Emmanuel Amunike, unaweza kuifanya nyeusi kuwa nyeupe

Muktasari:

  • Yupo aliyeniulizia David Mwantika anacheza klabu gani kubwa duniani kwa sasa, huyu anamkumbuka Mwantika kwenye ule mchezo kati yetu na Nigeria.

Katika namna ya ajabu, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imekuwa maarufu nchini Nigeria, inapendwa na inafuatiliwa. Katika mchezo uliopita dhidi ya Uganda nimepata simu kadhaa kutoka kwa baadhi ya waandishi wa habari wakiulizia namna gani Watanzania wanamkubali Emmanuel Amunike.

Yupo aliyeniulizia David Mwantika anacheza klabu gani kubwa duniani kwa sasa, huyu anamkumbuka Mwantika kwenye ule mchezo kati yetu na Nigeria.

Pia yupo aliyeniambia kwanini Samatta hafiki Ligi Kuu England au La Liga mpaka sasa. Nikagundua hizi ni stori tu ili wapate pa kuanzia kuelekea kwenye ujumbe wao wanaouhitaji, nao ni kocha wao Amunike.

Katika udadidisi nikagundua kuwa Amunike ni “legend” anayeaminika kwao na ni mtu ambaye wanaamini angekuwa na tija kwenye soka lao hasa soka la vijana lakini “Afrika ni kama ilivyoandikwa kuwa nabii hakubaliki kwao” ingawa hii haikuwa msingi hasa wa kuamini walichosema bali nilitaka kufahamu chakula kipi angetuwekea mezani ili nasi tushibe.

Kihistoria Mheshimiwa Rais Mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi alishatengua kauli ya kichwa cha mwendawazimu ambayo wengi tulizoea kuinukuu, na kihistoria pia ni kuwa tuna miaka zaidi ya arobaini tangu twende kushiriki Fainali za Afrika na hakuna uhakika wa kurejea tena. Labda utokee muujiza mwaka huu.

Aliwahi kufika Maximo akainua ari ya mgonjwa mahututi walau akatabasamu na kula chakula na ndugu zake wakawa wanakuja uwanja wa Taifa kwa nguvu kumtizama lakini hali ilizorota na akarejea tena chumba cha uangalizi maalumu “ICU” na mpaka leo hajatoka.

Hajafanikiwa kutoka kwa sababu wahisani wa soka letu pamoja na wasimamizi hawafahamu watamtoa vipi aidha kwa makusudi au kwa kutokufahamu. TFF wanasigana wao kwa wao, waandishi wanatizama kipi kinawalipa na viongozi wanatizama chakula kipi kinaleta kitambi kwa haraka zaidi.

Kwa wazee wenye imani waliwahi kusema kile kilichoandikwa na wengine tukakisoma kuwa chui hawezi kubadilika madoa. Tanzania imekuwa ni chui huyu ambaye soka lake halieleweki safari yake ni ipi, kwenda mbele au kurudi nyuma.

Wengi tumefurahi na tumeungana na Wanigeria hawa kufurahi namna tulivyocheza na Uganda, jirani zetu ambao tulitakiwa kuwa na imani kuwa wanafungika lakini mazingira tuliyokulia hayaturuhusu kuamini hivyo.

Kwa imani hii tunaelekea kuwatizama wachezaji hawa wakiwa wanacheza dhidi ya Cape Verde siku si nyingi kabla ya mchezo wa marudiano ndani ya siku nne pekee. Tupo katika kundi ambalo ni rafiki na hatuhitaji kukwepa mishale mingi ili twende Cameroon mwakani. Changamoto pekee ni kuwa hatukuwahi kuwa wanafunzi wazuri wa hisabati.

Hesabu ya kipi kifanyike ili kwenda hatua inayofuata hatukuwahi kuyaweza, hatujawahi hata kuwa wepesi wa kuiga na kutizamia hesabu ambazo wanafanya wengine.

Watalaamu wanasema punda na pundamilia wanafanana vitu vingi lakini hawawezi kuwa mnyama mmoja. Pengine kama Chui hawezi kubadili madoa yake basi sisi tunaweza kuigilizia na kumbadili punda huyu awe pundamilia japo kwa wakati mfupi.

Kazi hii ndiyo aliyokuwa nayo Amunike, kutuvusha kwenda kwenye fainali za mataifa ya Afrika. Sio kazi nyepesi lakini mwanga upo, na tunaweza kabisa kumdhibiti Farouk Miya na nduguye Emmanuel Okwi. Kwa sasa hatokuwa na uwezo wa kumfundisha Ibrahim Ajib kupiga pasi aliyompa Ngassa kwenye mchezo dhidi ya Stand United kila mara, bali anaweza kumfanya ajitume mara mbili zaidi ya anavyojituma kwa sasa.

Jukumu la Amunike ni kuhakikisha kuwa kila mchezaji anaomba kubadili jezi aliyovaa wakati wa mapumziko wa mchezo kwa sababu imeloa sana na inamkera mwilini, lazima walipiganie taifa ndani ya uwanja na washabiki watalipania nje ya uwanja.

Kama nchi kuna tamaa moja tu haijalishi inakamilishwaje, nayo ni mataifa ya Afrika. Bahati nzuri zaidi ni kuwa Amunike anafika katika kipindi ambacho safu yetu ya ushambuliaji, kiungo na beki ina majina unayoweza kutaja na ukaeleweka, majina yanayocheza soka la ushindani mbali nje ya nchi.

Sitarajii kuanza kupambana na Domayo awe na pasi za Sergio Busquet kwa sasa, natamani kuona upiganaji tu na hii inaanza kwenye nidhamu ya mchezo baada ya kuonyesha kuwa nidhamu ya timu ameanza kuisimamia na ungeweza kuona wachezaji wanazungumza lugha moja hata baada ya wale sita kufungiwa.

Pata matokeo kwenye Uwanja wa Cape Verde na Watanzania watajaza Uwanja wa Taifa kwa ngoma na mirindimo ya makabila yote, kuanzia Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya iwa mpaka Pwani bila shida yoyote bila kusahau ndugu zetu wenye gesi upande wa Kusini.

Lakini kubwa zaidi hii itampa heshima Amunike nyumbani kwao Nigeria ambao wanachukua muda wao kutazama mechi za timu yetu ya Taifa kwa sababu wanaamini ni kocha bora ambaye ameshindwa kutumika nchini mwao.

Baada ya Mheshimiwa Mwinyi kutengua laana, baada ya wachezaji wetu kadhaa kuwa na visa kwenye pasi zao za kusafiria na huku pia tukiwa tumeshaonyesha kuwa tunaweza kucheza hata na wababe wa kanda yetu hii, kwa sasa Amunike anatakiwa apambane timu iwe na morali tu kuliko hata ubunifu.

Wachezaji wanatakiwa kuamini tu kuwa muda ni wao huu, na sasa Punda wetu anaweza kuwa Pundamilia japo kwa muda na rangi aipake Amunike.

Tukishafuzu tujipange na kutumia hawa vijana wanaofanya vyema kwenye timu za vijana na kuwakilisha Taifa letu. Kwa sasa mwanga nauona kabisa, ni nia, nguvu na imani ndo filisofia pekee inayoweza kutufikisha. Si tuliona wenyewe balaa la Mwantika. Alipakwa rangi kidogo tu akafanana na Michael Essien. Tusonge Mbele Amunike, uwanja wa Taifa tutakuletea jeshi na ndio kazi ya Media.