VIDEO: Dovutwa: Mvuto wa Lowassa ulitufunika 2015

VIDEO: Dovutwa: Mvuto wa Lowassa ulitufunika 2015

Muktasari:

  • Katika safu ya mahojiano leo tunazungumza na Fahmy Nasorro Dovutwa ambaye ni mwenyekiti wa chama cha UPDP. Dovutwa alijitosa katika mbio za urais kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kushika nafasi ya mwisho, akiwa amepata asilimia 0.16. Katika makala haya, Dovutwa anazungumzia mambo mbalimbali ya kisiasa. Na juhudi zake mwaka 2015 hazikuweza kuboresha matokeo yake; alipata kura 7,785 badala ya zaidi ya 13,000 alizopata awali. Endelea

Swali: Umewahi kugombea urais mara mbili, una mpango wa kuwania mara tatu mwaka 2020?Jibu: Mungu akipenda nitagombea.Swali: Una maana gani, una maana wewe hujiandai ila unasubiri itokee tu?Jibu: Maandalizi yapo lakini unajua kuna suala la afya na uzima. Afya ikiwepo na uzima ukiwepo nitagombea. Unajua hakuna namna nyingine ya kumtambulisha mwanasiasa kama uchaguzi.

Swali: Ulipogombea mara ya kwanza mwaka 2010 katikati ya kampeni ulijitoa. Ukasema kura zako ziende kwa Jakaya Kikwete. Hii ilikuwa sawa?

Jibu: Hilo suala lilipotoshwa. Yalitokea hayakusemwa na ambayo hayakutokea ndiyo yaliyosemwa.Swali: Wewe ulisemaje?.

Jibu: Mimi nilisema baada ya kushindana na Tume ya Uchaguzi kwamba jina langu limekosewa katika karatasi za uchaguzi na Tume ikang’ang’ana kwamba walivyoandika wao ndivyo nilivyoandika mimi. Nikaamua kujitoa. Mimi ni Fahmi Nassoro Dovutwa, wao waliandika Yahmi Nassoro Dovutwa. Yahmi siyo Fahmi.

Swali: Lakini mgombea alikuwa wa chama cha UPDP na wewe ndiye ulitoka UPDP?.

Jibu: Wala hakuna mtu anayeitwa Yahmi. UPDP haina mtu huyo. Hata wagombea wenzangu walisema. Christopher Mtikila alikwenda Tume akasema yule siyo ya Yahmi na Fahmi. Mtu mwingine wa Demokrasia Makini naye alikwenda akawaambia lakini walikataa. Kwa hiyo baada ya kukataa, nikasema hakuna sababu. Kama risiti iliyotoka mahakamani na vielelezo vingine vinaonyesha Fahmi, lakini wao wakang’ang’ania Yahmi, nikasema basi huyo mgombea wao wanayemtaka aendelee lakini tutakutana mahakamani.

Swali: Huko mahakamani uliambulia nini?Jibu: Niko mahakamani. Ila wakati niko katika Bunge la Katiba, wakili wangu aliyumba kidogo na kesi ikatupwa. Sasa niko katika hatua ya rufaa. Hadi sasa tangu 2014 sijapata nakala ya hukumu ili nikate rufaa.Swali: Katika kesi hiyo unataka nini? Jibu: Ninachotaka mahakama itamke kwamba jina lililotumika pale si langu.

Swali: Baada ya tamko hilo watengue matokeo au iweje?Jibu: wanilipe fidia. Kwa sababu aliyeshinda uchaguzi wakati huo (Kikwete) hayupo tena madarakani.

Swali: Kwanini uliamua kura za Yahmi ziende kwa Kikwete na si kwa mgombea mwingine?Jibu: Kikwete si ndiye alimchagua mwenyekiti wa Tume. Hao wengine, (akina) Slaa, Lipumba hawakumchagua mwenyekiti. Wao wangetafuta mtu wao.

Kikwete alikuwa mgombea wa CCM na Tume iko loyal (tiifu) kwa CCM. Kwa hiyo nikasema mpeni huyohuyo mgombea wenu. Swali: Lakini hilo jina unalolikataa lilipata kura 13,176, si za kwako hizo?Jibu: Huyo si mimi. Wewe sidhani kama inaweza ikatokea unasema ‘Bwana Yahmi nakuomba’. Hata kama ningeshinda watu wangekuja kunipinga. Wangesema ‘huyo si Yahmi, ni Fahmi, leteni pasipoti yake au vitambulisho vyake’.Swali: Mara ya pili ulipogombea mwaka 2015 kura zikapungua hadi 7,785, nini kilitokea?.

Jibu: Unajua mwaka 2015 uchaguzi ulikuwa na faulo nyingi sana. Chama cha Mapinduzi kilicheza faulo na Ukawa nao walicheza faulo. Kwa hiyo, kwa wakati ule lazima tukubali nguvu ya Ukawa na hasa nguvu ya Lowassa ilikuwa na mvuto sana kwa wananchiilitufunika.Swali: Bado unauona huo mvuto wake?

