Fanyeni mazoezi mepesi mtajiepusha magonjwa

Muktasari:

  • Katika kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanya na kampuni yetu, wadau wa afya na serikali leo nitazungumzia mazoezi mepesi kama moja ya nyenzo rahisi yakukabiliana na magonjwa hayo.

Wiki iliyopita usiku wa Alhamisi kulikuwa na mjadala ulioandaliwa na kampuni inayochapisha gazeti hili Mwananchi Communication Limited (MCL) ikiwa na mada kuu ‘Afya yetu, Mtaji wetu’.

Katika kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanya na kampuni yetu, wadau wa afya na serikali leo nitazungumzia mazoezi mepesi kama moja ya nyenzo rahisi yakukabiliana na magonjwa hayo.

Mfano wa magonjwa ya kuambukizwa ni pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kisukari, kiharusi na unene uliokithiri.

Magonjwa haya hutokana na mienendo na mitindo mibaya ya kimaisha ikiwamo kutofanya mazoezi au kuukalisha mwili bila shughuli za kimwili na ulaji holela wa vyakula vinavyonenepesha mwili.

Mazoezi mepesi ni pamoja na kutembea, kukimbia, kuogelea na kucheza mziki. Mazoezi haya yanapofanyika mara kwa mara angalau kwa siku tano ndani ya wiki moja.

Mazoezi mepesi hujulikana kitabibu kama Aerobic exercise, ni mepesi madogo madogo ambayo yanapofanyika husaidia kuwa na upumuaji mzuri na mzunguko imara wa damu.

Utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa mazoezi haya yanasaidia wanadamu kuishi muda mrefu hii ni kutokana na mazoezi hayo kuwakinga na magonjwa ya moyo. Mazoezi haya huwa na tija endapo mtu atayafanya kwa muda wa dakika 30-60 kwa siku kwani kipindi hiki mwili tayari unakuwa umeanza kuchoma sukari (mafuta) yaliyorundikana mwilini.

Kwa wiki moja mazoezi haya yafanyike kwa siku tano, hivyo kutoa siku mbili zakupumzika ili kuupa nafasi mwili kujikarabati na vijeraha vidogo vidogo vya ndani kwa ndani.

Kwa wale ambao umri umesogea sana na wako katika mazingira magumu wanaweza kuyafanyia mazoezi haya hata katika mazingira ya ndani ya nyumba. Mfano zoezi ambalo ni rahisi ambalo linaweza kufanyikia nyumbani ni pamoja na kuruka kamba, kuendesha baiskeli, kupanda ngazi na kushuka, kukimbilia katika mashine maalum ya kukimbilia na kucheza mziki wa haraka haraka.

Zoezi jingine rahisi linaloweza kufanyika ni la kutembea, zoezi hili linafaa zaidi kwa wale watu wazima, wanaweza kupanga kutembea kwa makundi kuanzia wawili kuendelea. Mtindo mzuri wa kutembea ni ule ujulikanao kitabibu kama Diabetic Walk, kwa Kiswahili utembeaji wa wagonjwa wa kisukari. Utembeaji huu unahusisha utembeaji wa hatua na kutupa mikono mbele nyuma.

Utembeaji wa namna hii unasaidia viungo vingi kufanya kazi hivyo kuwezesha misuli ya maeneo mbalimbali mwilini kufanya kazi hivyo kuchoma mafuta ya mwili. Pengine unaweza kuwa na majukumu mengi ya ofisini kiasi cha kushindwa kufanya mazoezi, kundi hili wanaweza kutembea katika maeneo yao ya kazini.

Wanaweza kuamua kuacha kutumia usafiri wakuendea au kutokea ofisini na kuamua kutembea pia katika umbali mfupi mfupi, mfano wanaweza kuamua kila anapotoka kazini kutembea umbali fulani.