Eva, mwanamke aliyeacha ualimu kuingia katika siasa

Muktasari:

  • 2010 Mwaka ambao nilianza shu-ghuli zangu za biashara.
  • 1977 Mwaka alioza-liwa Eva wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.

Jina la Eva Mpagama si geni katika siasa za mkoa wa Dodoma na hasa katika Jimbo la Chilonwa, wilayani Chamwino.

Eva (41) maarufu kama Eva Mapambo ni miongoni mwa wanawake wanaokumbukwa katika harakati za kisiasa mwaka 2015 akiwa miongoni mwa waliotikisa katika uchaguzi wa nafasi ya ubunge jimbo la Chilonwa akitokea chama kipya cha ACT-Wazalendo.

Kama ilivyo kwa wanawake wengi, mwanadada huyu alipitia katika misukosuko mingi lakini alipambana hadi kufikia nafasi alipo ambako amekuwa kielelezo na mfano wa kuigwa.

Eva alizaliwa miaka 41 iliyopita wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma. Kitaaluma ni mwalimu ambaye hata hivyo hana mpango wa kushika chaki kufundisha darasani, bali kuelimisha jamii kupitia siasa.

Jicho lake linayatazama mambo mawili zaidi –biashara na siasa. Anasema hakati tamaa hadi ayafanikishwe. Pia, anaeleza masikitiko yake kwa wanawake wanaokata tamaa.

Katika siasa

Akiwa na umri wa miaka 30 (2007) alijiunga kwenye siasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo mwaka huohuo aligombea na kushinda nafasi ya mwenyekiti wa Baraza la wanawake mkoa wa Dodoma.

Aliendeleza harakati za kuwaunganisha wanawake wa Chadema na hata kuchangia chama hicho kupata mafanikio ya kushinda nafasi saba za udiwani (sita Manispaa na Moja Chamwino) katika mkoa ambao ni ngome kuu ya CCM.

Anasema ndani ya Chadema alifanya mambo mengi yaliyomtambulisha kwa jamii hata akawa maarufu kwenye siasa na kujiamini zaidi majukwaani.

Hata hivyo, katika mazungumzo na Mwananchi, mwanamke huyu anasema kuna jambo lilimuumiza ndani ya Chadema ambalo hawezi kulisahau katika maisha yake ndani ya siasa. Kama anavyoeleza:

Swali: Kipi kilichokuumiza

Jibu: Nilijenga jimbo kwa miaka mitano nikahakikisha najiweka vizuri na kweli nafasi yangu kushinda ilikuwa kubwa lakini kwenye siasa, we acha tu!

Swali: Kitu gani kilikutokea?

Jibu: Yaani, siku tatu kabla ya pazia la kurudisha fomu kufungwa, Chadema kiliniacha na kumteua mgombea mwingine. Ilinilazimu kuhama haraka na kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo. Huko nilishika nafasi ya pili, nyuma ya mgombea wa CCM, Joel Mwaka nikamwacha mbali mgombea wa Chadema.

Swali: Ilikuwaje ACT wakuamini haraka kiasi hicho?

Jibu: Walijua Eva Mapambo ana mtaji wa watu, hivyo isingekuwa rahisi kwao kuniacha hivihivi.

Swali: Wagombea huwa hawakubali kwa urahisi matokeo kwako ilikiwaje?

Jibu: Siasa si uadui, kinachopaswa kuhubiriwa na wanasiasa ni maendeleo ambayo kwangu naunga mkono kila mtu anayehubiri maendeleo na amani bila kujali tofauti za vyama.

Katika biashara

Swali: Kwa sasa unafanya nini na wapi

Kwa sasa ninafanya biashara zangu za mapambo ya ndani ambayo nilianza na mtaji mdogo wa kununua mapazia Dar es Salaam, nikaanza kununua nchini Uganda na hivi sasa nanunua kutoka India, China, Dubai na Uturuki.

Licha ya kilio cha wafanyabiashara wengi mimi anaona soko lipo kwa mtu anayejitambua.

Swali: Unawezaje kuchanganya biashara na siasa?

Jibu: Hapana, kwa sasa siasa nimesimama ingawa vitu hivi vinashabihiana.

Swali: Je, una mafanikio uliyopata katika shughuli zako?

Jibu: Ndiyo, yapo katika maeneo yote. Katika siasa nimejenga mtandao mkubwa unaonisaidia hata sasa katika biashara zangu. Lakini kwenye biashara nimepata mafanikio makubwa maana mtaji nilioanza nao ulikuwa mdogo sana, lakini nimeweza hata kufikia biashara za kimataifa

Swali : Nini unawaambia wanawake wenzako?

Jibu: Wanawake wasipende kubebwa wala wasiwe wepesi wa kukata tamaa kwa kila jambo, pia wawe na malengo.

Swali: Ni mwanamke gani unapenda kujifunza kutoka kwake?

Jibu: Kifupi niseme najikubali, najiamini na ningependa niwe mfano mimi mwenyewe.

Swali: Je, ukikutana na Rais John Mahufuli utamwambia nini?

Jibu: Natamani hata leo kukutana naye, lakini naomba kupitia gazeti lenu nimpongeze kwa kuwataka watu wafanye kazi, lakini namkumbusha awaamini zaidi wanawake.

Swali: Je, Wanachilonwa wakusubiri tena 2020?

Jibu: Ni mapema kusema kitu lakini niseme kuwa waendelee kumpa ushirikiano mbunge, nia iwe ni umoja na mshikamano. Wakati ukifika nitasema.

Swali: Una mapenzi na michezo, na mchezo gani unaupenda?

Jibu: Napenda muziki na hasa muziki wa rumba kutoka DRC.

Swali: Unawashauri nini vijana:

Jibu: Waache kulalamika badala yake wachape kazi bila kuchagua ilimradi iwe kazi halali na wajenge uaminifu.