofanywa na serikali si cha kidemokrasia na bali ni kufanya baadhi yao waishi kama malaika huku wengine wakiishi kama mashetani,” alisema.

Wanachama kutimkia CCM

Mapema mwaka huu akizungumzia suala la wanachama kutimkia CCM, Makamu mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa, Ansbert Ngurumo anasema ni heri kusalia na wanachama wachache wenye msimamo, moyo na nia ya dhati katika kile wanachokiamini kuliko kuwa na kundi la wanaoyumba na kusaliti itikadi.

Alisema Chadema ni taasisi kubwa isiyoyumbishwa na viongozi na wanachama wachache wanaohamia vyama vingine.