Giroud, dakika 546 bila bao Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Giroud anakuwa mchezaji wa pili kuondoka katika fainali za Kombe la Dunia mikono mitupu akiungana na Stephane Guivarc’h.

Mshambuliaji nguli wa Ufaransa, Olivier Giroud ameweka rekodi katika Fainali za Kombe la Dunia, baada ya kucheza dakika 546 bila kufunga bao.

Giroud anakuwa mchezaji wa pili kuondoka katika fainali za Kombe la Dunia mikono mitupu akiungana na Stephane Guivarc’h.

Guivarc’h ambaye kwa sasa ana miaka 47, aliweka rekodi hiyo katika fainali za mwaka 1998 aliposhindwa kuifungia Ufaransa bao licha ya timu hiyo kutwaa ubingwa.

Giroud ameonekana kutojutia kitendo hicho na badala yake amekuwa mtu mwenye furaha akitambia mafanikio ya Ufaransa kwa kutoa matamko ya kujivunia uwepo wake katika kikosi cha kocha Didier Deschamps.

Mshambuliaji huyo hakutoa mchango wa mabao 14 iliyopata Ufaransa katika fainali hizo licha ya kucheza mechi zote ikiwemo ya fainali waliyoshinda mabao 4-2 dhidi ya Croatia.

Nguli huyo aliyecheza mechi 13 na kufunga mabao matatu katika kikosi cha Chelsea, alisema ndoto ya Ufaransa kutwaa ubingwa imetimia licha ya kushindwa kufunga bao.

Giroud mwenye miaka 31, licha ya kukosolewa, anatajwa ni mshambuliaji asilia mwenye nguvu, akili ya kushambulia na mtu hatari katika eneo la timu pinzani anapokuwa na mpira.

“Nimekuwa nikishutumiwa sana kwamba sikufunga bao, nachukulia kama changamoto kwa sababu nimekuwa nikipata ujumbe kutoka kwa watu wakinifariji na kunipongeza,”anasema Giroud.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal, anasema licha ya kutofunga bao katika fainali hizo, lakini anajivunia kutoa mchango ulioipa ubingwa Ufaransa.

Nguli huyo alianza kucheza soka ya kimataifa mwaka 2011 na amefunga mabao 31 katika mechi 81 alizocheza katika kikosi cha Ufaransa akipita mikononi mwa makocha tofauti.