HOJA BINAFSI: Vipindupindu vya kupindua

Muktasari:

  • Kwa mfano, sijui kwa nini watu wanakuwa na wasiwasi juu ya sheria mpya ya mahesabu ya kila aina. Inaonesha jinsi ambavyo serikali yetu tukufu ya maturufu imeiva. Tuna wataalam wetu ambao watakusanya na kuchambua na kusambua mahesabu yote bila wasiwasi, bila kuwa na kosa wala harufu yake kosa. Ndiyo maana naunga mkono hii sheria mpya mia kwa mia.

We Makengeza, nakuandikia harakaharaka kabla makengeza yako hayajakuletea matatizo. Nakujua wewe, unashindwa kuona vitu vizuri ndiyo maana ni lazima nikunyooshe mapema kabla hujaathirika na vipindupindu vya kupindua mambo kama kawaida.

Kwa mfano, sijui kwa nini watu wanakuwa na wasiwasi juu ya sheria mpya ya mahesabu ya kila aina. Inaonesha jinsi ambavyo serikali yetu tukufu ya maturufu imeiva. Tuna wataalam wetu ambao watakusanya na kuchambua na kusambua mahesabu yote bila wasiwasi, bila kuwa na kosa wala harufu yake kosa. Ndiyo maana naunga mkono hii sheria mpya mia kwa mia.

Naam. Si kama zamani ambapo mahesabu yalijaa matatizo ya ajabu sana. Kwa mfano, nakumbuka huko nyuma, wakati nilikuwa huko mahali fulani (hakuna haja ya kutaja mahali maana nisingependa kujenga chuki), basi huko, ugonjwa wa ajabu ulilipuka katika kijiji fulani. Ulivyokuwa wa ajabu wakaenda waganga wa kata, na tarafa, na wilaya, na mkoa hadi wa taifa. Wote walivamia kijiji hiki ili wajue huu ugonjwa wa ajabu ukoje, na kuuzuia usienee sehemu zingine. Ilikuwa patashika kwenye kijiji kile nakwambia hadi wanakijiji wenyewe walichoka na kuchokaga. Hatimaye baada ya kupata na kushika kila mahali, ikagundulika kwamba kumbe shida ilikuwa ni malaria kali ambayo iliingia kichwani. Wakaondoka wale waganga wote, labda akabaki wa kata tu. Mechi kwisha.

Kumbe baada ya mwezi mmoja hivi ulikuwa ni wakati wa kupeleka mahesabu ya hali ya lishe katika vijiji vyote vya wilaya ile. Wakati ule, kulikuwa na ukame mbaya sana, pamoja na ugonjwa uliokuwa unamaliza muhogo. Kwa hiyo, kila kijiji kilitoa taarifa kwamba kama asilimia 3-5 ya watoto wao walikuwa na utapiamlo mkali na wengi zaidi walikuwa na utapiamlo wa wastani. Si jambo la ajabu … isipokuwa kijiji kile cha magonjwa. Wao walitoa taarifa kwamba kwao hakuna utapiamlo kabisa. Sifuri, ziro hamna. Wacha kwanza wilaya ifurahi, kisha mkoa, kisha Serikali pamoja na shirika la watoto duniani.

Lakini wengine walisema, na sibishi nilikuwamo mimi, hebu ngoja. Kwelikweli ndani ya janga la jangwa na magonjwa ya chakula, kweli kijiji hiki kikose hata kesi moja ya utapiamlo? Basi ikabidi kufanya utafiti zaidi na kukuta kwamba kijiji kilikuwa kimechoka kuvamiwa na wataalam wa kila aina, na kupimwa, na kuhojiwa, na kuhubiriwa, na kulaumiwa, wakaona njia bora ilikuwa kutoa taarifa kwamba watoto wao wote wana afya njema ili wasisumbuliwe.