Jibu: Kwa vile Ukawa wenyewe umekuwa si Ukawa ule, sidhani kama utakuwapo tena huo mvuto.Swali: Ukawa ile ikoje na ya sasa ikoje?.

Jibu: Ukawa ile ilikuwa na akina Emmanuel Makaidi, ilikuwa na CUF ambayo sasa ina matatizo; ilikuwa na NCCR ambayo nayo ina matatizo. Karibu kila chama kina matatizo, kwa hiyo Ukawa imebakia ni Chadema. Kwa hayo (Lowassa) hana nguvu ile ya mwanzo aliyokuwa nayo akiwa na washirika ambao wengi hawapo.

Swali: Nje ya Ukawa hakuna vyama vingine vikubwa?.

Jibu: Kitu ambacho mara nyingi nakizungumzia lakini hakitiliwi maanani. Umefika wakati vyama vya upinzani tukae. Tuna tofauti zetu, lakini tukao. Yanayotokea yanatuathiri wapinzani wote. Na CCM haichagui kusema huyu UPDP, huyu NCCR, inasema imeushinda upinzani. Ukitazama wazee wetu hawakuwa wanabagua wapinzani. Mfano Mtikila alikuwa ni mkorofi lakini walikuwa hawamuachi nyuma. Yeye alikuwa anapenda kwenda mahakamani. Mkikaa, mkazungumza na kumaliza bila kutaka kwenda mahakamani yeye hakubali, lakini walikuwa wanakaa naye.

Swali: Umesema Mungu akipenda utagombea tena urais. UPDP bila shaka mna watu wengi, huoni mwanachama mwingine wa kushika kijiti?

Jibu: Uchaguzi uko huru, mimi nitachukua fomu na mwingine achukue fomu. Mwenye vigezo (sifa) atapita.

Swali: Ulipogombea mara ya kwanza na ya pili ndani ya chama mlishindanishwa?

Jibu: Mimi nilichukua fomu, wengine wote hawakuwa tayari kuchukua fomu. Unajua vyama vyetu unagombea uchaguzi kwa fedha zetu za mfukoni. Mtu anaona kuzipiga moto pesa zake ambazo angetumia kusomesha watoto au kujenga nyumba, inakuwa si rahisi. Unajua watu wengi huwa wanadhani tunapata pesa kutoka serikalini. Sasa wanapokuja huku na hakuna pesa za serikalini wanarudi nyuma.

Swali: Yapo madai pia kuwa mnapewa pesa na CCM pia?

Jibu: Mimi sijaziona hizo pesa. (Sisi na) Chama cha Mapinduzi ni kukutana kwenye mikutano na kucheka tu, lakini linapokuja suala la uchaguzi hawamjui mtu.

Swali: Ulipogombea mara ya mwisho ulitumia shilingi ngapi?

Jibu: Nilitumia pesa za kutosha.

Swali: Pesa za kutosha ni kiasi gani?

Jibu: Sijaangalia.

Swali: Hukuwa na bajeti?

Jibu: Bajeti ilikuwapo lakini haikufikiwa, ndiyo maana tulikosa. Kwa hiyo kujua zilitumika kiasi gani mpaka nirudi ofisini.

Swali: UPDP mna ofisi?

Jibu: Nyingi tu. Makao makuu ipo Mtaa wa Mtoni Kidatu, Zanzibar; Dar es Salaam iko Mwembechai. Katibu mkuu yuko Zanzibar.

Swali: Umesema ofisi zipo nyingi, nyingine ziko wapi?

Jibu: Buguruni, Dar es Salaam, Pwani ipo Kisarawe, Morogoro Mjini, Dodoma na nyingine.

Swali: Hizi ofisi zina watumishi. Je, zinalipiwa na nani na watumishi wanalipwa au wanajitolea?

Jibu: Tunazilipia sisi wanachama na zina watumishi. Hawa wanajitolea tu, kulipwa mpaka tupate uhuru.

Swali: Uhuru gani tena?

Jibu: Tushike nchi. Kwani hata waliokuwa wanachangia Tanu, uhuru ulipopatikana wakakoma kuchanga.

Swali: Kwanini kwenye chama unajulikana wewe tu, kwa nini viongozi wengine hawajulikani?

Jibu: Hakuna kitu ambacho kina umimi kama kwenye siasa. Mimi kuna kitu nahitaji kwenye siasa. Mfano, CCM wameboronga, nahitaji kutaka kusema CCM wameboronga. Lakini, wanajua CCM wanaharibu, lakini mtu kutoa chake na kwenda kusema CCM wameboronga inakuwa vigumu. Kama mtu anataka kujulikana atoe chake ajulikane. Kama wewe hela yako unataka kukaanga mayai, hiyo ni juu yako.

Swali: Kwa utafiti au makisio UPDP ina wanachama wangapi?

Jibu: Tangu tumeanza kuchapa kadi tumeshafikia watu 115,000. Hata hivyo hatuna uhakika kama bado wapo.