Ester Bulaya: Mwanamke asiyeogopa mikikimikiki ya kisiasa

Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema) Ester Bulaya

“Siogopi kuburuzwa mahakamani kwa sababu ya kusimamia ukweli na kutetea haki” Ni maneno ya mbunge wa Bunda Mjini (Chadema) Ester Bulaya ambaye mara kwa mara amekuwa akikumbwa na misukosuko ikiwamo kushikiliwa na polisi na kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma mbalimbali.

Bulaya ambaye ni mbunge kwa vipindi viwili awali alipata fursa hiyo kupitia chama tawala cha (CCM) mwaka 2010 na awamu iliyofuata alitimkia Chadema na kuwania jimbo la Bunda Mjini ambako alimshinda mwanasiasa mkonge aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo ya Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.

Tofauti na alivyokuwa chama tawala Bulaya akiwa Chadema amekuwa akifanya saisa za mikikimikiki jambo linalosababisha mara kwa mara kujikuta mikononi mwa polisi kisha kufunguliwa mashtaka mbalimbali yakiwamo ya uchochezi.

Bulaya pia amewahi kuadhibiwa na Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge na kumtia hatiani yeye pamoja na wabunge wenzake sita kwa makosa mbalimbali ikiwamo kudharau madaraka ya Bunge.

Katika adhabu hiyo Bulaya pamoja na mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu waliadhibiwa kutokuhudhuria vikao vilivyobaki vya mkutano wa tatu na vikao vyote vya mkutano wa nne.

Wengine waliokubwa na adhabu hiyo ni pamoja na Pauline Geku, Halima Mdee, Zitto Kabwe, Godbless Lema ambao walitakiwa kutohudhuria vikao vyote vilivyobaki vya mkutano wa tatu huku John Heche akitakiwa kutohudhuria vikao 10 vya mkutano wa tatu

Kwake Bulaya misukosuko hiyo haimtishi na badala yake anadai hakuna kitu kinachompa faraja kama atateseka au kuathirika kwa sababu ya kazi yake ya siasa aliyoamua kuifanya.

“Mimi ni mwandishi wa habari hata kama leo nisingekuwa mbunge bado ningetumia kalamu yangu kusema, Siwezi kufa kibudu ni bora niseme,” anasisitiza Bulaya.

Bulaya anasema inamsikitisha anapoona baadhi ya viongozi wamevimbiwa madaraka na kutekeleza yasiyofaa kwa kuogopa kupoteza madaraka.

“Mifano ipo mingi unakuta kiongozi huyo kabla hajateuliwa alikuwa akitumia majukwaa ya vijana kutetea masilahi yao lakini baada ya kuteuliwa lugha inabadilika anaongea asichokiamini.”

“Wakati mwingine ukikaa nao hata wao wanalalamika, wanatuomba tuwasaidie kusema, lakini wakisimama hawawezi wamekuwa ndumilakuwili,” anaongeza.

Bulaya anasema ataendelea kupigania anachokiamini na haogopi kupoteza maisha kwa kuwa anataka kuweka heshima akumbukwe kwa mchango wake na siyo unafiki kwani kuwa mbunge bubu haitamsaidia.

“Nitaendelea kuwasemea wanyonge, naamini wana-Bunda bado wana imani na mimi; miaka mitatu kuna vitu vingi nimefanya nahitaji muda zaidi,” anasisitiza.

Bulaya ambaye anajigamba kufanya vizuri katika sekta mbalimbali ikiwamo maji na huduma za afya ukilinganisha na mtangulizi wake, anasema amefanikiwa hayo kunatokana na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi.

“Wabunge wanawake wanafanya vizuri zaidi kwa sababu tuna woga wa kufanya maovu na kuharibu. Angalia idadi ya wanawake wanaofanya ufisadi utagundua wanaume wanaongoza, hivyo bado hali na nia ninayo wakinipa nafasi tena nitafanya vizuri zaidi.”

Hata hivyo, Bulaya anasema kinachomtesa sasa ni jinsi hali ya kisasa ilivyo na kwamba watawala hawafuati Katiba badala yake wanaongoza kwa mihemko.

“Kila mtu anaogopa; sasa mtendaji ni mmoja tu, mawaziri hawafuati taratibu badala yake wanaangalia bosi anataka nini, Bunge linapokwa mamlaka yake demokrasia inakwenda mrama sijui tunaenda wapi? Alihoji.

Kufuatia hali hiyo, Bulaya anashauri mamlaka kuwa na uongozi shirikishi kwa kuwa mtu mmoja hawezi kufanya kila kitu hivyo wasaidizi sasa hawasemi ukweli kwa kuogofya.

Aidha, Bulaya anasema vyama vya upinzani siyo uadui na kwamba viko kwa mujibu wa Katiba, hivyo vinapaswa kuheshimiwa ili kujenga demokrasia.

“Tushindane kwa hoja lakini lazima watawala waweke Tanzania kwanza na si maslahi ya mtu au kikundi chochote.

Mambo aliyowahi kufanya

Hivi karibuni mbunge huyo ambaye ni waziri kivuli wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu aliibua sintofahamu ya formula au kikokotoo cha 1/580 kilichopo kwenye kanuni za sheria hiyo na kusema kuwa inaeleza kila mstaafu atakuwa akilipwa asilimia 25 ya mafao kwa mkupuo na asilimia 75 inayobaki atalipwa kidogokidogo kila mwisho wa mwezi kama mshahara.

Hoja hiyo iliyoonekana kutikisha vichwa ilimuibua Spika Job Ndugai na kusema kuwa Bunge halihusiki hata kidogo huku Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ikitoa ufafanuzi wa ukokotoaji wa mafao ya wastaafu kutokana na kanuni mpya za mwaka 2018.

Mbunge huyo machachari pia amewahi kuwasilisha maelezo binafsi juu ya kutokuwapo kwa mashine ya mionzi ya kansa ya kizazi kwa wanawake katika Hospitali ya Ocean Road na mwisho wa siku Serikali ilikiri na kununua pamoja na hospitali zote kubwa

Pia, amewahi kuwasirisha hoja binafsi juu ya mtandao wa dawa za kulevya na kuhoji pamoja na Sheria nzuri ya Dawa za Kulevya kupitishwa bado Rais ameshindwa kumteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya na siku mbili baada ya hoja yake Kamisha Rogers Siang’a aliteuliwa.

Bulaya pia wakati akiwa CCM alishirikiana na vijana kuandaa Sheria ya Baraza la Vijana ambako anasema katika mapendekezo yake aliyoyatoa kwa ajili ya marekebisho yalichukuliwa yote 17.