Ndiyo maana nashukuru sana kwamba leo mambo kama hayo hayawezi kutokea maana nadhani hata mimi ningekamatwa kwa kutilia shaka takwimu rasmi ambazo zilikuwa zimepitishwa hadi juu kabisa. Siku hizi hawawezi kufanya makosa kama haya.

Tuchukue mfano mwingine. Kuna stori, sijui kama ni kweli au la, lakini ilivuma enzi zangu kwamba baba wa taifa alipoenda kwenye mkutano wa kimataifa, akaitwa pembeni na shirika la chakula na kilimo duniani na kuulizwa kwa nini hataki kuomba msaada wa chakula. Akashangaa na kusema kwamba hakuna haja maana chakula kipo. Lakini, wale mabwana walimwonyesha ramani ya ukame na njaa hivyo Mwalimu aliporudi akawaita wakuu wake wa mkoa kuwauliza kulikoni. Wakamthibitishia, tena kwa takwimu kwamba hakukuwa na hali ya njaa hata kidogo. Watu wote walikuwa wanakula na kusaza. Mwalimu hakushawishika hivyo aliwatuma watu wake kufanya uchunguzi. Kumbe wakuu wa mkoa nao walikuwa na watu wao hivyo walijua mapema na hawa wa Mwalimu walipelekwa sehemu nzurinzuri hadi wakaridhika na kurudi na kusema kwamba hawa mabwana wa nje wana lao jambo. Bila shaka ubeberu uliwasumbua.

Lakini Mwalimu hakuridhika. Kwa nini wamwambie uongo? Hivyo aliwaita mapadre, na mashekhe, na wachungaji ili wamweleze na wao, wakamwambia kwamba hali ilikuwa mbaya sana ndipo chakula kikaagizwa haraka sana ili kuwanusuru na njaa.

Unaona madhambi ya enzi zile Makengeza? Lakini siku hizi utapata wapi kiongozi mbaya wa namna hii. Wanavyopenda kuwasikiliza wananchi na kujua matatizo yao, wanavyopenda kusema ukweli kuhusu hali halisi ya mikoa na wilaya zao, sina shaka kabisa. Enzi zile, sheria yetu mpya ingeleta matatizo lakini si leo maana nani ana hofu? Kila mtu anapenda kusema ukweli moja kwa moja.

Naweza kutoa mifano mingi tu ya kuonesha jinsi ambavyo sisi tumekuwa watu nambari wani wa mahesabu. Tuchukue chaguzi zetu. Nani anaweza kuwa na wasiwasi kuhusu matokeo tunayotangaziwa. Mhusika mkuu wa uchaguzi ni mhusika mkuu wa maendeleo, ya nini kurudisha nyuma maendeleo kutangaza takwimu isiyo sahihi?

Na iwapo sasa tumejaa wataalamu wa kweli na wajasiri, wanaowajibika vizuri namna hii kila wakati hata kwenye ngazi ya kijiji na kata, huku taifani tuna wasiwasi gani?

Hebu nitoe mfano wa kawaida. Mimi kwa kweli inanikera sana kuona tabia za watu wengine, eti wakiingia kwenye chumba kisafi lazima wanyanyue zulia kidogo au kuangalia nyuma ya kabati kuona kama kuna uchafu umefichika. Ni kukosa ustaarabu kabisa. Mwenye nyumba amejitahidi kujenga taswira ya usafi, ni kazi yetu kama wageni ndani ya nyumba yake kufurahia usafi ule na kushangilia, vinginevyo hatuna adabu. Uchafu ule uliofichika unatuhusu nini? Ni tabia ileile ya vipinduvipindu vya kupinduapindua.

Na nchini kwetu ni vilevile. Tumejitahidi kusafisha kila kitu, hata kuondoa uchafu wa upinzani, tumetumia pesa nyingi kuwaogesha wawakilishi wa wananchi ambao kwanza walisimama ndani ya zizi la matope matupu lakini sasa wamekubali kubadilika, wameogeshwa ili waweze kuingia katika nyumba yetu safi. Angalia mahesabu.