Giroud azimia uwanjani, kocha Ufaransa apata kiwewe

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo aliumia katika mchezo wa kirafiki uliokuwa wa kujiandaa na fainali hizo ambao timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1

Mshambuliaji nguli Olivier Giroud, ameumia vibaya kichwa zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza fainali za Kombe la Dunia nchini Russia.

Mshambuliaji huyo aliumia katika mchezo wa kirafiki uliokuwa wa kujiandaa na fainali hizo ambao timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Mchezaji huyo wa Chelsea, ameibua hofu kama anaweza kupona kwa wakati kabla ya kuanza michuano hiyo Alhamisi wiki hii.

Giroud alitokwa damu nyingi baada ya kugongana vichwa na mchezaji wa Marekani Matt Miazga katika mchezo wa kirafiki uliopigwa juzi usiku nchini Ufaransa.

Giroud na Miazga walipoteza fahamu na wote walitokwa damu nyingi kabla ya kupata huduma ya kwanza.

Mfaransa huyo alionekana kuzidiwa na maumivu na alilala chini kwa dakika tano akitibiwa jeraha la kichwa.

Kocha Didier Deschamps, alishuhudia mshambuliaji huyo mkongwe, alitolewa kwa msaada akiwa amezungushiwa bandeji kichwani.

Tukio hilo lilitokea kipindi cha pili, lilimtoa Giroud nje ya uwanja na nafasi yake kujazwa na Ousmane Dembele.

Deschamps anasubiri ropoti ya madaktari kuona kama mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal kama atapona kwa wakati kabla ya kuanza fainali hizo.

Nahodha wa Marekani Julian Green, alianza kuifungia bao timu hiyo kabla ya mshambuliaji kinda Kylian Mbappe kusawazisha.

Ufaransa itafungua pazia la fainali hizo kwa kuvaana na Australia kabla ya kuzivaa Peru na itamaliza mechi za makundi dhidi ya Denmark.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Chelsea, baada ya kukosa namba ya kudumu katika kikosi cha Arsenal kabla ya kutimkia Stamford Bridge katika usajili wa dirisha dogo Januari ili kupata nafasi ya kuitwa timu ya Taifa.