Hazard aziweka pabaya Chelsea, Real Madrid

Muktasari:

  • Kauli hiyo imetolewa na kocha mpya wa timu hiyo Maurizio Sarri aliyesema atapambana kufa au kupona kumbakiza Hazard.

London, England. Klabu ya Chelsea imesema kamwe Edin Hazard hawezi kutua Real Madrid kwa gharama yoyote.

Kauli hiyo imetolewa na kocha mpya wa timu hiyo Maurizio Sarri aliyesema atapambana kufa au kupona kumbakiza Hazard.

Real Madrid imekuwa ikimuwinda muda mrefu nahodha huyo wa Ubelgiji bila mafanikio, lakini msimu huu wa majira ya kiangazi imesema haikubali.

Chelsea imesisitiza licha ya mshambuliaji huyo kuwekewa mezani pauni150 milioni, lakini haondoki Stamford Bridge.

Hazard amegoma kutia saini mkataba mpya licha ya kuahidiwa mshahara mnono wa pauni 300,000 kwa wiki.

Sarri alisema Hazard hawezi kuwageuka na kujiunga na Real Madrid na matarajio yake ni kumuona akibaki Chelsea msimu ujao.

Mshambuliaji huyo alipandisha dau lake baada ya kucheza kwa kiwango bora Fainali za Kombe la Dunia nchini Russia.

Hazard aliiongoza Ubelgiji kushika nafasi ya tatu katika fainali hizo zilizomalizika Julai 15 na Ufaransa ilitwaa ubingwa.

Sarri aliyejaza nafasi ya Mtaliano Antonio Conte aliyefukuzwa, alisema haamini kama Hazard anaweza kuipa kisogo Chelsea katika usajili wa majira ya kiangazi.

Mshambuliaji huyo hayuko na kikosi cha Chelsea ambapo kimeweka kambi ya muda nchini Australia kwa maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu England.

Mshambuliaji huyo anaendelea kuponda raha nchini Hispania, baada ya kumalizika Fainali za Kombe la Dunia.

Hazard alijiunga na Chelsea mwaka 2012 kutoka Lille ya Ufaransa alikocheza kwa mafanikio kabla ya kutua Stamford Bridge.

Mchezaji huyo aliyekulia Ufaransa kabla ya kwenda Ubelgiji, alifunga mabao 36 katika mechi 147 alizocheza kwenye Ligi Kuu Ufaransa. Rekodi yake akiwa Chelsea inaonyesha alicheza mechi 208 na kufunga mabao 69.